Ukaaji mbaya unavyochangia maumivu ya mgongo

May 2, 2020 6:35 am · Joshua
Share
Tweet
Copy Link
  • Mkao wako huathiri namna mfumo mzima wa nyonga utakavyokua.
  • Hii huwakumba sana madereva wa muda mrefu pamoja na wafanyakazi ambao hukaa muda mrefu.
  • Asilimia kubwa ya matatizo ya mgongo hutokana na kutozingatiwa kwa kanuni za kibaiomekaniki.

Ninapoanza kutumia kalamu yangu ya uandishi ningependa kukusihi ya kuwa afya yako ni ya muhimu sana kuliko kitu chochote. Hakuna mbadala wa afya. 

Hivyo basi hauna budi kuzingatia kanuni za afya katika kipindi hiki cha ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona. Jukumu la afya ni la kwako binafsi. 

Niwatie moyo wale wote ambao wanapitia kipindi kigumu cha ama kuumwa au kuuguliwa na wapendwa wao. Pia wale wote waliofiwa kwa ugonjwa huu Mwenyezi Mungu muweza wa yote na awapatie ninyi nguvu na faraja. InnaLilahi!

Wiki iliyopita tuliangazia mfumo mzima wa namna mgongo na tishu shirika zilivyo umbika na zinavyoweza kusababisha maumivu ya mgongo kwa namna moja ama nyingine. Tuangazie sasa ni namna gani maumivu yanaweza kuja kwa muktadha wa namna tulivyoongelea awali.

Mkao wako huathiri namna mfumo mzima wa nyonga utakavyokua. Chukulia mfano umekaa katika sehemu ambayo haina uwiano. Upande mmoja utakuwa tofauti na ule mwingine. Ikitokea kuna mabadiliko tabia ya mwili ni kufidia. 

Ukaaji wako usio sahihi unaweza kuwa sababu ya maumivu ya mgongo. Picha|Mtandao.

Hivyo mfumo huu wa kufidia tatizo lililo kwenye nyonga utaendelea hadi kubadili umbo la mkao wa mgongo kwa wakati huo. Hii huathiri uwiano wa misuli ikiilazimu mingine kukaza zaidi na mingine kulegea. 

Pia hulazimisha baadhi kuwa mifupi na mingine mirefu kwa kuvutika zaidi. Tafakari iwapo mfumo huu wa ukaaji ukawa sugu maana yake maumivu na mabadiliko haya yatakua sugu. Hii huwakumba sana madereva wa muda mrefu pamoja na wafanyakazi ambao hukaa muda mrefu. 

Ni vizuri kuhakikisha sehemu uliokalia imenyooka na kama ina sifongo basi haina mbonyeo wa kupita kiasi. 

Unyanyuaji mbaya wa vitu hupelekea mkazo kwenye misuli. Hii hutokana na kujaribu kutengeneza nguvu zaidi kuhimili uzito. Pia ni matokeo ya kutumia misuli ya mgongo zaidi katika ubebaji badala ya misuli ya paja na mikono. 

Mkazo ukizidi misuli ya mgongo iliojishikiza katika pingili huweza ama kuvutika kupita kiasi na kutegua pingili au kupata michubuko midogo midogo yenye kuleta maumivu.

Ukaaji mbaya unaoathiri mikunjo ya asili ya mgongo. Tuliangazia kuwa mgongo una umbo lake lenye mikunjo ya asili ambayo kazi yake kubwa ni kuhakikisha mgawanyo wa kani na mgandamizo uko sawa. 

Iwapo mikunjo hii itaathiriwa basi mgawanyo wa migandamizo hii huathiriwa nakupelekea mkazo katika eneo husika. Mabadiliko haya ni ama kunyooka zaidi au kujikunja kupita kiasi. 

Pia kani hizi za kibaiomekani huweza pelekea mzio zaidi kwenye diski za mgongo na hivyo kuathiri anatomia yake. Hii huweza kusababisha kugandamizwa kwa neva husika. 


Zinazohusiana:


Mwili wa binadamu umeundwa kuchakaa. Na kuchakaa huku ni kuzeeka. Hivyo viungo vya mwili huanza kupoteza ubora na uimara wake wa utendaji. 

Mabadiliko haya pia huzikumba diski za mgongo kwani hupoteza umbo lake la kawaida kwa kuanza kusinyaa taratibu. Mabadiliko haya husababisha mgawanyo wa kani kuwa mbaya na hivo maumivu huanzia hapa. 

Ukweli ni kuwa, asilimia kubwa ya matatizo ya mgongo hutokana na kutozingatiwa kwa kanuni za kibaiomekaniki. Na hii hutokana na shughuli zetu za kila siku. 

Kwa lugha nyingine ni kwamba hali hizi kwa asilimia kubwa zinaepukika. Ninashauri taasisi kuwa na tabia ya mafunzo ya namna mbalimbali za kuepukana na matatizo ya neva na mifumo ya misuli na mifupa. 

Kukunjwa kwa jamvi sio mwisho wa maongezi. Tukutane tena katika kijiwe hiki tukiangazia kanuni na dondoo muhimu za afya. Sitoacha kukusihi kuchukua tahadhari dhidi ya corona kwa kunawa mikono mara kwa mara, kuepuka mikusanyiko na kutumia barakoa iwapo utahitaji kutoka. Kuwa salama na mlinde na mwingine. Nipo!

Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mazoezi tiba na mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) na Mkurugenzi wa Indigo Afya. Hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.

Enable Notifications OK No thanks