Hii ndiyo biashara inayomtesa zaidi bilionea Mo Dewji
- Ni kilimo cha chai ambacho amekuwa akitumia muda mwingi bila mafanikio.
- Ana mpango wa kujielekeza katika mazao mengine ikiwemo maparachichi.
Dar es Salaam. Bilionea wa Tanzania, Mohammed Dewji amesema moja ya biashara zake zinazomtesa zaidi na kuwekeza fedha nyingi ni ya kilimo cha chai, jambo linalomfanya aanze kufikiria kuwekeza katika mazao mengine ikiwemo maparachichi.
Bilionea huyo kupitia kampuni yake ya Mohammed Entreprises Limited (MeTL) anamiliki mashamba matatu yaliyolimwa chai yenye ukubwa wa hekta 2,350 huku hekta 1,200 ameingia mkataba na wakulima wadogo kulima zao hilo.
Mashamba hayo yenye viwanda vya kuchakata chai yanapatikana katika Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga na Rungwe katika mkoa wa Mbeya ambako kuna hali ya hewa inayoruhusu kustawi kwa zao hilo la biashara.
Mo Dewji ameleza hisia zake jana (Januari 31, 2020) katika ukurasa wake wa Twitter wakati akijibu maswali ya wafuasi wake yakiongozwa na hashatag ya #AskMoDewji.
Amesema amekuwa akitumia muda mwingi kuinua biashara yake ya chai na kupoteza fedha nyingi lakini bado hajafanikiwa kufikia malengo aliyokusudia.
“Ninajitahidi kutumia muda mwingi katika biashara ya chai. Nimekuwa nikipoteza pesa kwa miaka, tangu kuanzishwa kwake, niwe mkweli. Sasa naangazia kutumia baadhi ya hii ardhi yenye rutuba kwa mazao mengine yenye faida kama maparachichi, ambayo nimeanza kuifanya hivi karibuni,” amesema Mo Dewji katika ukurasa huo.
Bilionea huyo ambaye ametajwa kuwa miongoni mwa mabilioni 20 wa Afrika katika ripoti ya jarida la Forbes la mwaka 2020, alikuwa akijibu swali mfuasi wake, Bill Nenga @JuliusMollel13 aliyetaka kujua ni sehemu gani ya biashara ambayo hamuingizii faida.
I’m struggling big time in the TEA business. I’ve been loosing money for years, since inception to be honest. I’m now looking at using some of this fertile land for other lucrative crops like avocado, which I’ve started venturing into recently etc. #AskMoDewjihttps://t.co/IY56GwDEx0
— Mohammed Dewji MO (@moodewji) January 31, 2020
Kwa mujibu wa MeTL, mashamba hayo yanazalisha takriban tani 5,000 za chai kwa mwaka ambapo tano 4,000 ni chai nyeusi (black tea) ambayo imekuwa inasaidia kupambana na saratani, ugonjwa wa moyo, shinikizo la damu, na kupambana na uzee.
Kampuni hiyo ambayo huzalisha asilimia 15 ya chai yote ya Tanzania, asilimia 95 ya chai yake husafirishwa moja kwa moja nje ya nchi au katika mnada wa chai uliopo Mombasa nchini Kenya na inayobaki huuzwa kwa wasindikaji wa ndani.
Hata hivyo, Serikali iko katika mchakato wa kuanzisha soko la chai nchini ambapo minada yote ya chai inayozalishwa itakuwa inafanyika jijini Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa nje ya nchi ili kuwanufaisha wakulima na kuiongezea Serikali mapato.
Soma zaidi:
Mo Dewji ambaye kampuni yake inayofanya kazi katika nchi 11 za Afrika ikiwemo Kenya na kuajiri watu zaidi ya 24,000, pia anajishughulisha na kilimo cha mkonge, pamba, michikichi na karanga.
Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018, kinaeleza kuwa chai ni miongoni mwa mazao ya biashara yanayoingizia Tanzania fedha nyingi za kigeni ambapo mwaka juzi iliingiza dola za Marekani milioni 45.9 sawa na Sh105.8 bilioni
Hata hivyo, uzalishaji wake ulipungua kutoka tani 27,500 mwaka 2017 hadi tani 26,900 mwaka juzi.