Kanuni 1: Hewa safi inavyoshikilia uhai wa maisha yako

November 30, 2019 9:56 am · Joshua
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kinga ya magonjwa mbalimbali kwa binadamu.
  • Unywaji wa maziwa siyo suluhisho la kusafisha hewa mwilini. 
  • Kaa katika mazingira yanayokuwezesha kupata hewa safi kila wakati.

Maisha ya binadamu yanaongozwa na kanuni ambazo zinasaidia kuweka mambo sawa na kupunguza athari  zinazoweza kutokea kama hakuna utaratibu ambao jamii imekubaliana kuufuata. 

Hata katika masuala ya afya hasa inayomuhusu binadamu, nako kuna kanuni zake ambazo zikizingatiwa kwa usahihi, dunia itakuwa sehemu nzuri ya kuishi. Nakuletea mfululizo wa makala haya ya kanuni nane za afya ambazo ni muhimu kuzingatia.

Ilikua mwaka 1875 katika jiji la Paris nchini Ufaransa. Kwa zaidi ya miaka miwili wanasayansi watatu walikua wanafanya juhudi kufanikisha jaribio lao la kwanza la kisayansi. 

Wanasayansi hao walitengeneza maputo makubwa kwa lugha maarufu “air balloons”  ya kuelea angani na walikuwa wanataka kuweka rekodi mpya ya kupaa kwa kiwango cha juu zaidi kutoka usawa wa bahari. 

Walifanikiwa katika hilo, walitaka kupaa juu zaidi lakini kwa gharama ipi? Taratibu kwa kadiri puto lile lilivozidi kwenda juu na abiria wake watatu ndani. Walipofika futi 24,430, wawili kati ya watatu walikua hoi bin taabani lakini bado walikua na shauku ya kufika kimo cha juu zaidi. 

Lakini ilipofika futi 28,000 sawa na mita 8,600 kutoka usawa wa bahari,  mmoja wa mwanasayansi aliwaona wenzake wawili wakiwa chini wamelala, wafu. Ndiyo waliifikia rekodi , lakini ni katika umauti. Hapakua na hewa ya kutosha katika kimo hicho, hewa ya uhai ya oksijeni haikupatikana tena.

Bila hewa binadamu hufa. Hewa ni elementi muhimu ya binadamu na wanyama wote. Mtu huweza ishi kwa wiki kadhaa bila chakula, au kwa siku kadhaa bila maji lakini akikosa hewa hufa ndani ya dakika chache tu. 

Ili tuwe na damu nzuri yenye afya ni kupumua vizuri. Hii hufanya mapafu yapokee hewa ya kutosha na kuipa damu oksijeni ya kutosha ambayo hurutubisha tishu mbalimbali za mwili ikiwemo neva. 

Husaidia kutengeneza hamu ya kula na hata kuchakata chakula mwilini. Kama oksijeni haitoshi, damu hutembea mwilini pasipo na mashiko, uchafu na taka sumu ambazo zingetolewa nje na hewahujazana mwilini na kuleta kadhia mbaimbali za kiafya. 

Kila seli ndani ya moyo wako inahitaji hewa safi na ya kiwango chenye oksijeni ya kutosha kulingana na matumizi yake.

Uvutaji wa hewa chafu ni hatari kwa afya yako. Picha|Mtandao.

Umuhimu wa hewa safi mwilini

Ni muhimu kuwa na nyumba au chumba chenye mzunguko mzuri wa hewa safi na ya kutosha. Hewa chafu huuchosha mwili maana inaupa mwili kazi ya ziada na kufanya tishu muhimu kukosa oksijeni ipasavyo. 

Hii hupelekea kuwa na ufikiri duni pamoja na msongo wa mawazo. Iwe mchana, iwe usiku hakikisha kuna mzunguko bora wa hewa ndani ya eneo ulilopo.

Ukiwa na changamoto kupata usingizi usiku, unaweza jaribu zoezi hili dogo tu, fungua madirisha hakikisha kuna hewa ya kutosha inayoingia ndani ya chumba unacholala. 

Acha hewa izunguke ndani ya nyumba yako. Katika hali ya kawaida utashangaa utakapopitiwa usingizi. Hii ni kwa sababu hewa ya kutosha inaingia ambayo inafanya upumuaji wako ufanyike na uipatie damu yako oksijeni ya kutosha kurutubisha seli zako na tishu za mwili wako. 

Itakusaidia kuondoa mkazo pamoja na sonona na kukupa usingizi mwanana. Unapoianza asubuhi yako, mara uamkapo vuta pumzi nzito ukiwa kitandani kisha simama jinyooshe na taratibu vuta pumzi ndefu ndani siyo juu ya kifua au mapafu yako kisha achia taratibu. 

Hii husaidia kuongeza uwezo wa mapafu yako kuchukua hewa. Fanya hivi mara tano au sita. Fanya hili zoezi joni umalizapo kula pia. Toka nje ya nyumba yako kisha vuta pumzi ndefu na pumua ukiweza hata mara 18.

Usikae muda mrefu eneo lenye moshi wa sigara hata kama ni rafiki zako. Washauri umuhimu wa kuacha sigara. Tafuta sehemu yenye hewa safi. Hewa ni tiba.


Zinazohusiana: 


Epuka harufu kali na gesi hatari, hewa inapokua imechafuka huhamisha takataka zote hizi na kuziweka mwilini mwako. Uvutaji wa hewa safi ni msingi muhimu katika kujenga afya ya mwili wako. 

Jitahidi hata unapojenga au unapotafuta mahala pa kuishi pawe ni sehemu isiyo na msongamano pia isiwe nyumba iliyobanana na kuwa na mzunguko mdogo wa hewa. 

Ukiweza unapokuwa kwenye foleni, funika pua yako kwa kitambaa laini. Lakini kwa sababu hili ni jambo gumu, unapofika eneo lenye msongamano mdogo wa watu au maeneo ya makazi, fanya zoezi la kupumua ili kutoa ile hewa chafu iliyojazana mwilini mwako.

Mafundi wa viwandani nao inahusu

Mafundi ambao hufanya kazi na rangi ama viwandani, ni vizuri kufunika pua zao kupitia vifaa maalumu “face masks” ili kuepusha kuvuta hewa hizi ambazo huathiri kwa kiasi kikubwa mapafu. 

Ikumbukwe kuwa kunywa maziwa baada ya kuvuta hewa chafu hakuna msaada wa moja kwa moja kama baadhi ya mafundi wengi hufanya. 

Tambua kuwa sumu ile huingia katika mfumo wako wa upumuaji kisha katika damu. Maziwa huchakatwa kama chakula tumboni na kutunzwa. Kuikinga wakati wa kazi ndiyo uchaguzi sahihi. Na hiii ndiyo kanuni ya kwanza ya afya. Je kanuni ya pili ni ipi? Usikose muendelezo wa makala haya wiki ijayo.

Dk Joshua Lameck Sultan ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba katika Chuo cha Tiba na Sayansi Shirikishi Moshi (KCMC) pamoja na hospitali ya KCMC. Pia ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) ambapo hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.

/
No matches found for this filter
No forex gainers today
No forex losers today
25 May, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
25 May, 2026
No active movers today
Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
MIKOA 5 YA KIPOLISI INAYOONGOZA KWA MAKOSA BARABARANI

MIKOA 5 YA KIPOLISI INAYOONGOZA KWA MAKOSA BARABARANI

Nukta TV

SERIKALI YAKAMILISHA MAZUNGUMZO MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA

SERIKALI YAKAMILISHA MAZUNGUMZO MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA

Nukta TV

🔴LIVE: KAPINGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA 2026/2027 BUNGENI.

🔴LIVE: KAPINGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA 2026/2027 BUNGENI.

Nukta TV