Majaliwa apiga marufuku ujenzi wa viwanda maeneo ya shule

March 4, 2020 5:13 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  akiweka jiwe la msingi la jengo la Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Machi 3, 2020. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Asema shughuli za viwanda zinawaondolea utulivu wanafunzi wakiwa darasani.
  • Amtaka mfanyabiashara aliyejenga karakana katika eneo la shule ya msingi Mshikamano iliyoko Halmashauri ya Mji Handeni aondoke.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepiga marufuku shughuli zisizohusiana na taaluma ikiwemo ujenzi wa viwanda katika maeneo ya shule ili kutoa fursa kwa wanafunzi kuwa katika mazingira tulivu ya kujifunzia.

“Sheria inakataza kuweka matumizi yoyote yasiyokuwa ya kitaaluma katika maeneo ya shule kwani yanasababisha kelele hivyo wanafunzi kushindwa kusoma vizuri,” amesema Majaliwa jana Machi 3, 2020 akiwa katika ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Handeni mkoani Tanga.

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo baada ya kupokea malalamiko ya wazazi kuhusu eneo la shule ya msingi Mshikamano iliyoko Halmashauri ya Mji Handeni kuuzwa kwa mfanyabiashara ambaye amefungua karakana ya kutengeneza magari.

Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa halmashauri hiyo ukazungumze na mfanyabiashara huyo  ili  aondoe karakana katika eneo hilo na kumtafutia eneo mbadala kwa ajili ya kuendesha shughuli zake na eneo hilo libaki kwa ajili ya masuala ya kitaaluma.


Zinazohusiana: 


Pia, ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Handeni upange matumizi bora ya ardhi kwa kuainisha maeneo ya makazi, biashara, viwanda na huduma za kijamii ili kuepuka mji huo kujengwa bila ya mpangilio.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwataka wananchi kuwafikisha kwenye vyombo vya dola walimu watakaobainika kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi. 

“Serikali imeweka sheria kali ya kumlinda mtoto wa kike, ukimpa mimba, ukimchumbia au kumuoa adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela,” amesisitiza Majaliwa.

Enable Notifications OK No thanks