Njia za kupunguza gharama za bili za maji nyumbani
- Njia hizo ni pamoja na kutumia mabomba banifu, kupunguza matumizi ya ndoo na kuhifadhi maji kwenye tenki.
- Kwa kuepuka matumizi ya maji yasiyo sahihi, unaweza kuokoa fedha nyingi zitakazo kusaidia kwenye shughuli zingine.
Dar es Salaam. Ni bayana kuwa maji ni sehemu muhimu ya maisha ya mwanadamu. Yanatumika katika shughuli mbalimbali za uzalishaji viwandani, mashambani na hata nyumbani.
Kwa wale wanaotumia maji ya bomba yanayosambazwa na watoa huduma kama Dawasco (Kampuni ya Usambazaji Maji Jijini Dar es Salaam) wanalazimika kulipia huduma hiyo kila mwezi ili kutumia maji katika nyumba zao.
Lakini baadhi yao wamekuwa wakishangazwa na kutofautiana kwa bili za maji kila mwezi, jambo linaloibua changamoto hasa katika ulipaji wake.
Inawezekana hufahamu kuwa zipo tabia za matumizi ya maji yasiyofaa katika nyumba yako yanayochangia kubadilika mara kwa mara kwa bili ya maji. Baadhi ya tabia hizo ni kufua au kuosha vyombo mara kwa mara.
Hizi ni baadhi ya njia zinazoweza kukusaidia kuwa na matumizi sahihi ya maji na kukuwezesha kupata bili ya maji inayoendana na matumizi halisi ya maji kila mwezi:
1. Punguza matumizi ya ndoo bafuni na bustanini
Kwa mujibu wa fundi mabomba wa jijini Dar es Salaam, Christopher Pesambili, matumizi ya ndoo mabafuni na umwagiliaji wa bustani yanasababisha matumizi makubwa ya maji.
Amesema kwa haraka mtu anaweza asigundue lakini “ukitumia bomba la mvua kuoga utatumia maji kiasi kwani linamwaga maji kwa mfumo wa mvua. Ukitumia ndoo, kopo la lita moja linaweza lisitakatishe hata sabuni iliyopo kwenye nywele.”
Pesambili ambaye ana uzoefu wa muda mrefu wa kutengeneza mabomba ya maji yaliyoharibika majumbani, anasema kama mtu akiingia chooni na kuflashi kwa maji yaliyo kwenye ndoo utatumia maji mengi kuliko yule anayetumia mfumo ya maji iliyounganishwa na matenki kuflashi maji wakati wa haja.
Unashauriwa kutumia kutumia vyoo vya kuflashi ili kuepuka kutumia maji mengi ya ndoo ili kupunguza gharama za maji kila mwezi.
Ukitumia bomba la mvua kuoga utatumia maji kiasi kwani linamwaga maji kwa mfumo wa mvua. Picha| Mybath.sk.
2. Tumia tanki la maji la akiba
Unashauriwa kuwa na matanki ya kuhifadhia maji ambayo unaweza kuyajaza maji ili yatumike kwa kipindi fulani kuliko kutumia moja kwa moja maji ya bomba.
Msoma mita wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa), Mwanahamisi Yusuph amesema kwa wafanyakazi ambao huwaacha wasaidizi wa kazi nyumbani, njia hii ni nzuri kwa sababu ukiweka maji kwenye tanki, ni rahisi kujua yametumika kwa kiasi gani kuliko kutumia moja kwa moja kutoka kwenye mita.
“Kama ukitumia tanki, ukapandisha kwa mfano maji ya uniti tatu (kipimo cha matumizi ya maji) utajua kabisa kwa mwezi kama umepandisha maji kwenye tanki mara nne, utalipia uniti 12. Tofauti na kama yakiwa yanatokea moja kwa moja kwenye mabomba ya Dawasa.
“Hii njia itakufanya ufuatilie mwenendo wa matumizi ya maji nyumbani kwani kama maji yakiisha mapema kabla ya kawaida, utajua kuwa hata matumizi yake sio ya kawaida,” amesema Yusuph.
Zinazohusiana
- Unayoweza kufanya kudhibiti matumizi makubwa ya umeme nyumbani
- Mazoezi yanayoweza kuongezea ufanisi kazini
- Namna umeme vijijini unavyoweza kutumika kuchochea maendeleo
3. Osha vyombo na fua nguo kwa makundi
Wapo baadhi ya watu ambao huosha chombo au nguo moja moja huku bomba likiwa linatoa maji mfululizo. Tabia hii inachangia kuongezeka kwa matumizi ya maji.
Mjasiriamali wa chakula na matunda wa jijini Dar es Salaam, Liberatha Respicius amesema ni vema kukinga maji kwenye vyombo vikubwa kama mabeseni au ndoo na kisha kuviosha vyombo au nguo kwa pamoja. Kufanya hivyo kutasaidia kutumia maji machache na hivyo kupunguza bili yako.
Njia hii inaweza kutumika na mabachela na wengineo kwenye kufua nguo na kuosha vyombo.
4. Kagua mabomba ya maji mara kwa mara
“Kuna nyakati zingine nilikuwa nalipia Sh100,000 kwa mwezi nikaja nikashangaa gharama imeongezeka hadi Sh132,000 vijana nyumbani wakaanza kunilalamikia kuwa ninamwagilia maji mengi kwenye bustani lakini haikuwa kweli.
“Nililazimika kuita fundi akatoa paving zote tukakuuta maji yanavuja tena yanavuja haswa,” amesema mama mazingira wa mtaa wa Amani, jijini Dar es Salaam Mama Musa.
Ukaguzi wa mifumo ya usambazaji maji kwenye nyumba yako mara kwa mara ni muhimu hasa pale unapogundua kuna mabadiliko ya bili za maji.
Yapo mabomba ambayo unabonyeza na yanatoa maji kwa muda mfupi na mtu akihitaji maji zaidi, atabonyeza tena. Mabomba haya ni tofauti na yale ambayo mtu anafungua na maji hutiririka hadi atakapo lifunga. Picha|Mtandao.
5. Tumia mabomba banifu nyumbani kwako
Mabomba banifuni yale yanayopunguza mtiririko wa maji kwa kutumia teknolojia ya kuhisi au ya kuzuia maji.
Kama ilivyoandikwa kwenye makala ya matumizi ya umeme nyumbani, njia hii ni muhimu sana kwa mtu anayejenga nyumba kwani itasaidia kupunguza bili yako ya maji na pia ya umeme.
Yapo mabomba ambayo unabonyeza na yanatoa maji kwa muda mfupi na mtu akihitaji maji zaidi, atabonyeza tena. Mabomba haya ni tofauti na yale ambayo mtu anafungua na maji hutiririka hadi atakapo lifunga.
Pia yapo mabomba ambayo yameunganishwa na mifumo ya kidijitali yenye uwezo kuhisi. Yanafanya kazi kwa kuhisi uwepo wa mtu na huzima pale hisia hiyo ikitoweka.
Yale maji ambayo hupotea wakati ukipiga mswaki, wakati ukijipaka sabuni wakati wa kuoga na wakati wa kufanya usafi yanaweza kutumika kwa kazi nyingine kama utachagua kutumia mabomba banifu.
Endelea kusoma makala muhimu kutoka kwenye tovuti hii ya www.nukta.co.tz kwa dondoo muhimu zitakazokusaidia kuboresha maisha yako.