Unayotakiwa kuangalia kabla ya kununua pafyumu
- Zingatia unene wa mfuko wako na jinsia yako.
- Wakati wa kutumia angalia mazingira uliyopo.
- Wataalam wa afya wameshauri kuwa matumizi ya pafyumu yazingatie hali ya kiafya.
Dar es Salaam.Hakuna asiyependa kunukia lakini swali ni harufu yako inampendeza kila mtu? Shiriki katika safari hii ambayo huenda ikabadili mtazamo wako pale unapotembelea duka la kununua pafyumu ya kujipulizia mwilini.
Pafyumu ni kati ya bidhaa binafsi ambazo watu hutumia kwaajili ya kujiongezea harufu tofauti na ya mwili na hivyo kuwa na harufu iliyotengenzwa ma malighafi mbalimbali.
Harufu hiyo huwasaidia watu kunukia vizuri mbele ya watu na wakati mwingine kukata halafu ya asili hasa maeneo yenye joto na mikusanyiko ya watu.
Hata hivyo, siyo kila mtu anapenda pafyumu na wengine hutumia bidhaa za asili kama limao, tango au sabuni kukata harufu mbaya ya mwili.
Kama unapenda pafyumu, bado hauna haja ya kuhofia. Muhimu ni kufahamu mambo machache unayotakiwa kuzingatia wakati wa kununua na kutumia pafyumu yako ili usiwakere watu wanaokuzunguka.
Je, unahitaji kuzingatia nini unapoenda kununua bidhaa hiyo ?
- Jinsia yako
Fahamu kuwa siyo kila pafyumu imetengenezwa kwaajili ya kila jinsia. Zipo pafyumu maalumu kwa ajili ya wanawake na zingine ni kwa wanaume tu.
Hata hivyo, zipo pafyumu ambazo hazibagui jinsia yaani, kila mtu anaweza kutumia. Wakati umefika dukani kununua bidhaa hiyo hakikisha unasoma maelezo ya jinsia ili kama wewe ni mwanaume usije ukaingia choo cha kike.
Ujazo wa manukato unaweza tofautiana na matarajio yako ya gharama lakini nimuhimu kuzingatia ubora wa manukato hayo kuliko ujazo wake. Picha| Giphy.
- Matumizi yake
Siyo kila pafyumu imetengenezwa kwa ajili ya matumizi ya shughuli za kila siku. Zingine hutumika maalum kwa ajili ya maiti misibani.
Ni vizuri kuwa na uelewa juu ya “Brand” ya pafymu unayanunua ili usije ukajikuta kila unayepishana naye anakutazama kwa jicho la mshangao
- Bajeti yako
Muuzaji wa manukato kwenye duka la Ariyha Scents liliopo Makumbusho jijini Dar es Salaam, Hawa Ismail amesema kila chupa ya manukato ina bei yake.
Uzuri ni kwamba, zipo hadi chupa zinazouzwa kwa gharama chini ya Sh5,000 kwenye maduka ya bidhaa hiyo.
Hawa amesema ni muhimu kujua kuwa pafyumu za wabunifu mashuhuri ulimwenguni huuzwa kwa bei za juu kuliko pafyumu za kawaida.
“Utakuta perfume inauzwa hadi laki tatu. Usishangae kwani thamani yake itaendana na ubora wake. Zinakaa kwenye nguo tofauti na manukato mengine,” amesema Hawa.
Zinazohusiana
- Bajeti inavyookoa matumizi mabaya ya fedha ngazi ya familia
- Zingatia haya wakati ukifanya manunuzi msimu wa sikukuu
- Mambo ya kufanya wakati wa mapumziko ya mwisho wa mwaka
- Uthabiti wa pafyumu yako
Loyce Msolwa ni muuzaji wa manukato ya kila aina. Yeye amesema kununua payumu “original” au thabiti ni moja ya vitu vya kuzingatia.
Mdau huyo wa harufu za kutengenezwa amesema “ukinunua pafymu hauna haja ya kuioga. Unaweza kupulizia mara tatu tu na harufu yake ikatosha kabisa.”
“Kila pafymu ina muda wake wa kunukia lakini harufu yake inaweza isikufikie kwa kuwa umeipulizia mbali. Mara zote hakikisha unapulizia mbele ya shingo yako, kwenye sehemu ya ndani ya kiwiko chako, na pia nyuma ya shingo,” amesema Msolwa.
- Watu unaokaribiana nao
Kwa upande wake Daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba Joshua Sultan amesema kutumia manukato makali kunaweza kuwa hatarishi kwa watu ambao wana shida katika mfumo wao wa kupumua.
Daktari huyo ambaye ametolea mfano wa wagonjwa wa pumu amesema ni hatari kwao kwani harufu kali ambazo haziwiani nao zinaweza kuwasababishia matatizo makubwa yakiwemo kifo na matatizo ya ubongo endapo hawatopata matibabu baada ya kupata mzio unaoweza kutokana na harufu iliyowafikia.
“Baadhi ya manukato yana harufu kali na endapo mtu mwenye changamoto kwenye mfumo wake wa kupumua atakutana nayo, yanaweza kumsababishia shambulio la mfumo wa upumuaji,” amesema Dk Sultan.
Zaidi, mtaalamu huyo amesema ili kuepukana na shida kama hizo mtu ambaye anafahamu yupo na changamoto hizo anatakiwa kutembea na dawa zitakazomsaidia akikutana na harufu kali ya pafyumu.
Pia anashauliwa kutumia barakoa endapo atakua katika mazingira ambayo hawezi kuyaepuka.
“Kama mtu unashida hiyo, ukiwa na mtu mwenye manukato makali, vaa barakoa au hakikisha unatembea na dawa zako kila uendapo,” ameshauri Dk Sultan.