Kutana na mwanadada wa miaka 26 anayeongoza taasisi ya kuwainua wasichana kiuchumi Tanzania

November 7, 2019 7:59 am · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link

Lydia akiwa katika masomo yake ya elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), yeye na wenzake  waliamua kuanza kuwasaidia wasichana kwa kuendesha warsha pamoja na matamasha yaliyolenga kuelimisha na kumuunga mkono mwanamke kwa ujumla. Picha | Mtandao.


  • Ni mhitimu wa chuo kikuu anayeongoza taasisi ya ‘Her Initiative’ inayofanya kazi kwa lengo la kumkomboa mtoto wa kike dhidi ya ukatili wa kijinsia.
  • Alikuwa na ndoto ya kuwasaidia wanawake tangu akiwa shule ya msingi.
  • Utoaji wa elimu kwa wasichana, kuwasaidia kuanzisha miradi ya kiuchumi ni njia zinazotumiwa na taasisi hiyo.

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea na mikakati ya kuzuia na kukomesha ukatili wa kjinsia kwa wasichana, baadhi ya taasisi nao wanatumia mbinu mbalimbali ili kuhakikisha mtoto wa kike anakuwa huru ili kutimiza ndoto zake ikiwemo kuelimika na kupata fursa za kiuchumi.

Lakini wapo wanawake ambao hawasubiri kufanyiwa kila kitu, bali wanachukua hatua kuwasaidia wasichana waliopo shuleni kujitambua na kuinuka kiuchumi. 

Lydia Charles (26) ni miongoni mwa wanawake hao ambaye  katika safari yake ya kupata elimu kuanzia elimu ya msingi mpaka masomo yake ya elimu ya juu, alibaini kuwa ukatili wa kijinsia kwa wasichana unasababishwa zaidi na ukosefu wa kipato cha kujikimu kimaisha au kuanzisha miradi ya kiuchumi. 

Katika kutatua changamoto hiyo, Lydia akiwa katika masomo yake ya elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), yeye na wenzake  waliamua kuanza kuwasaidia wasichana kwa kuendesha warsha pamoja na matamasha yaliyolenga kuelimisha na kumuunga mkono mwanamke kwa ujumla.

Hata hivyo, mwaka wakaamua kuanzisha taasisi inayojulikana leo hii kama ‘Her Initiative’ iliyoanza mwaka 2012 inayojikita katika kuwasaidia wasichana kujikwamua kiuchumi ili wafikie ndoto za elimu na kujitegemea.

“Sikuwahi kujua kama nitakuja kuanzisha taasisi ya Her Initiative, ni kupitia matamasha na warsha mbalimbali zilizohusu kumpigania msichana na kumuelimisha ndiyo zilifungua watu macho na kunishauri kwamba naweza kuanzisha kitu kikubwa zaidi kwa lengo moja la kumwezesha mtoto wa kike” amesema Lydia.


Soma zaidi:


Mbinu zinazotumika na taasisi ya ‘Her Initiative’ katika kumwezesha mtoto wa kike kujikwamua kiuchumi ni utoaji wa elimu juu ya mbinu wanazoweza kutumia katika kukuza kipato chao na kujikinga na tatizo la unyanyasaji wa kijinsia.

Pia kuwasaidia kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi inayoweza kuwaingizia kipato na kuwaunganisha na taasisi mbalimbali zinazoweza kuchangia katika maendeleo ya msichana kwa ujumla.

Moja ya programu wanayotekeleza ni ‘Panda’ inayolenga kuwajengea uwezo wasichana wa umri wa kati ya miaka 18 hadi 25 kuwa na tabia za kuwa huru kifedha kwa kuwapata maarifa na ujuzi. 

Her Initiative imefanikiwa kubadilisha maisha ya wasichana wengi kwa kuwasaidia kujitegemea na wengine kuweza kuanzisha miradi na biashara zao ambazo kwa sasa zinawaingizia kipato kizuri na kuwasaidia katika changamoto mbalimbali za kimaisha. 

Hata hivyo, Lydia na timu yake bado wana kibarua kigumu kuwafikia wasichana waliopo katika maeneo mbalimbali nchini, ikizingatiwa kuwa kwa sasa wako katika mikoa wa Dar es Salaam.

Enable Notifications OK No thanks