Rais Magufuli, Watanzania waomboleza kifo cha Dk Mahiga

May 1, 2020 6:55 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Waziri huyo wa Katiba na sheria amefariki alfajiri ya leo akiwa nyumbani kwake Dodoma.
  • Magufuli amesema atamkumbuka kwa uchapakazi wake Serikalini.
  • Viongozi na Watanzania waguswa na msiba wa kiongozi huyo wa muda mrefu.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania John Magufuli ameungana na viongozi wa Serikali na Watanzania kuomboleza kifo cha Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Augustine Mahiga kilichotokea alfajiri ya leo nyumbani kwake jijini Dodoma baada ya kuugua ghafla.

Rais Magufuli katika taarifa yake iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, amesema marehemu baada ya kuugua alifikishwa hospitali leo (Mei 1, 2020) akiwa tayari amefariki dunia. 

Aidha, ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu, Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai, Wabunge na wafanyakazi wa Wizara ya Katiba na sheria.

Pia amewatumia salamu za pole wananchi wa Mkoa wa Iringa kwa kuondokewa na mpendwa wao na anaungana nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi. 

“Pamoja na umri wake mkubwa na uzoefu wa kushika madaraka katika nyadhifa mbalimbali za kitaifa na kimataifa, marehemu Balozi Mahiga alikuwa mnyenyekevu na mtiifu kwa kila jukumu nililomtuma,” amesema Rais Magufuli.

Katika taarifa hiyo, Dk Magufuli amemwelezea marehemu Balozi Mahiga kama mchapakazi, mzalendo na mwanadiplomasia mahiri aliyeiwakilisha na kuipigania Tanzania katika nyanja za kimataifa kwa miaka mingi.


Zinazohusiana


Pia kiongozi huyo amekuwa akimwakilisha Rais Magufuli katika mikutano mbalimbali ya kikanda na ya kimataifa sanjari na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Balozi Mahiga amefariki akiwa na miaka 74 huku akiacha alama yake kwa watanzania kutokana na uchapakazi wake ukiwemo wa kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa kuanzia mwaka 2003-2010.

Pia alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania kuanzia mwaka 2015-2019 kabla ya kuhamishiwa katika Wizara ya Katiba na Sheria hadi mauti yalipomfika leo. 

Wanasiasa, Watanzania wamlilia

Baada ya Rais kutangaza kifo cha mwanadiplomasia huyo, wanasiasa na Watanzania wametoa salamu zao za pole kwa ndugu na familia huku baadhi yao wakimuelezea marehemu kwa tabia yake ya usikivu na unyenyekevu.

Mbunge wa Tarime vijijini, John Heche amesema nchi imepoteza mtu makini ambaye atakumbukwa daima kwa uwezo wake wa kumsikiliza kila mtu.

“Leo Taifa limepoteza mtu mwema, mbobezi wa diplomasia, rafiki yangu na baba yangu mzee Mahiga, nakulilia sana, tulikua wote bungeni, tofauti na wabunge na mawaziri wengi wa CCM, ulitambua hotuba yetu ukasifu uwezo na ushauri wa waziri kivuli Salome Makamba. Nitakukumbuka daima,” amesema Heche katika ukurasa wake wa Twitter. 

Naye Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema amepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Balozi Mahiga na anatoa pole kwa wafiwa wote.  

Naye aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema katika ukurasa wake wa Twitter kuwa  “Mzee Mahiga nimefahamiana naye kabla ya kuingia kwenye siasa wakati nasoma Marekani yeye alikuwa Balozi Umoja wa Mataifa. Namfahamu kama gwiji wa Diplomasia. Nimepoteza mtu muhimu sio tu Mwanasiasa bali mzee wangu wa karibu sana.” 

Enable Notifications OK No thanks