Yaliyochangia uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 7.2 robo ya pili 2019

October 28, 2019 1:59 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Umekua kwa wastani wa asilimia 7.2  katika robo pili ya mwaka 2019 kutoka asilimia 6.1 kipindi kama hicho mwaka 2018. 
  • Ukuaji huo umechangiwa zaidi na shughuli za ujenzi, madini, habari na mawasiliano.
  • Shughuli za uzalishaji; umeme, gesi na usambazaji wa viyoyozi; na usafiri na uhifadhi zimeporomoka katika uchangiaji wa pato halisi la Taifa. 

Dar es Salaam. Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema kuwa uchumi wa Tanzania unaendelea kuimarika baada ya kukua kwa wastani wa asilimia 7.2 katika robo pili ya mwaka 2019 kutoka asilimia 6.1 kipindi kama hicho mwaka 2018 ukichangiwa zaidi na shughuli za ujenzi, madini, habari na mawasiliano.

Kwa mujibu wa ripoti ya pato la Taifa ya robo ya pili ya mwaka 2019 (Aprili-Juni) inaeleza kuwa shughuli za ujenzi ndiyo zilikua kwa kiwango cha juu zaidi katika kipindi hicho kwa asilimia 19.6 huku zikiongoza kwa kuchangia kwa sehemu kikubwa ukuaji wa pato halisi la Taifa (Real GDP).

Ujenzi huo ulihusisha makazi, majengo ya ofisi, maduka, madaraja, reli na maeneo ya kutolea huduma za umma. 

“Shughuli hii ilirekodi ukuaji wa asilimia 19.6 katika robo ya pili ya mwaka 2019, ikilinganishwa na asilimia 5.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2018,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo. 

Serikali inaendelea na ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge Railway (SGR)) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro itakayogharimu Dola za Marekani bilioni 1.2 (Sh2.7 trilioni) ikiwa ni sehemu ya mradi wa kilomita 1,219 hadi Mwanza.


Soma zaidi:


Sambamba na hilo imekarabati reli ya kati hasa katika njia ya kuelekea mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania, upanuzi wa bandari ikiwemo ya Dar es Salaam ili kuongeza kasi ya upakuaji wa mizigo inayoingia na kutoka.

Shughuli nyingine zilizochangia kwa kiwango kikubwa katika ukuaji wa pato halisi la Taifa katika robo ya pili ya mwaka huu ni madini na uchimbaji kwa asilimia 17.2, habari na mawasiliano (10.3) na usambazi wa maji  uliochangia kwa asilimia 10.

Miongoni mwa sekta zilizoporomoka katika uchangiaji wa ukuaji wa pato halisi la Taifa katika kipindi hicho cha mapitio ni shughuli za uvuvi ambazo zimeshuka zaidi ya mara mbili kutoka asilimia 12.8 katika robo ya pili mwaka jana mwaka 2017 hadi asilimia 5.3 mwaka huu.

Sekta zingine ambazo kasi ya ukuaji imeshuka katika uchangiaji wa ukuaji wa pato la Taifa ni uzalishaji; umeme, gesi na usambazaji wa viyoyozi; na usafiri na uhifadhi. 

Enable Notifications OK No thanks