Furaha unayoweza kuipata ukiwa bachela

January 24, 2020 10:52 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Furahia muda na marafiki zako na weka familia yako karibu.
  • Pamoja na hayo, penda kubadirisha mazingira na tembelea sehemu zenye mambo unayoyapenda
  • Kwakuwa upo Single, haina maana ndiyo usijipende, upendo unaanzia kwako na kisha kwa wengine.

Dar es Salaam. Sio lazima kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi kwani sio mashindano yatakayokupatia zawadi kwa kuwa ndani yake wala hakuna hukumu hapo mbeleni kama hautakuwa kwenye mahusiano.

Kama wewe ni kijana na yule umpendaye hakupendi au haujampata, usijione dhaifu wala usiyefaa bali ukiwa unasubiri, ni vyema ukatumia muda wako kujijenga na kufurahia maisha.

Kama wewe ni bachela “single” na uko kwenye sintofahamu ya kufurahia maisha yako bila kujiingiza katika majuto kwa kuachwa au kukataliwa na mabinti au vijana wa kiume, basi dondoo hizi zitakufaa:

Jifunze kutoka nje ya mazingira yako

Huenda unafurahia muda wako nyumbani ukihisi akupendaye atashushwa kama mvua inyeshavyo.

Ni muda wa wewe kuanza kutoka mara moja moja ukutane na watu wapya kwani kwa kufanya hivyo, utakutana na watu wapya na kutengeneza mtandao nzuri kwa ajili yako.

Unaweza kutoka wewe mwenyewe kama una uwezo wa kufurahia muda wako binafsi au ukatoka na marafiki zako kwenda katika mazingira mapya yanayoweza kukutanisha na watu wapya.

Huenda unafurahia muda wako nyumbani ukihisi akupendaye atashushwa kama mvua inyeshavyo. Picha| howstuffworks.

Jipende

Siyo kwa sababu hauna mtu wa kukutumia meseji za asubuhi na “emoji” za makopakopa ndio ushindwe hata kujijali.

Kwenye kipindi hiki ambacho upo peke yako, ni busara kujipenda kwani hujui ni nani anavutiwa na wewe lakini tabia yako ya kukosa umaridadi inaweza kumpeperusha.

Vaa nguo nzuri na safi, kula vizuri, tengeneza nywele zako na uwe nadhifu. Ni muhimu kwako na kwa wakuzungukao.

Unaweza kumtambulisha rafiki yako ambaye hajipendi kwa marafiki zako maridadi? Ndivyo hali unayowapatia marafiki zako kila mara endapo haujithamini.


Zinazohusiana.


Hudhuria maeneo yenye vitu unavyovipenda

Kama unapenda mpira na ni shabiki wa timu ya Yanga au Simba, siyo mbaya ukaenda uwanjani ukiwa umevalia jezi yako (kama unajiamini utashinda) Natania tu! 

Ni rahisi kuanzisha mazungumzo na mtu ambaye mna jambo muhimu linalowaunganisha, lakini huko unaweza kutengeneza marafiki ambao kamwe hamuwezi kukosa suala la kuzungumza.

Huenda huangalii mpira wala huchezi aina yeyote ya mpira lakini siku hizi kuna michezo ya usiku “game nights” ambazo zinahusisha michezo kama “Monopoly” na hata kujifunza jinsi ya kucheza staili mbalimbali zikiwemo “Salsa” huko pia utafurahia muda wako na kukutana na watu wengi.

Huenda huangalii mpira wala huchezi aina yeyote ya mpira lakini siku hizi kuna michezo ya usiku “game nights”. Picha| Meetup.

Kaa karibu na marafiki 

Kwa muda huo, mbali na mahusiano ya kifamilia, una mahusiano na marafiki zako na ndugu. Ni vyema kuwaweka karibu na kufurahia kila punje ya sekunde unaokuwa nao. 

Kwa kufanya hivyo itakuondolea mawazo yakiwemo ya kujiona haufai au kuna kitu hakipo sawa kuhusu wewe.

Bado unatafuta furaha? Huwezi kukosa hata kimoja kati ya hivyo kurejesha furaha yako wakati wa ubachela wako. Kama hali yako ni ngumu, tafadhali wasiliana na wataalamu wa saikolojia kwa msaada zaidi. 

Usicheze mbali ijumaa ijayo kwani tutazungumzia jinsi ya kufurahia hali yako ya kiuchumi. 

Rodgers George ni mwanahabari wa tovuti ya Nukta anayepatikana kwa mawasiliano haya: Twitter:@FlairRodgers.

Enable Notifications OK No thanks