Njia za kuepuka foleni kali ya Dar es Salaam kwa kutumia teknolojia
Dar es Salaam. Iwapo wewe ni miongoni mwa watu wanaochoshwa na foleni inayolikabili jiji la Dar es Salaam, sasa huenda ukapata ahueni kidogo. Ahueni hiyo inakuja kutokana na Google kuwa na huduma inayokusaidia kufahamu hali ya foleni katika eneo mji wako kwa kutumia programu ya kompyuta na simu ya Google Maps.
Google Maps, ambayo miaka ya nyuma ilikuwa inakusaidia tu kujua umbali na muda unaoweza kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine, sasa inaweza kukuambia hali halisi ya foleni katika barabara za eneo husika kama Dar es Salaam.
Kwa kutumia takwimu zinazozalishwa na watumiaji wa barabara wanaotumia mfumo wa kubainisha eneo (GPS), programu hiyo inaonyesha barabara unayoenda ina foleni kiasi gani na kwa kasi ipi unaweza kufika unakotaka kwenda.
Mbali na taarifa za foleni za moja kwa moja, Google Maps kwa sasa inaweza kukueleza ni muda gani mzuri kusafiri kupitia barabara mbalimbali hususan kuu na zile muhimu za jiji kama Ali Hassan Mwinyi, Nelson Mandela, Julius Nyerere, Morogoro na nyinginezo kwa kutumia tathmini ya takwimu za hali ya foleni kwa muda mrefu.
Namna ya kujua hali ya foleni kwa sasa
Kwa wanaotumia simu za mkononi ni vyema wakawa na program ya Google Maps. Kama unatumia simu ya Android mara nyingi Google Maps huwa inakuwepo lakini kama haipo hakikisha unaipakua kutoka Play Store. Hii ni pia kwa wanaotumia iPhone ambazo hutumia iOS. Wanapswa kuipakua Google Maps kupitia Apps Store.
Ifungue Google Maps ukiwa umeshawasha huduma ya GPS ili programu ijue eneo ulipo na kukusaidia kukuongoza. Tafuta uelekeo uendao mfano kutoka Tabata Segerea hadi Posta. Hapo utaona inakuonyesha barabara na hali ya foleni ikiwemo muda utakaotumia.
Hali ya foleni inaonyeshwa kwa rangi ya kijani ikiwa na maana barabara ipo shwari, njano (wastani), nyekundu foleni ya wastani na damu ya mzee ni foleni kali ambayo magari yanatembea polepole.
Kama unatumia kompyuta nenda Google andika eneo ulilopo halafu chagua ramani ili uingie kwenye huduma za ramani. Baada ya kupata Google Maps bofya uelekeo au ‘directions’ ambapo utaombwa kuweka eneo unalotaka kwenda.
Ukiweka eneo hilo kama nilivyoeleza kwenye mfano hapo juu wa kutoka Posta kwenda Segerea moja kwa moja utaonyeshwa barabara inayopendekezwa na hali ya foleni kwa rangi.
Iwapo si mwelewa wa Kiingereza unaweza kubadili lugha ya programu kuwa Kiswahili. Baadhi wataona na chati kuonyesha hali ya foleni katika eneo husika.
Kujua hali ya foleni wakati wote
Huenda bado hujatoka nyumbani na utakuwa na mizunguko mirefu ndani ya jiji hivyo unataka kujua hali ya foleni katika barabara utakazopita. Unaweza kupata historia ya foleni katika maeneo hayo ili ufanye uamuzi wa njia za kupita ili ufike haraka au utoke muda ambao takwimu zinakuonyesha foleni huwa kidogo.
Kujua historia na ufunguo wa maana za rangi kuhusu foleni, nenda kwenda menu ya Google Maps halafu chaguo trafiki kwa Kiswahili ama Traffic kwa Kiingereza. Hapo barabara zote za jiji zitaonekana na hali ya foleni ya wakati huo ikiwemo barabara utakayotumia ikiwa pana kuliko nyingine.
Hapo utakuja ufunguo wa hali ya foleni ikiwa na chaguo la “hali ya trafiki moja kwa moja” au “Live traffic” na “hali ya trafiki ya kawaida”.
Kwa kuwa unataka kujua historia chagua hali ya trafiki (foleni) ya kawaida na utaonyeshwa ufunguo wenye siku zote za juma na muda. Chagua muda wa wakati huo na siku utaona hali ya foleni inabadilika na iwapo sehemu kubwa ni nyekundu fikiri kubadili muda mwingine wa kutoka kwa kuangalia takwimu zinapokuonyesha hali ni kijani.
Kama utatakiwa kutoka muda huo basi tafuta njia mbadala ya kupita kwa kutumia msaada wa Google Maps.
Kujua habari zaidi kuhusu teknolojia na urahisishaji maisha tembelea pia ukurasa wetu wa Facebook: @NuktaTanzania na Twitter: @NuktaTanzania.