Majaliwa apokea msaada wa Sh1.2 bilioni kupambana na Corona
- Ni fedha na vifaa mbalimbali vikiwemo vitakasa mikono, gesi na majenereta.
- Vitasaidia katika mikakati ya kupambana na virusi vya Corona.
- Waliotoa misaada hiyo ni pamoja na benki na wafanyabiashara.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepokea msaada wa fedha pamoja na vitu mbali mbali kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) wenye thamani ya sh. Sh1.2 bilioni kutoka kwa wadau zikiwemo taasisi za fedha na wafanyabiashara.
Majawaliwa mmepokea msaada huo leo (Machi 28, 2020) katika ofisi ndogo ya Waziri Mkuu iliyoko Magogoni, jijini Dar Es Salaam na amewashukuru wadau hao na kuwataka Watanzania waendelee kushirikiana na Serikali katika hatua zinazochukuliwa kukabiliana na ugonjwa huo.
Miongoni mwa wadau waliotoa msaada huo ni taasisi za kifedha ikiwemo benki ya UBA Tanzania iliyotoa Sh230 milioni, CRDB (Sh150 milioni) na NMB imetoa Sh100 milioni.
Wadau wengine ni kampuni ya Karimjee Jivanjee Ltd na kampuni zake tanzu wametoa Sh200 milioni pamoja na kuhaidi kufanyia matengenezo kinga ya magari yote ya Toyota yanayotumika katika kukabiliana na COVID-19 kwa muda ya siku saba bure,
“Familia ya Karimjee imetoa jenereta la kilowati 180 lenye thamani ya Sh75 milioni,” imeeleza taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyotolewa leo.
Wengine ni Watoa Huduma ya Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS) ambao wametoa bidhaa mbalimbali zikiwemo magari ya matangazo yatakayotumika kutoa elimu kwa muda wa miezi minne kupitia kampuni ya Advent Construction, maji ya kunywa (Bakhressa Group), Billboard (Ashton Media) vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh150 milioni.
Zinazohusiana
Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) wametoa matanki 1,000 yenye thamani ya Sh25 milioni huku kila moja likiwa na ujazo wa lita 250, matanki hayo yametengenezwa maalumu kwa ajili ya kunawia mikono.
Pia kampuni ya GS1 Tanzania Limited imetoa vitakasa mikono chupa 1,600 zenye thamani ya Sh8 milioni.
Kampuni ya Tanzania Oxygen Ltd nayo imetoa msaada wa Sh158 milioni ambapo wamehaidi kufanyia ukarabati kiwanda kikubwa cha kuzalisha oksijeni. Mount Meru imetoa vitakasa mikono vyenye thamani ya Sh2 milioni huku Hospitali ya Aga Khan ikitoa dawa, sabuni, vitakasa mikono na vifaa tiba vyenye thamani ya Sh10.3 milioni.
Pia, kampuni ya gesi ya Oryx imehaidi kutoa msaada wa kusambaza gesi kwa ajili ya kupikia na matumizi mengine katika hospitali kama kufulia na kwenye vituo vya kuwahifadhi watu wanaohisiwa kuwa pamoja wagonjwa wa COVID-19.
“Gesi hiyo ina thamani ya Sh25 milioni, Tredea Cosmetics Ltd wametoa vitakasa mikono vyenye thamani ya Sh1.6 milioni,” imeeleza sehemu ya taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokea hundi ya Sh230 milioni ukiwa ni mchango wa Benki ya UBA wakati alipopokea michango kutoka kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona, Machi 28, 2020. Kulia ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kushoto ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Usman Isaka na wa nne kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo, Farhiya Warsama. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.
Umoja wa Mama lishe-Ilala na Machinga wa Kariakoo wametoa sabuni na vitakasa mikono vyenye thamani ya Sh2 milioni. Wakati huohuo, Chemba ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA) wametoa shuka 50, magodoro10, sabuni za maji chupa 170 na vitakasa mikono chupa 400 vyote vikiwa na thamani ya Sh5 milioni.
Baada ya kupokea misaada hiyo, Waziri Mkuu kwa niaba ya Rais John Magufuli amewashukuru wadau hao kwa vitu mbalimbali walivyovitoa kwa ajili ya kupambana na COVID-19 kwani vifaa pamoja na fedha walizozitoa zitaisadia Serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali kwa upande wake inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kupambana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha hausambai zaidi nchini.
Kuhusu wadau wengine wanaohitaji kutoa misaada, Waziri Mkuu amesema Ofisi yake iko wazi pia wanaweza kupeleka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kwa walio nje ya nchi au sehemu yoyote wanaweza kutuma fedha kupitia akaunti yenye Jina la: National Relief Fund Electronic Akaunti Na: 9921159801