WHO: Janga la corona bado halijafika ukingoni

April 27, 2020 4:19 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Ghebreyesus amesema wanaguswa na kuongezeka kwa visa katika baadhi ya mabara ulimwenguni.
  • WHO kuanza kutoa tafsiri kwa wanahabari wa Kiswahili katika mikutano kuhusu COVID-19.

Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema janga la ugonjwa wa virusi vya corona “bado lipo sana tu” kutokana na kuongezeka kwa visa vya wagonjwa wapya katika baadhi ya mabara ulimwenguni.

“Janga hili bado halijafikia ukingoni,” Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Ghebreyesus amesema leo (Aprili 27, 2020 katika mkutano wake na wanahabari na kurudia tena “janga hili bado halijifikia ukingoni”.

Dk Tedros amesema kuwa janga hilo halijafikia ukingoni kutokana na mwenendo wa kuongezeka kwa visa katika mabara ya Afrika, Ulaya Mashariki, Amerika Kusini, na baadhi ya nchi za bara la Asia.

“Katika mabara yote hayo idadi ya visa na vifo haviripotiwi kikamilifu katika nchi hizo za maeneo hayo kutokana na uwezo mdogo wa kupima,” amesema bosi huyo wa WHO katika mkutano huo na wanahabari.

Amesema WHO inaendelea kuzisadia nchi mbalimbali ulimwenguni hususan zinazoendelea katika kupambana na ugonjwa huo kwa kutoa ushauri na vifaa tiba ikiwemo vya kuwakinga wahudumu wa afya.


Soma zaidi: 


Dk Tedros amesema kuwa WHO inatoa ushauri mzuri wa kisayansi katika kukabiliana na ugonjwa na jukumu la nchi husika kukataa au kukubali ushauri huo.

“Kutokana na uzoefu wetu unaonyesha baadhi ya nchi zimekubali nyingine huenda zikakataa lakini mwisho wa siku kila nchi inabeba mzigo wake na narudia sisi hatuna nguvu za kuamrisha nchi kufuata ushauri bali utayari wa nchi kukubali au kukataa…hii ni kwa kila nchi ila tutaendelea kutoa ushauri kwa misingi ya ushahidi wa kisayansi,” amesema Tedros.

WHO pia limesema lipo mbioni kuanza kutoa huduma za kutafsiri mikutano yake na wanahabari kwa Kiswahili katika siku za hivi karibuni ikiwa ni moja ya jitihada za kuhakikisha habari kuhusu mapambano ya ugonjwa wa virusi vya corona zinawafikia wengi zaidi.

Dk Tedros amesema leo wameongeza huduma za kutafsiri kwa wanahabari wanaozungumza lugha ya Kireno.

“Baada ya hii tutaanza kutoa huduma hii kwa Kiswahili na Kihindi,” amesema Dr Tedros.

Kiongozi huyo wa juu wa shirika hilo amesema wataendelea kutoa taarifa katika lugha nyingi iwezekanavyo kuhakikisha taarifa zinawafikia watu wengi zaidi ulimwenguni.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Ghebreyesus. WHO imesema janga la corona bado halijafika ukingoni. Picha|UN.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW