Zingatia haya unaponunua ‘earphone’

October 25, 2019 5:00 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Zingatia teknolojia iliyotumika kuzitengenezea.
  • Jiandae na gharama kwani kizuri hakiuzwa kwa bei ndogo.
  • Fanya utafiti kufahamu kile unachokitaka na kile unachomudu.

Dar es Salaam. Pembezoni kidogo mwa stendi ya Makumbusho, duka la vifaa vya kielektroniki linaonekana kujazwa bidhaa za kielektroniki huku ikimuwia vigumu mtu alie nje kumuona hata muuzaji kwani kila pande ya duka hilo lina bidhaa kiasi cha kukosa pakuegemea.

Upande mmoja wa duka hilo umepangwa spika za masikioni za kila aina na ni hakika mtu anayeenda kununua bidhaa hiyo lazima apate kigugumizi cha maamuzi.

Tofauti na miaka ya nyuma kwa sasa spika za masikioni zinapatikana hadi kwa Sh4,500 tu na kuendelea kula midundo mbalimbali kutoka kwenye simu na vifaa vingine vya muziki.

Pamoja na unafuu wa vifaa hivyo, kuna masuala gani ya kiafya yanayohusiana na ubora wa vifaa hivyo vya kielektroniki maarufu zaidi miongoni mwa vijana?

Mtaalamu wa masuala ya afya, Dk Joshua Sultan ambaye ni daktari wa mafunzo kutoka Chuo cha Tiba na Sayansi Shirikishi Moshi (KCMC) amewahi kuiambia Nukta kuwa kusikiliza muziki na mengineyo kwa spika za masikioni sio shida. Shida inaanzia kwenye muda unaotumika na zaidi, teknolojia inayotumika na msikilizaji.

Kutokana na namna zilivyotengenezwa kwa kutozingatia masuala mengi ya kiafya lakini watu wengi wanaonekana wakikata mitaa wakiwa wamevalia vifaa hivyo vya bei rahisi masikioni mwao bila ufahamu wa madhara yake.

Soma zaidi juu ya madhara ya spika za masikioni hapa

Kwa kuzingatia hilo, Nukta inakuletea baadhi dondoo za kuzingatia wakati unanunua spika za masikioni ili kuhakikisha zinalinda afya yako:

1. Uwezo wa kukabiliana na kelele

Mtu hulazimika kuongeza sauti ya simu yake pale anapokuwa kwenye sehemu zenye kelele kama soko na hata usafiri wa umma. Kwa kufanya hivyo anatesa ngoma yake ya sikio kwani sauti anayoweka ili kuepuka kusikia kelele za nje  inaweza zielemea ngoma za sikio.

Mtaalamu wa masuala ya teknolojia Emmanuel Evance amesema teknolojia hii inapatikana kwenye spika za masikio ambazo huwa na king’amuzi (sensor) ambayo huondoa mawimbi ikinasa kelele za nje. Ving’amuzi hivyo  hupooza kelele hizo na hivyo mtumiaji wake kutokusikia kelele yeyote.

Baadhi ya earphones zenye teknolojia hii ni pamoja na Bose QuietComfort 20 (Sh574,400), Audio Technica ATH-ANC23 Quietpoint (Sh112,582), na Bang & Olufsen H3s ANC inayouzwa kwa wastani wa Sh 390,00.

Hata hivyo, licha ya ubora wa teknolojia hiyo, changamoto yake ni kutokuonekana kwa urahisi pale mtu anapokuwa amezivaa. Picha| Mtandao.

2. Urahisi wa kuonekana.

Teknolojia ya Earbuds imekuja kwa kishindo. Hata hivyo, licha ya ubora wa teknolojia hiyo, changamoto yake ni kutokuonekana kwa urahisi pale mtu anapokuwa amezivaa na upo kwenye mazingira yenye watu ambao huenda wasijue kama umevalia spika za masikio. ​

Katika kufanya manunuzi yako ya earphones utakazo zitumia kwenye umati wa watu, ni vyema ukachagua zile zenye waya ili kuepusha usumbufu kwa kuwa mtu akiona waya anajua kuwa unatumia teknolojia hiyo.

3. Fanya utafiti na jua kile unachokitaka.

Zipo kampuni nyingi zinazotengeneza earphones lakini kupitia kufanya utafiti unaweza ukajua makampuni ambayo yanatoa teknolojia hiyo ikiwa na ubora.

Zipo tovuti nyingi za teknolojia ambazo zimefanya majaribio ya earphones na kuziainisha ubora na changamoto zake. Unaweza kupitia tovuti kama Consumer report, The Verge na zingine nyingi ili kujua kipi ni bora na kipi unaweza kumudu.


Zinazohusiana


Hata hivyo, yapo mambo mengine mengi unayotakiwa kutokuyafanya ukiwa unatumia teknolojia hii yakiwemo kuzitumia sehemu zenye watu wengi na hata kuzivalia wakati wa mazoezi ya nje.

Kama ilivyosemwa awali na Dk Sultan ni vyema kupunguza muda wa kutumia vifaa hivyo kwa kuwa hata kama zina ubora, kuzitumia kwa muda mrefu mfululizo siyo jambo la busara na jema kwa afya ya masikio.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW