DPP aanza kuwaachia huru watuhumiwa wa uhujumu uchumi

September 23, 2019 1:32 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

DPP, Biswalo Mganga leo ametangaza utaratibu utakaotumika kuwasemehe watuhumiwa wa makosa ya uhujumu uchumi waliopo mahabusu  ambao wako tayari kukiri kosa na kurejesha fedha za Serikali. Picha|Mtandao.


  • Ni siku moja baada ya Rais Magufuli kushauri watuhumiwa hao wasamehewe kama watakubali kutubu.
  • Amefuta mashtaka ya watuhumiwa waliojiunganishia isivyo halali bomba la mafuta la Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).
  • Watuhumiwa watakaoachiwa huru ni wale ambao wako tayari kukiri kosa na kurejesha fedha za Serikali.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam imewafutia mashtaka watuhumiwa watano wa kesi ya uhujumu uchumi ya kujiunganishia bila uhalali bomba la mafuta la Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba ametoa uamuzi huo leo (Septemba 23, 2019) baada ya ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP) kueileza mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na kesi hiyo. 

Waliofutiwa mashtaka na kuachiwa huru ni Audai Ismail, Chibony Emmanuel, Roman Abdon, Amina Shaban na Zubery Ally. 

Huenda hatua hiyo ya DPP ikawa ni utekelezaji wa ushauri wa Rais John Magufuli alioutoa jana (Septemba 22, 2019) wa DPP kwenda kuwasikiliza watuhumiwa wa makosa ya uhujumu uchumi waliopo rumande ili ambao wako tayari kutubu na kulipa fedha waweze kuachiwa huru.

Dk Magufuli alisema wapo watu wamekaa ndani kwa kesi za uhujumu uchumi wa kutakatisha fedha na kukwepa kodi kwa muda mrefu anawahurumia sana kama ambavyo anawahurumia wengine.

“Kuanzia Jumatatu (Septemba 23, 2019) hadi siku ya Jumamosi ya wiki inayokuja, kama wako watu wa namna hiyo ambao wako mahabusu kwa sababu ya kesi za uhujumu uchumi ambazo zitawafanya wasitoke mapema kwa mujibu wa sheria yetu lakini wako radhi kurudisha zile fedha na kutubu kwamba hawatarudia, mimi ningeshauri watu wa namna hiyo kama sheria inaruhusu, DPP wakatoke humo ndani,” alisema Rais Magufuli jana Ikulu Jijini Dar es Salaam.


Soma zaidi: 


Wakati mahakama ikiwaachia watuhumiwa hao leo, DPP Biswalo Mganga ametangaza utaratibu utakaotumika kuwasemehe watuhumiwa wa makosa ya uhujumu uchumi waliopo mahabusu  ambao wako tayari kukiri kosa na kurejesha fedha za Serikali.

Amebainisha kuwa jambo hilo linawezekana endapo mshtakiwa mwenyewe ataiandikia ofisi yake barua kupitia kwa mkuu wa gereza ya kukiri kosa na kuwa tayari kulipa fedha.  

Amesisitiza kuwa mtuhumiwa mwenyewe ndiye anatakiwa kuandika barua na siyo kuwakilishwa na Wakili kwani Wakili anaweza kubadilika na hata mtuhumiwa kumkana kwamba hakumtuma kufanya alichokifanya.

“Utaratibu ni kwamba, mtuhumiwa mwenyewe aliyeko mahabusu anatakiwa aniandikie barua kupitia kwa mkuu wa gereza akikiri kosa na kuomba kutubu haraka iwezekanavyo na sisi tutachukua hatua,” amesema  DPP Mganga.

Huenda huo ni muondelezo wa azma ya Rais Magufuli kupunguza idadi ya watuhumiwa na wafungwa waliopo magerezani, kwani amewahi kufanya hivyo mwezi Julai mwaka huu.  

Julai 18, 2019 akiwa mkoani Mwanza, Rais John Magufuli aliiagiza Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Ofisi ya DPP kutembelea mahabusi na magereza katika mikoa yote ya Tanzania ili kubaini na kuwaachilia huru watuhumiwa wa makosa mbalimbali ambao hawajatendewa haki.

Agizo hilo la Rais alilitoa baada ya watuhumiwa zaidi ya 70 wakiwemo askari polisi wanane walioshitakiwa kwa usafirishaji wa shehena ya dhahabu kuachiwa huru kutoka katika Gereza Kuu la Butimba jijini Mwanza.

Enable Notifications OK No thanks