Watanzania tunakwama wapi ubunifu kwenye vyombo vya habari?

March 9, 2020 8:28 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Majibu ya swali hilo utayapa Machi 11, 2020 katika mdaharo uliondaliwa Mfuko wa vyombo vya habari Tanzania (TMF) jijini Dar es Salaam.
  • Wadau watajadili suluhisho za kidigitali zitakazosaidia kuboresha utendaji na ufanisi wa tasnia ya habari Tanzania katika kutoa habari sahihi na kukuza mapato.
  • Mdahalo huo ni sehemu ya Wiki ya Ubunifu (#IW2020). 

Dar es Salaam. Kama wewe ni miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakijiuliza bila kupata majibu kuhusu kukosekana kwa ubunifu kwenye vyombo vya habari Tanzania basi majibu utayapata muda si mrefu.

Mfuko wa vyombo vya habari Tanzania (TMF)  kwa kushirikiana na  kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa na Hamasa Magazine wameandaa mdahalo utakaowaleta pamoja wadau wa vyombo vya habari na teknolojia kujadili kuhusu kubuni suluhisho za kidigitali zitakazosaidia kuboresha utendaji na ufanisi wa tasnia ya habari Tanzania ili mchango wake katika shughuli za maendeleo.

Mdahalo huo utakaofanyika Machi 11, 2020 jijini Dar es Salaam ni sehemu ya Wiki ya Ubunifu (#IW2020) ambayo imeandaliwa na Mfuko wa Ubunifu wa Maendeleo ya Watu (HDIF) kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo ikiwemo Tume Ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Seedspace Dar es Salaam na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Uingereza (DFID).

Mdahalo huo ulioandaliwa na TMF na kubeba dhima ya “Kutoka wazo hadi suluhisho: Kubuni suluhisho za kidijitali kwa ajili ya vyombo vya habari Tanzania utakuwa wazungumzaji wakuu wanne akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa, Nuzulack Dausen.

Wazungumzaji wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa TMF, Fausta Msokwa, Baraka Kilanga kutoka Hamasa Magazine na Dastan Kamanzi kutoka TMF. 


Soma zaidi:


Miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa kwa kina katika mdahalo huo unaokusudia kuipeleka tasnia ya habari Tanzania katika hatua ya juu zaidi ni pamoja na changamoto za vyombo vya habari zinavyoweza kutumika kama fursa ya kubuni njia za kidijitali na ukuaji wake.

Wadau watajidili pia mifumo ya kibiashara na teknolojia za kidijitali za ndani na kimataifa zinazoweza kutumiwa na vyombo vya habari kukua na kuchangia katika maendeleo ya jamii na Taifa. 

Mdahalo huo unakuja kipindi ambacho tunashuhudia sekta mbalimbali ikiwemo ya fedha, elimu na kilimo zikiwa mstari wa mbele kutumia mifumo ya dijitali kuboresha maisha huku vyombo vya habari vikibaki nyuma.

Huenda wadau watakaoshiriki tukio hilo muhimu, wataibuka na suluhisho la kidijitali la  kudumu litakalosaidia vyombo vya habari kufaidika na maendeleo ya sayansi na teknolojia. 

Kwa wanaotaka kushiriki mdahalo huo umuhimu utakaofanyika katika ukumbi wa mikutano wa LAPF Millenium Tower, Kijitonyama wanashauriwa kujisajili hapa http://lnnk.in/qBL

Wiki Ya Ubunifu huandaliwa kila mwaka ambapo huwakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo kujadili hatua zilizopigwa katika kuendeleza ubunifu nchini na maeneo yanahitaji msukumo wa kipekee wa matumizi ya teknolojia.

Pia ni jukwaa muhimu kwa wabunifu kuonyesha kazi zao hasa suluhisho za teknolojia zinazogusa sekta mbalimbali ili kuboresha maisha ya watu na kuifanya Tanzania kuwa sehemu nzuri ya kuishi.

Enable Notifications OK No thanks