Sababu za baadhi ya vyoo vya umma kuwa na milango mifupi
- Muonekano huo ni ule ambao milango ya vyoo inabaki na nafasi ya wazi sehemu ya chini, ambapo mtu aliyepo nje anaona kwa sehemu ndani ya chumba cha choo.
- Baadhi ya sababu ni pamoja na kutoa urahisi wa kusafisha, kutumika wakati wa dharura na kupunguza gharama za ujenzi.
Huenda ukawa mmoja ya watu wanaojiuliza maswali mengi juu ya mwonekano uliopo katika vyumba mbalimbali vya vyoo vilivyopo katika baadhi ofisi, hoteli na au maeneo yenye mkusanyiko wa watu wengi.
Muonekano huo ni ule ambao milango ya vyoo inabaki na nafasi ya wazi sehemu ya chini, ambapo mtu aliyepo nje anaona kwa sehemu ndani ya choo.
Hata hivyo ili mtu wa nje amuone aliyepo ndani ya chumba itambidi ainame lakini hawezi kuonana kila kitu. Zipo sababu mbalimbali za kutumia mtindo huo wa milango ya vyoo katika maeneo husika.
Urahisi wa kusafishaji wa vyoo
Moja ya sababu zinazopelekea milango hiyo kuwa mifupi ni pamoja na kupata urahisi katika usafishaji wa vyoo kwani muda mwingine unaweza kutumia muda mrefu kufanya usafi sehemu moja kutokana na jinsi miundombinu ilivyokaa.
Lakini kwa aina hiyo ya milango ni rahisi kwa msafishaji wa choo kusafirisha bila hata kuingia ndani ya chumba cha choo.
Inaweza kutumika wakati wa dharura
Kwa milango yenye uwazi chini, ni rahisi kujua nini kinaendelea ndani na nje ya chumba cha choo na hata pale inapotokea dharura kama mtu kuugua ghafla.
Hii inasaidia watu waliopo nje kumwona na kutoa msaada haraka kabla hajapata madhara zaidi au kifo hakijamchukua. Hata mtu aliyepo ndani anaweza kupitisha mkono au hata kutoka kwa kutumia uwazi wa chini endapo amepata hali isiyo ya kama ikiwemo kitasa cha mlango kugoma kufunguka.
Moja ya sababu zinazopelekea milango hiyo kuwa mifupi ni pamoja na kupata urahisi katika usafishaji wa vyoo kwani muda mwingine unaweza kutumia muda mrefu kufanya usafi sehemu moja kutokana na jinsi miundombinu ilivyokaa. Picha|Tulinagwe Malopa.
Inaepusha watu kufanya mambo yasiyotakiwa chooni
Penye wengi kuna mengi. Baadhi ya watu wanaweza kutumia fursa ya vyoo vyenye milango iliyokamilika kufanya mambo ambayo hayatakiwi maeneo ya umma kama ngono, kutumia dawa za kulevya, kuiba na hata uharibifu wa vifaa.
Namna nzuri ya kupunguza tabia kama hizo ni kuweka milango yenye uwazi chini, jambo linalowaogopesha watu wenye nia mbaya kutimiza matakwa yao.
Milango hiyo haina gharama
Milango ya kawaida ambayo haina uwazi inahitaji ufundi wa kuiweka ili iendane na freumu za mlango ili ifanye kazi kwa ufanisi. Lakini milango yenye uwazi hauhitaji gharama kubwa kwa sababu unaweza kuifunga kwa njia rahisi.
Inapunguza gharama kwa wamiliki nyumba kwa sababu haihitaji matengenezo makubwa hata ikiharibika.
Soma zaidi:
- Hizi ndizo sababu kwanini hoteli zinatumia mashuka meupe
- Matumizi sahihi ya choo cha kukaa kukulinda dhidi ya UTI
Ni rahisi kujua kama mtu yuko ndani ya chumba
Kutokana na ukweli vyoo vya umma hutumiwa na watu wengi, milango yenye uwazi inampa urahisi mtu aliyepo nje kujua kama ndani ya chumba cha choo kuna mtu ili asimsumbue kwa sababu haja ni sehemu ya starehe ya mwanadamu.
Hata hivyo, milango hiyo inaweza kuwaletea changamoto watumiaji kwa kuwaondolea uhuru na haki yao ya faragha wanapokuwa wanatumia vyoo hivyo.
Latest