Bodaboda zinavyochangia matatizo ya macho, upofu
- Kutumia usafiri wa bodaboda kunakukutanisha na upepo ambao unaweza kukusababishia changamoto za macho.
- Kati ya changamoto hizo ni kuona kwa shida, kupata magonjwa ya macho na upofu.
- Wataalamu wanashauri kutumia kofia ngumu zenye kiziba uso.
Dar es Salaam. Kutokana na foleni, haraka au hata mapendeleo, baadhi ya watu hasa katika majiji makubwa kama Dar es Salaam hupenda kutumia usafiri wa bodaboda ili kukidhi mahitaji yao ya usafiri kwani usafiri huo ni rahisi na unaweza kupita katika maeneo ambayo magari hayawezi.
Licha ya umuhimu wa usafiri huo, bado umekuwa ukichangia kwa sehemu kubwa ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikiwachia watu majeraha, ulemavu na hata kuwasababishia vifo.
Wakati usafiri huo ukichangia ajali nyingi, wadau wa usalama barabarani wameendelea kutoa elimu kwa madereva na abiria kuzingatia sheria wakati wanatumia vyombo hivyo vya moto ikiwemo kuvalia kofia ngumu wakati wakitumia usafiri huo.
Hata hivyo, mbali na kushauri matumizi ya kofia ngumu, bado zipo changamoto za kiafya ambazo zinawapata watumiaji wa usafiri huo ambazo hachukua muda mrefu kuonekana.
Matatizo ya macho ambayo watu wanayapata, huenda yanachangiwa na kutumia kofia ngumu za pikipiki zisizo na kifuniko cha uso au baadhi ya watu kudharau kutumia kofia hizo.
Kama wewe ni miongoni mwa watu ambao wanapuuzia kutumia kofia au kufunika uso wakati unatumia bodaboda, basi unayaweka macho yako katika hatari kubwa ya kupigwa na upepo.
Daktari kutoka Kituo cha afya cha Ngarenanyuki cha jijini Arusha, Jonas Kaguo anasema kutumia usafiri huo kunaweka macho ya mtumiaji katika hatari kubwa kwani upepo hubeba vitu vingi ikiwemo majani, wadudu na hata mchanga ambao unaweza kukudhuru ikiwemo kukusababishia majeraha, uoni hafifu au upofu.
“Kwa safari hizi, jicho lako lipo hatarini ukizingatia pikipiki zinapita hadi kwenye vichochoro. Huko unaweza kukwaruzwa na miti au majani yake na kukupelekea hadi kufanyiwa upasuaji wa jicho,” amesema Dk Kaguo.
Hata hivyo, baadhi ya madereva wa bodaboda bado hawajui madhara yatokanayo na kutokuvaa kofia zinazofunika uso wakati wanaendesha pikipiki, licha ya kuwa wamekuwa wakikumbana na mikasa mingi. Picha| Mwananchi.
Kaguo amesema katika kituo cha Afya cha Ngarenanyuki hupokea wagonjwa kati ya 15 hadi 20 kwa mwezi wakiwa na dharula ya macho iliyotokana na usafiri wa pikipiki.
“Upepo kama upepo unasababisha jicho kuuma. Ile presha ya upepo inaharibu ile presha ya wastani inayohitajika na jicho.
“Unapokuwa umefungua jicho, unahitaji presha ya kawaida ili kuona lakini kutokana na ule upepo, jicho linapata irritation (muwasho) na kupelekea kutoa machozi,” amesema Dk Kaguo.
Kwa mujibu wa shirika la afya duniani (WHO), inakadiriwa kuwa takribani watu bilioni 2.2 wana uoni hafifu au upofu, huku watu bilioni 1 kati yao wakiwa pengine tatizo lao halijashughulikiwa au ambao ulemavu wao ungeweza kuzuilika.
Walio katika hatari zaidi ya kupata matatizo ya macho
Madereva wengi wa bodaboda wengi wanaopuuzia matumizi ya kofia, ndiyo wako katika hatari zaidi kwa sababu hukutana na upepo mkubwa zaidi kuliko abiria ambaye anaweza kujikinga kwenye mgongo wake.
Clein Shangali ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Kampasi ya Dar es Salaam (TUDARco) ambaye ni mtumiaji wa usafiri huo amesema mara kadhaa amekutana na sintofahamu wakati akitumia usafiri huo.
Mbali na kushuhudia dereva wa bodaboda akifunikwa na mfuko wa plastiki na kupoteza mwelekeo wa chombo chake, Clein amesema mchanga umewahi kuingia machoni wakati akiwa barabarani, jambo lililomuweka katika hatari ya kupata ajali.
“Bodaboda nyingi hazina Helmet (kofia ngumu) zenye kifunika uso. Hata zenye nazo, zinatumika na madereva huku abiria akipewa isiyonacho. Binafsi mchanga umewahi niingia, nilishtuka nikijiuliza kama ni mdudu au laa lakini ulikuwa mchanga. Nilimwambia dereva asimame niutoe,” amesema Shangali.
Zinazohusiana
- Tusipowasaidia, Tanzania itawapoteza bodaboda wote
- Lugola ataja bodaboda wanaopaswa kupelekwa polisi
- CHATI YA SIKU: Bajaj, Bodaboda zinavyoangamiza watu Tanzania
Kwa mujibu wa Shangali, kasi ya usafiri huu ambao mara nyingi inakuaga siyo “ya kitoto” inaweza kusababisha ajali, endapo atakayeingiliwa na vumbi, mchanga au mdudu akiwa ni dereva.
“Ni lazima ashtuke na inaweza kupelekea akapoteza mwelekeo,” anasema Shangali wakati akiongea na www.nukta.co.tz kuhusu uzoefu wake wa kutumia bodaboda.
Madhara unayoweza kupata kwenye macho yako
Kwa mujibu wa tovuti ya inayoangazia usafiri wa pikipiki ya Motorbike Writer, madhara mengine ya kutumia usafiri huu kwa muda mrefu bila kinga ya macho kunaweza kusababisha maambikizi na macho kupata ukungu (blur) kwa sababu ya kukauka kwa unyevu wa macho.
Pia husababisha kuumwa kwa kichwa kwa sababu macho ni moja ya viungo vikuu vya mwili, yanahusiana moja kwa moja na ubongo.
“Jicho linapopata upepo kwa muda mrefu, moja kwa moja unaweza kupata maumivu ya kichwa. Ni bora kutumia “helmet” kwa ajili ya kichwa,” amesema Kaguo.
Hata hivyo, baadhi ya madereva wa bodaboda bado hawajui madhara yatokanayo na kutokuvaa kofia zinazofunika uso wakati wanaendesha pikipiki, licha ya kuwa wamekuwa wakikumbana na mikasa mingi.
Kwa gharama za kawaida, helmet yenye kioo inauzwa kwa takriban Sh110,000 bila gharama za usafirishaji kupitia soko la mtandaoni la Amazon huku isiyo na kioo ikiuzwa kwa gharama ya takribani Sh69,000. Picha| SDE.
Daniel Susuma ambaye ni dereva wa pikipiki mkoani Morogoro ameiambia www.nukta.co.tz huenda shida ya kichwa anayoipata mara kwa mara nyakati za usiku ikawa inasababishwa na kutokutumia kofia yenye kioo cha kuziba macho.
“Mara nyingi usiku nasikia maumivu ya kichwa na saa zingine hata mchana hasa kama nimeenda safari ya masafa marefu. Upepo ni mkubwa sana barabarani,” amesema Susuma ambaye kofia yake haina kiziba uso.
Ufanye nini kujikinga?
Ili kuepukana na changamoto hizo, Dk Kaguo amesema ni vema kununua miwani za plastiki isiyokuwa na na kizuia jua (Sunglasses) kwa matumizi ya usafiri huu ili kujikinga na mwanga mkali wa jua.
“Siyo kila kioo unaweza kukivaa kwa afya ya jicho. Usinunue sunglasses (miwani ya jua) kwa sababu zinakupa shida nyingine tena. Jicho lako litatakiwa kutumia nguvu nyingine kujifungua ili kupata mwanga wa kutosha kuona,” amesema Kaguo.
Kwa gharama za kawaida, helmet yenye kioo inauzwa kwa takriban Sh110,000 bila gharama za usafirishaji kupitia soko la mtandaoni la Amazon huku isiyo na kioo ikiuzwa kwa gharama ya takribani Sh69,000.
Kinga ni bora kuliko tiba. Ni heri ukaingia gharama za kununua kofia yenye kiziba macho sasa, kuliko kusubiri macho yako yaharibike.
Hata hivyo, kama umepata matatizo ya macho kutokana na kutokuvaa kofia, ni vema ukamuone daktari ili upate matibabu na kuzuia kupata matatizo makubwa zaidi ikiwemo upofu.
Latest