Unayoweza kufanya kukusaidia kuacha kuvuta sigara

September 28, 2019 5:49 am · Joshua
Share
Tweet
Copy Link
  • Njia bora ya kuacha ni kuacha mara moja siyo kuacha taratibu, lakini hii inaweza kuwa changamoto kwa wengi.
  • Ifanye nafsi yako itambue madhara yatokanayo na uvutaji wa sigara mfano kansa ya koo, kansa ya mapafu na kuziba kwa mishipa ya damu.
  • Wakati wa kuacha kula chakula bora, kunywa maji mengi na jitahidi kuoga maji ya moto ili kuondoa sumu iliyopo mwilini. 

“Afya ni mtu mwenyewe “ ni mmoja kati ya semi ambazo zinatumika kuelezea umuhimu wa afya ya binadamu.

Suala la afya ni suala la mtu mmoja mmoja. Ni dhahiri kuwa kila mtu ana maamuzi na uhuru juu ya afya yake bila kuingiliwa na mtu.  Lakini bado kuna haja ya watu kwenda shule na kusoma kuhusu afya na kupata ushauri juu ya ya maamuzi sahihi ya afya yako. 

Shirika la Afya Duniani (WHO) linatupa maana ya afya kuwa ni hali ya kuwa na utimilifu wa kimwili, kiakili na kijamii na siyo tu hali ya kutokuwa na ugonjwa. 

WHO inaeleza kuwa magonjwa mengi yanatokana na mtindo wa maisha ya watu ambao unaweza kuwa na matokeo chanya au hasi kwa afya.  

Uvutaji wa sigara na unywaji pombe kupita kiasi, ni miongoni mwa mambo yanayochochea kudhoofika kwa afya. Uvutaji wa sigara pekee unahusishwa na asilimia 80 hadi 90 ya vifo vitokanavyo na saratani ya mapafu. 

Unywaji pombe na vinywaji vikali huhusishwa na hatari ya magonjwa kama kiharusi, shinikizo la juu la damu, magonjwa ya figo pamoja na kuharibika kwa ini. 

Matumizi ya pombe na sigara yakizidi yanakufanya kuwa teja. Na zoezi la kuacha huwa gumu zaidi. Kuacha ni hiari lakini ni muhimu.

Uvutaji wa sigara na unywaji pombe kupita kiasi, ni miongoni mwa mambo yanayochochea kudhoofika kwa afya. Picha|Mtandao.

Jinsi ya kuacha kuvuta sigara

Leo tunaangalia mambo muhimu unayoweza kufanya ili uache kuvuta sigara ambazo tumesema zina madhara kiafya hasa katika mfumo wa upumuaji. 

Njia bora ya kuacha ni kuacha mara moja siyo kuacha taratibu, lakini hii inaweza kuwa changamoto kwa wengi. Ni heri kuwa na siku mbaya kadhaa kuliko kuwa na siku nyingi za kuumia. 

Mateso ya taratibu hayana raha yoyote. Amua kuacha, ukiwa na mtazamo chanya siyo hasi. 

Usiwaze namna ambavyo utaikosa raha ya sigara. Baada ya kuacha sehemu ngumu inayofuata ni siku tatu za mwanzo, baada ya siku tano watu wengi hujikuta wameanza kupunguza hamu ya kuvuta sigara.

Onyesha nia ya kuacha

Jisemeshe na nafsi yako “naamua kuacha kuvuta” uwezo wa nia ni muhimu sana katika hili. Unaposema mara nyingi unaimarisha nia yako ya kufanya hivyo. 

Nafsi yako itambue madhara yatokanayo na uvutaji wa sigara mfano kansa ya koo, kansa ya mapafu, kuziba kwa mishipa nk. Yamkini hata kwenye pakiti ya sigara unayovuta unaona ujumbe wa tahadhari. Chukua hii kama nia yako.

Kuna zaidi ya kemikali hatari 2,000 zinazopatikana ndani ya tumbaku, na 400 kati ya hizo ni “carcinogenic” yaani huhusishwa na uchochezi wa saratani. Tengeneza orodha ya sababu za kuacha sigara. Jikumbushe  kila mara kupata hamasa. 


Zinazohusiana: 


Jiepushe na vitu vinavyohusiana na sigara

Ondokana na vitu vyote ulivyonavyo vinavyohusiana na tumbaku kama makopo vya kuzimia sigara, pakiti zilizobaki nk. Kaa mbali na wavutaji kwa kadiri uwezavyo. Hii itakusaidia kutopata msukumo wa kuvuta sigara tena.

Oga maji ya moto   

Oga maji ya moto mara mbili au tatu kwa siku kwa takribani dakika 15 hadi 30. Jiachie, pumzika na furahia maisha mapya. 

Hii husaidia kuondosha sumu haraka zaidi mwilini, kwa sababu mwili wako utakuwa na mihemko mizito, kuoga maji ya moto kutasaidia kushusha hali hii na kuimarisha mzunguko wa damu.

Jinsi sumu ya “Yellow nicotine” inavyowahi kuondoka mwilini mapema sana ndivyo inavyoweza kuwa rahisi kuondosha uteja (Addiction) wa tumbaku.

Utakapoacha sigara utatambua kuwa mara nyingi utakua unatokwa jasho usiku, na kuchafua hata mashuka unayotumia yanaweza kuwa ya njano kutokana na jasho hilo. Hii ni nzuri, nikotini inaondoka nje ya mwili wako.

Ondokana na vitu vyote ulivyonavyo vinavyohusiana na tumbaku kama makopo vya kuzimia sigara, pakiti zilizobaki nk. Kaa mbali na wavutaji kwa kadiri uwezavyo. Picha|Mtandao.

Pata hewa safi na chakula bora

Kila wakati unapohisi hamu ya kuvuta, pata nafasi ya kuvuta hewa kwa kuanza na kupumua taratibu ila kwa nguvu “slow deep breathing”.  Kwa kadiri unavyopata nafasi ya kutoka nje na kuvuta hewa safi kwa kutembea hii husaidia kusafisha mwili wako. 

Nyumba yako iwe na hewa safi ili kuondosha harufu ya moshi wa sigara

Kunywa japo glasi tano hadi nane za maji kila siku. Fanya hivi katikati ya mlo mmoja na mwingine. Husaidia kuondosha sumu. Jitahidi usinywe pombe katika mda huu kwa sababu hudhoofisha nia yako na unaweza kujikuta katika hali ya mwanzo.

Kula kwa wingi matunda ya kutosha na mbogamboga, jamii ya machungwa, vitamini C husaidia kuondosha sumu mwilini, pia juisi ya karoti na ndimu. 

Wavutaji wakubwa wa sigara hupendelea vyakula vya kuchoma na vyenye viungo vingi ikiwemo nyama nk. Unaweza kuviepuka kwa muda. Vina vichochezi ambavyo huongeza hamu ya kufanya baadhi ya vitu.

Sukari pia inapozidi kwenye vyakula unavyotumia huchochea hali kama hio pia. Punguza matumizi ya sukari kipindi unachokuwa ukiacha sigara.

Jitahidi kuwa na kitu cha kufanya ili kujipa majukumu na kutokuwa “idle” muda mwingi.

Angalia mtazamo chanya wa mambo. Kuwa mtu wa malengo. Jiwekee nia ya kuwa mtu bora ili kutimiza malengo yako na kuwafurahisha wanaokuzunguka na kukutegemea. Wewe ni mtu bora na inawezekana.

Dk Joshua Lameck Sultan ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba katika Chuo cha Tiba na Sayansi Shirikishi Moshi (KCMC) pamoja na hospitali ya KCMC. Pia ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) ambapo hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.

Enable Notifications OK No thanks