TTB yatangaza mikakati kuinua sekta ya utalii Tanzania
- Ni mikakati kumi iliyowekwa na bodi hiyo kupambana na makali ya ugonjwa wa corona kwenye sekta ya utalii.
- Mikakati hiyo ni pamoja na kushirikiana na wadau wa utalii kuja na mpango mkakati wa umoja pamoja na kuandaa vipindi maalumu kuhamasisha utalii wa ndani.
Dar es Salaam. Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imetangaza mikakati 10 ya muda mrefu inayolenga kuinua soko la utalii nchini Tanzania ambalo kwa sasa limeathirika na ugonjwa wa Corona ikiwemo kuimarisha timu ya mauzo na mbinu za kisasa za utangazaji vivutio vya utalii.
Mwenyekiti wa Bodi ya hiyo Jaji Mstaafu Thomas Mihayo amesema ugonjwa wa COVID-19 umeathiri kwa sehemu kubwa sekta ya utalii duniani na inahitajika mikakati mipya kuinua tena shughuli za utalii nchini.
Jaji Mihayo aliyekuwa akizungumza leo amesema wanashirikiana na wadau wa utalii kuandaa mkakati wa pamoja wa kukabiliana na janga la COVID-19 kwenye sekta ya utalii pamoja na kuandaa mkakati mpya wa mauzo wa kimataifa kupitia ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID).
Sambamba na mkakati huo bodi hiyo imepanga kushirikisha watu mashuhuri na mabalozi wa utalii Tanzania kwa ajili ya kutangaza utalii hasa kwa njia ya mtandao.
Mkakati mwingine ni kuimarisha timu ya mauzo, kubuni mbinu za kisasa na kitaalamu zenye ubunifu wa kuandaa mikakati ya mauzo ya mtandao, kutangaza utalii wa ndani kupitia programu maalum za mashule na vyuo vya elimu.
Pia TTB itashirikiana na Balozi za Tanzania nje ya nchi kuweka mikakati bayana ya kuwapata mabalozi wa utalii watakaoitangaza nchi na vivutio vyake.
Kwa sasa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Uhifadhi Ngorongoro (NCAA) wameingia ubia na kampuni ya Great Migration Camp ambayo kwa pamoja wamebuni kipindi maalum cha ‘’Serengeti Live Show’’.
“Kipindi hicho kinarushwa mubashara na vingine kurekodiwa kwa awamu kwenye mitandao ya TTB na washirika wake nchini na nje ya nchi kuonesha utalii wa Tanzania,” amesema Jaji Mihayo.
Madhumuni ya vipindi hivyo ni kukonga mioyo ya watalii ambao wameahirisha safari zao za kuja Tanzania kwa hofu ya Corona na kupitia vipindi hivyo bodi hiyo itaendelea kutangaza nchi kupitia kampeni ya “Tanzania Unforgettable” ili kuhamasisha sekta ya utalii.
Zinazohusiana
- Shabiki wa Taifa Stars ateuliwa balozi wa utalii Uingereza
- Tanzania yaangazia masoko 18 duniani kukuza utalii
Mwenyekiti huyo amesema mara baada ya kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa Corona, bodi hiyo ilianza kuchukua tahadhari zikiwemo kuandaa na kurusha makala fupi ya dakika 1.5 iliyosambaa duniani kuhamasisha watalii kujikinga na Corona na kuwakumbusha wasifute safari zao za utalii nchini Tanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TTB, Devotha Mdachi amesema mwezi Mei mwaka huu Ofisi yake inatarajia kufanya kikao na wadau wa sekta ya utalii nchini ili kujadili mikakati ya pamoja inayolenga kuimarisha soko la utalii nchini.
Kwa mujibu wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) utalii wa kimataifa utashuka kati ya asilimia 20 na 30 na hali hiyo itaziweka mashakani ajira milioni 50 za watu walioajiriwa katika sekta hiyo.