App ya Sheria Kiganjani kuiwakilisha Tanzania shindano la Seedstars duniani

August 24, 2019 9:58 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Imechaguliwa baada ya kuzibwaga startups 11 katika shinda la Seedstars lililofanyika Jijini Dar es Salaam jana. 
  • Itashiriki mkutano wa Seedstars nchini Uswisi na kushindania mtaji wa uwekezaji wa hadi takriban Sh2.3 bilioni na tuzo zingine. 
  • App ya Sheria Kiganjani ni programu tumishi ya simu inayotoa saada wa kisheria kwa njia ya mtandao. 

Dar es Salaam. Programu tumishi ya Sheria Kiganjani imeibuka mshindi wa kwanza katika shindano la Seedstars World kuiwakilisha Tanzania katika mkutano wa dunia wa Seedstars nchini Uswisi mwaka ujao na kujiweka katika nafasi ya kushindania mtaji wa uwekezaji wa takriban Sh2.3 bilioni na tuzo zingine. 

App ya Sheria Kiganjani ni programu tumishi ya simu ambayo imekua ikitoa msaada wa kisheria kwa njia ya mtandao ikiwemo kuwaunganisha wananchi na mawakili waliopo maeneo mbalimbali Tanzania

Pia inatoa elimu ya sheria ili kuondoa pengo la upungufu wa washauri wa sheria nchini.

Sheria Kiganjani ilitangazwa mshindi katika shindano hilo lililozishirikisha kampuni changa 12 kusaka kampuni bora (startups) zinazowekeza katika teknolojia, jana (Agosti 23, 2019) jijini Dar es Salaam. 

App hiyo ambayo inamilikiwa na kampuni ya uwakili ya vijana ya Extent Corporate Advisory (ECA) ilifanikiwa kuzibwaga kampuni 11 zilizoshindanishwa zikiwemo nne za Zanzibar na saba za Tanzania bara.

Startups za Zanzibar ni Zanzibar Health Innovation, Nyumbani Care, Drone Wings na Zanzibit.

Kwa upande wa Tanzania bara, startups saba zilizokuwa zikichuana na Sheria Kiganjani ni Mtabe App, MyHI, Kilimo Fresh Foods na Noobites zimefanikiwa kuingia katika fainali hiyo. Nyingine ni Nuru, EX-Africa Tanzania, na MITZ Innovations. 

Ushindi huo wa App hiyo inayotoa elimu ya sheria, unaiwezesha kushiriki mkutano wa Seedstars wa Afrika Desemba mwaka huu na ule wa dunia utakaofanyika Uswisi utakaozikutanisha startups kutoka maeneo mbalimbali duniani. 

Katika mkutano huo wa dunia, startups hizo zitachuana na mshindi wa kwanza atapata mtaji wa hadi Dola za Marekani milioni moja (takribani Sh2.3 bilioni) na tuzo zingine.


Soma zaidi: 


Mmoja wa Wabia wa ECA, Nabiry Jumanne ameiambia www.nukta.co.tz kuwa kuchaguliwa kwao kuiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo ya dunia  ni heshima kubwa hasa katika kuthamini msaada wa kisheria wanaoutoa kupitia teknolojia ya simu za mkononi. 

“Tutaiwakilisha vyema Tanzania katika hatua ya Afrika na dunia, maana kwa hatua zote zilizopita (Sheria Kiganjani) hatujapata uwakilishi katika hatua ya fainali,” amesema Jumanne. 

Amesema ushindi huo ni chachu kwao katika kuendelea kuboresha bidhaa ya Sheria Kiganjani katika vipengele vingi ili kuweza kuifanya kuwa rafiki kwa watumiaji wa chini waliopo vijijini, na wasioweza kutumia intaneti. 

“Siku si nyingi tutazindua huduma ya USSD code (meseji za kawaida) ili kwa watumiaji wa simu za tochi waweze kupata msaada wa kisheria. Hii yote ni kutokana na udhamini wa mtandao wa TIGO,” amesema.

Wafanyakazi wa App ya Sheria Kiganjani na washiriki wengine wa shindano la Seedstars wakifurahia, baada ya App hiyo kutangazwa mshindi jana. Picha| Senzighe. 

Hivi karibuni, App hiyo ilichaguliwa kuingia katika kinyang’anyiro cha tuzo za Afrika za sheria mwaka 2019 zinazotarajiwa kufanyika Septemba 6 mwaka huu Johannesburg, Afrika Kusini. 

Hii ni mara ya tano kwa kampuni ya Seedstars kwa kushirikiana na Mfuko wa Ubunifu wa Maendeleo ya Watu (HDIF) na Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania kuandaa shindano hilo Tanzania likilenga kampuni changa ambazo zimekua mstari mbele kutumia teknolojia katika shughuli zao.

Katika shindano lililofanyika mwaka jana, Tanzania iliwakilishwa na App ya NALA Money; inayomuwezesha mtu  kufanya miamala yote akiwa popote bila kusubiri muunganiko wa mtandao wa intaneti au kupanga foleni benki na kwenye vibanda vya kutolea pesa.

Enable Notifications OK No thanks