Tanzania kuuza tani milioni moja za mahindi, unga Kenya
- Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema maofisa kutoka Tanzania na Kenya watakutana wiki ijayo kujadili kwa kina baadhi ya masuala muhimu ikiwemo mgawanyo wa chakula hicho.
- Kwa kuanzia, Tanzania itaiuzia Kenya kilo milioni 2 sawa na tani 20,000 za mahindi.
Dar es Salaam. Serikali imesema itaiuzia Kenya tani milioni moja za unga na mahindi kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kuisadia nchi hiyo jirani kukabiliana na uhaba uliopo wa chakula.
Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa timu ya maofisa kutoka Kenya na Tanzania itakutana wiki ijayo kujadiliana kwa kina kukamilisha taratibu muhimu za kufanikisha makubaliano hayo.
Bashe, ambaye aliteuliwa mwishoni mwa wiki iliyopita kushika wadhifa huo, amesema leo wakati wa majadiliano na maofisa wa Kenya kuwa tayari mamlaka zinazoshughulika na chakula nchini zimeshathibitisha uwezo wa kupeleka chakula hicho.
“Wenzetu wa Kenya wana upungufu wa chakula kama tani 1.5 milioni na tunaweza kuafford (kuwapatia) milioni moja tu. Hivyo, tumekubaliana kwa ujumla kuwauzia tani milioni moja za mahindi na unga wake ili kukabiliana na upungufu huo,” amesema Bashe.
Zinahusiana:
- Kigoma kinara usajili wa mashamba Tanzania bara
- Mnada wa Kahawa kuwanufaisha wakulima?
- Wakulima wanavyopigania bei nzuri ya mahindi Afrika Mashariki
Kwa kuanzia, kiongozi huyo ameeleza kuwa Tanzania itaiuzia Kenya kilo milioni 2 sawa na tani 20,000 za mahindi.
Hatua hiyo ya Serikali ni sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa na Rais John Magufuli na mwenzie wa Kenya, Uhuru Kenyatta ya kuuziana chakula hicho ili kuwaokoa majirani hao na bala la njaa.
Mapema leo (Julai 25, 2019) Bashe aliongoza kikao cha maofisa wa Serikali kutoka taasisi zinazoshughulikia chakula ikiwemo Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko pamoja na maofisa wa Kenya ambao ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Profesa Hamadi Boga na Balozi wa nchi hiyo nchini, Dan Kazungu.
“Tumeshakubaliana bei za unga na mahindi tutaujulisha umma hapo baadaye,” amesema Bashe ambaye awali katika kikao hicho alilisitiza bidhaa zote zitakazopelekwa Kenya ziwe zimetiwa nembo kuwa zinatoka Tanzania kwa ajili ya kuhakikisha ubora wa chakula hicho.