App ya Get a Ride ilivyojipanga kupunguza changamoto ya usafiri mikoani

August 7, 2019 1:03 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Inawawezesha watu kupata usafiri wa mkoani muda wowote kwa kutumia magari binafsi. 
  • Inasaidia pia kupunguza gharama za nauli kwa sababu inatumia mfumo wa kuomba ‘lift’
  • Ni sehemu ya kupunguza ajali za barabarani na kuongeza undugu kwa Watanzania. 

Dar es SalaamWakati watoa huduma za usafiri mtandaoni wakijikita katika miji mikubwa Tanzania, vijana wabunifu wamekuja na teknolojia mpya inayowawezesha watu kusafiri kutoka mkoa mmoja hadi mwingine kwa kutumia magari ya watu binafsi. 

Kwa sasa kampuni za Uber na Bolt ziko mstari wa mbele kutoa huduma za usafiri wa taxi ndani ya majiji ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma lakini hawana utaratibu wa usafiri wa mkoani. 

Kutokana na changamoto hiyo, vijana wa Kitanzania wamebuni programu tumishi (App) ya “Get a Ride” ambayo inamuwezesha mtu yeyote kusafiri mkoa mmoja hadi mwingine kwa kutumia magari binafsi ya watu wanaoenda katika mikoa husika. 

Lengo la kuanzishwa kwa App hiyo ni kuunganisha madereva na wasafiri ili kuwepo na mazingira ya urafiki baina ya watu mbalimbali katika safari ndefu.

App hiyo inayotumia mfumo wa watu kuomba ‘lift’ kwa madereva wenye magari binafsi kwa kulipia kiasi kidogo cha pesa au kuchangia pesa ya mafuta. 

“Bei za usafiri ni makubaliano baina ya msafiri na dereva na bei hizo ni ndogo sana ukilinganisha na bei za mabasi,” amesema Peter Kitulla, Afisa biashara na masoko wa App hiyo. 


Soma zaidi:  


App hiyo inakuwa na orodha ya magari binafsi yanayoenda mkoa husika ambapo baada ya mtu kujiunga nayo anaweka taarifa zake za msingi na jinsi anavyoweza kupata magari hayo na kuhakikisha usalama unakuwepo wakati wote.

“Mteja na dereva anaweza jiunga moja kwa moja kwa kutumia simu yake. Ili kuhakikisha usalama wa watumiaji, dereva anahitaji kupitia usajili wa mtandaoni na kisha kumalizia na kuhakikiwa ana kwa ana na ofisi za Get a ride,” amesema Kitulla.

Mbali na faida zote, App hiyo inakuwezesha kusafiri muda wowote, kukutanisha na watu wapya na kupunguza uchafuzi wa mazingira.

Hata hivyo, wadau wa usafiri wamesema kuwa mfumo huu huenda ukasaidia mambo mengi ikiwepo kurahisisha gharama za maisha na kupunguza vifo vinavyotokana na ajali za barabarani kwa sababu gari linakua na mtu zaidi ya mmoja, jambo linalofanya dereva asichoke haraka.

App hiyo inakuwezesha kusafiri muda wowote, kukutanisha na watu wapya na kupunguza uchafuzi wa mazingira.Picha| Mtandao.

Mkazi wa Dar es Salaam, Christian Kulwa amesema mfumo huo utapunguza gharama za usafiri na huenda mabasi ya kusafirisha abiria yakapunguza bei pia. 

“Kusafiri kutoka Dar hadi Arusha ni Sh40,000. Kama mfumo huu unanisafirisha muda wowote na kwa bei nafuu basi ni mfumo mzuri,” amesema Kulwa ambaye pia ni Msimamizi wa kampuni ya Lina Mills ya jijini hapa. 

Pamoja na hayo yote, mfumo huu bado haujawafikia watumiaji wa simu zinazotumia mfumo endeshi wa simu za Apple “IOS” ambapo kwa sasa watumiaji wa “Android” pekee ndio wanaonufaika na App hiyo.

Peter amesema changamoto hiyo inafanyiwa kazi na ndani ya muda mfupi, kila mtu mwenye simu janja atakuwa na uwezo wa kutumia mfumo huo.

Mpaka sasa, Get a Ride ina mwezi mmoja tangu imeingia sokoni lakini ina watumiaji zaidi ya 200. Huenda App hiyo ikarejesha kuaminiana na undugu kwa Watanzania kwa kwa kupeana lift wakati wa safari za mikoani.

Enable Notifications OK No thanks