Viongozi, wanaharakati watofautiana Waziri Mkuu wa Ethiopia kupata tuzo ya Nobel
Ahmed anakuwa mshindi wa 100 wa tuzo hiyo ya amani ya Nobel na atatunukiwa mwezi Disemba mwaka huu. Mshindi wa tuzo hupatiwa pia fedha taslim dola za Marekani 900,000 sawa na takribani Sh2 bilioni. Picha|Mtandao.
- Tuzo hiyo ya amani kwa mwaka 2019 imechukuliwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed.
- Ametunukiwa tuzo hiyo ya heshima kwa kufanikiwa kutatua mgogoro wa mipaka na nchi jirani ya Eritrea.
- Viongozi na wanaharakati duniani watofautiana Ahmed kupata tuzo hiyo.
Tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka 2019 imechukuliwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed kwa juhudi zake za kuimarisha amani na ushirikiano wa kimataifa, huku viongozi na wanaharakati mbalimbali duniani wakitoa maoni tofauti juu ya tuzo hiyo.
Ahmed anakuwa mshindi wa 100 wa tuzo hiyo ya amani ya Nobel na atatunukiwa mwezi Disemba mwaka huu. Mshindi wa tuzo hupatiwa pia fedha taslim dola za Marekani 900,000 sawa na takribani Sh2 bilioni.
Jumla ya washiriki 301 waliochaguliwa katika tuzo hizo zenye hadhi kubwa, washiriki 223 ni watu binafsi na kampuni 78.
Kamati ya tuzo hiyo ya Nobel imesema kuwa Ahmed ametunukiwa tuzo hiyo ya heshima kwa kufanikiwa kutatua mgogoro wa mipaka na nchi jirani ya Eritrea.
“Tuzo hiyo ina maana kuwa imetambua juhudi za washirika wanaotaka amani na makubaliano nchini Ethiopia , Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla,” inaeleza sehemu ya hotuba ya kamati hiyo iliyotolewa jana.
Baada ya Ahmed kutangazwa, viongozi mbalimbali duniani wamejitokeza kumpongeza kwa juhudi zake kuleta amani na kufanya mageuzi makubwa ya demokrasia Ethiopia.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amempongeza huku akisema kuwa “mara nyingi nimekuwa nasema kuwa upepo wa matumaini unavuma kwa kasi kubwa barani Afrika. Waziri mkuu Ahmed ni moja ya sababu za kuwepo kwa upepo huo.”
Katika taarifa iliyotolewa jana na msemaji wake, Guterres ambaye yuko ziarani Denmark amesema kuwa dira ya Ahmed imesaidia maridhiano ya kihistoria kati ya Ethiopia na Eritrea.
“Ilikuwa ni heshima kubwa kwangu kushuhudia utiaji saini wa makubaliano ya amani mwaka jana,” amesema Gutrres.
Soma zaidi:
- ATCL ilivyojitanua kimataifa
- Mambo unayotakiwa kufanya ukifika mapema ‘Airport’
- Ethiopia yavunja rekodi ya dunia upandaji miti, Tanzania ikijikongoja
Guterres amesema hatua hiyo ya kihistoria imefungua fursa mpya kwenye ukanda huo wa pembe ya Afrika ya kuweza kufurahia usalama na utulivu na uongozi wa Ahmed umeonyesha mfano bora kwa wengine Afrika na kwingineko wa kuachana na yaliyopita na kuweka mbele maslahi ya watu.
Mkataba huo wa amani kati ya Ethiopia na Eritrea ulimaliza mzozo wa miaka 20 kati yao kufuatia vita vya mpakani vya mwaka 1998 hadi 2000.
Naye Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Moussa Faki ameitaja tuzo aliyopata Ahmed kama ni heshima kubwa kwa Afrika kwani amekuwa mstari wa mbele kuhimiza amani na kuifanya Ethiopia kuwa sehemu salama ya kuishi.
It is with great pride that I congratulate Ethiopian PM @AbiyAhmedAli on being the 100th recipient of the Nobel Peace Prize for his historic peacebuiding efforts that have given the world hope at a time it needs servant leadership more than ever. pic.twitter.com/9I17iAZ4ch
— Moussa Faki Mahamat (@AUC_MoussaFaki) October 11, 2019
Shirika la haki za binadamu la Amnesty International limeeleza kuwa tuzo hiyo iwe chachu kwa Ahmed kuendelea kutatua changamoto za uvunjwaji wa haki za binadamu katika nchi yake ikizingatiwa bado kuna ubaguzi wa kikabila, lugha na makundi ya uhalifu.
Kwa upande wake, Mwanaharaki wa kisiasa nchini Eritrea, Vanessa Tsehaye, amesema katika ukurasa wake wa Twitter kuwa haoni sababu ya kusheherekea tuzo aliyopata Ahmed kwa sababu amekuwa akishirikiana na Rais wa Eritrea, Isaias Afwerki ambaye amemtaja kama dikteta anayechelewesha maendelo ya watu wake.
Tuzo za Nobel zilianzishwa na Mwanasayansi wa Sweden, Alfred Nobel mwaka 1895 ambapo hutolewa tuzo tano za; kemia, fasihi andishi, tuzo ya amani, fizikia na Fiziolojia(Dawa).