Prof Kabudi: Hatutafunga mipaka ya Tanzania
- Amesema hatua hiyo itaruhusu kupita bidhaa muhimu kuelekea katika nchi zisizo na bandari.
- Amesema Corona ni hatari lakini shughuli zingine lazima ziendelee.
Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof Palamagamba Kabudi ameendelea kusisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuacha wazi mipaka yake licha ya tishio la janga la Corona ili kuruhusu bidhaa muhimu kufika katika nchi zisizo na bandari.
Tanzania inategemewa na nchi zaidi ya nane za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kupitisha bidhaa zao katika bandari ya Dar es Salaam.
Nchi hizo ni pamoja na Zambia, Congo DRC, Uganda, Rwanda na Burundi ambazo baadhi zimefunga mipaka yake kama tahadhari ya kusambaa kwa virusi vya COVID-19.
Kabudi ametoa msimamo huo wa Tanzania katika hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2020/2021 iliyowasilishwa leo (Mei 13, 2020) Bungeni jijini Dodoma.
“Katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona, Tanzania imeendelea kuacha mipaka yake wazi kwa kuruhusu bidhaa muhimu kuelekea katika nchi zisizo na bandari kupita,” amesema Kabudi.
Amesema Tanzania ni kiungo muhimu cha usafirishaji wa bidhaa kwa baadhi ya nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini ya Maendeleo ya Africa (SADC).
“Corona ni hatari, lakini kukosekana kwa mahitaji muhimu kwa nchi zisizo na bandari kama chakula, dawa na mafuta ya petroli ambavyo vinapitia katika bandari yetu kuelekea katika nchi zisizo na bandari kunaweza kuwa ni hatari zaidi,” amesisitiza Prof Kabudi.
Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof Palamagamba Kabudi akizungumza wakati alipokuwa akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Madini kwa mwaka 2018/2019. Picha|MAELEZO.
Amesema hatua hiyo ya kuacha mipaka wazi ni utekelezaji wa azimio la mkutano wa dharura wa pamoja wa baraza la mawaziri la kisekta la masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya uliofanyika kwa njia ya mtandao Machi 2020.
Katika kutekeleza azimio hilo, amesema mamlaka za vituo vya pamoja mipakani (OSBPs) zimeelekezwa kuhakikisha zinaepusha vikwazo visivyo vya lazima kwa kukaa pamoja na wenzao wa nchi jirani waliopo katika vituo hivyo kutatua changamoto za mipakani katika kipindi hiki cha ugonjwa wa Corona bila kuathiri upatikanaji wa bidhaa hizo muhimu katika nchi zisizo na bandari.
Hata wakati Tanzania ikisema haitafunga mipaka yake kulinda kusaidia nchi jirani, Zambia imefunga mpaka wake na Tanzania wa Nakonde kwa muda kuanzia Mei 11 hadi itakapotangazwa ili kukabiliana na ongezeko la visa vya COVID-19 nchini humo.
Soma zaidi:
- Bajeti ya Wizara ya Ulinzi yapaa kwa mara ya pili mfululizo.
- Bashungwa: Sijapewa fedha za maendeleo wizara ya viwanda, biashara 2019-2020
- Kamwelwe aomba matrilioni kugharamia ujenzi, uchukuzi Tanzania
Bajeti yaongezeka
Ili kuweza kutekeleza kikamilifu majukumu yake mwaka 2020/2021, wizara hiyo imepanga kutumia bajeti ya Sh199.7 bilioni na kati ya fedha hizo Sh20 bilioni ni kwa ajili ya maendeleo na kiasi kilichobaki kitatumika kwa matumizi ya kawaida.
Bajeti hiyo imeongezeka kutoka Sh166.9 bilioni ya mwaka 2019/2020 ambao unaisha Juni 30.
Hata hivyo, hadi kufikia Aprili 30, 2020 wizara hiyo ilikuwa imepokea kutoka hazina kiasi cha Sh133.3 bilioni sawa na asilimia 79.8 ya fedha zote za bajeti zilizoidhinishwa katika mwaka wa fedha 2019/2020.
Prof Kabudi amesema katika mwaka wa fedha 2020/2021 pamoja na masuala mengine, wizara imeweka kipaumbele katika kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nje, kuvutia watalii, kutafuta misaada na mikopo yenye masharti nafuu.
Aidha, waziri huyo amesema watakamilisha Sera ya Mambo ya Nje 2020, kuboresha kanzidata ya diaspora itakayotoa taarifa itakayosaidia kuandaa mwongozo wa namna ya kuwashirikisha Diaspora wa Tanzania kuchangia katika maendeleo ya nchi yao.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Mambo Nje, Ulinzi na Usalama Sebastian Kapufi ameishauri Serikali kutoa fedha ambazo zimebaki kwa wizara hiyo ifikapo Juni 30 ili itekeleze miradi yake iliyopangwa 2019/2020.
“Kamati inasisitiza Serikali katika mwaka 2020/21 kutoa kipaumbele katika miradi ambayo ina umuhimu wa kipekee kiuchumi. Kwa mfano ujenzi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Oman itatupatia fursa nyingi ikizingatiwa kuwa Oman ni miongoni mwa nchi zenye uchumi mzuri duniani,” amesema Kapufi.
Latest