Kwanini ni muhimu kupambana na hofu

November 17, 2021 3:28 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Kupambana na hofu yako kutakujengea uthubutu, huruma na ushujaa.
  • Inashauriwa kutokutabiri matokeo na kusimama hata unaposhindwa.

Dar es Salaam. Sidhani  kama yupo mtu ambaye hana hofu duniani. Kama yupo basi hongera zake. 

Kwa wengine hofu zao ni kujaribu mambo mapya, wengine ni kuelezea hisia zao na baadhi, kutoka nje ya boksi lao ni kazi ngumu kama ilivyo kuvuka bahari ya hindi kwa mtumbwi.

Wasichokijua wengi ni kuwa kushindwa kupambana ana kwa ana na hofu zako kunakunyima kukua na hata kufungua milango mipya ya talanta zako.

Msaikolojia na mtoa ushauri, Dk Kurt Smith ameandika kwenye ukurasa wake wa mediumkuwa hofu ni hisia ya kawaida na ni muhimu pia. Na kwa ambaye anadai hana hofu na hakuna kinachomtisha ni aidha anadanganya au hayupo sawa kisaikolojia.

Katika kupambana na hofu zako, ni muhimu kufahamu baadhi ya vitu ikiwemo uwezekano wa kutokufanikiwa kwa haraka na kusitasita kufanya jambo. 

Lakini kubwa zaidi ni kuwa, kupambana na hofu zako ni hatua muhimu katika ukuaji binafsi.

Kuna faida gani za kukutana na hofu zako ana kwa ana yaani “man to man”?

Mapambano dhidi ya hofu yako ni yako wewe mwenyewe. Picha| Home Dialysis Central.

Kujenga uthubutu ndani yako

Kwenye kundi la rafiki zako, huenda yupo yule ambaye anasifika kwa kufanya maamuzi magumu muda wote. Yule ambaye anafanya vitu ambavyo wengine wote wanaogopa kufanya.

Unaweza kuiweka kwenye ngazi ya familia, pale nyumba inapovamiwa, inategemewa baba wa familia kusimama kifua mbele kuilinda familia na kama baba hayupo, mama alinde watoto wake.

Muktadha huo pia upo kwenye maisha ya kila siku. Pale hofu inapokuja, inahitaji ukusanye nguvu zako zote tayari kwa kuishinda hofu hiyo. 

Ushindi wako utakufanya hofu nyingine zinazokuja mbeleni uzione kawaida na hivyo kuwa na uthubutu. Pale hofu ikikushinda, itakuwa ni ngumu kwa wewe kutoboa anga kwa kile unachohofia.

Mfano, kama unaogopa kujitetea kwa mtu anayekuonea, unamruhusu aendelee kukuonea hadi atakapochoka. Ukithubutu kujitetea, itakupa nguvu ya kuendelea kujitetea kila mara unapoonewa.


Ni mwanzo wa ujenzi wa hekima na kupata uzoefu

Waswahili wanasema ‘nyani mzee amekwepa mishale mingi.’ Angewezaje kuikwepa mishale hiyo kama angelikaa chini na kusubiri upepo uipeperushe? Bila shaka nyani huyo alisimama na kuikimbia mishale hiyo akiruka mti kwa mti.

Kwa maisha ya sasa, kadri unapoishinda hofu yako unapata hekima juu ya ulichokishinda. Unaweza hata kuwa na nguvu ya kumshauri mtu cha kufanya pale anapokuja kukuelezea changamoto kama uliyowahi kuipitia.

Lakini endapo hautoishinda hofu yako, huenda changamoto yako ikakushinda na ukaishia kumkatisha tamaa mtu kwa kumwambia “hapo rafiki yangu hata sina cha kukushauri, mwenyewe nimeshindwa” pale anapokuja kwako akitarajia kupata msaada.

Mshauri wa ujasiriamali kutoka tovuti ya Entrepreneur, Matthew Toren amesema mara zote hekima hutokana na uzoefu wa kukabiliana na hofu.

Ni chaguo lako. Pale inapokulazimu kupambana na hofu yako, unaweza kuchagua kukimbia au kukunja mkono wa shati lako na kupambana mkono kwa mkono hadi uishinde hofu yako.

Pale hofu yako  inapoinuka, ni uamuzi wakokukimbia au kupambana nayo. Picha| PI Comms.

Kuwa na huruma na uthabiti

Hauwezi kuelewa kwanini mtu anashindwa kufanya kitu fulani kama haujawahi kutembea kwenye hatua anazokanyaga. Ni sawa na kusema, hauwezi kuyaelewa maisha ya mtu kama kiatu chake hakikutoshi.

Toren amesema, kukabiliana na hofu kutamsaidia mtu kuona huruma kwa mtu pale anapokuwa anapitia kilekile alichokikabiri mwanzo. Pia, unakuwa na uthabiti wa jambo kuwezekana kufanyika.

Mathalan, kama haujawahi kuua nyoka hata mara moja, utawezaje kumuua ukikutana naye, au hata kujua sehemu ya kumpiga ili nyoka huyo ajumuike na wahenga wake? Kama umewahi kumua, ni rahisi kumwambia mtu “mpige kichwani” na nyoka akafa.


TANGAZO


Utawezaje kuwa na uthubutu?

Haihitaji sayansi ya kupaisha roketi angani kupambana na hofu zako. Japo siyo rahisi kama ninavyoandika lakini inawezekana na safari hiyo itakufundisha yale mwalimu wako alipitiwa kukufundisha darasani.

Hakuna mtu anayeweza kukushika mkono kwenye safari hiyo, ni wewe tu na Mungu wako.

Kufikia huko, unatakiwa kuweka umakini wako kwenye kufikiria jinsi gani utayafurahia matokeo ya kuishinda hofu yako iwe ni ya kusema ukweli na hata yoyote.

Pia, unatakiwa kuachana na kutabiri kitachotokea. Mfano kama unashindwa kutoka nje usiku, kushindana na hofu hiyo, acha kutabiri mambo kama “itakuwaje kukiwa na fisi” ua “itakuwaje” yoyote itakayokuja kichwani kwako.

Jingine ni  kutarajia kushindwa. Hakuna mtu aliyewahi kufanikiwa ambaye alifanya  jambo biila kushindwa. Unatakiwa kujua kuwa, kushindwa kupo na ni kawaida. Cha muhimu ni  kile unafanya baada ya kufeli. Je, utaamka kupambana tena au ndio utakuwa mwisho wako?

Ninarudia tena, siyo kitu rahisi kama livyo kukoroga sukari kwenye chai lakini amini kwamba, matokeo yake utayafurahia.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW