Ripoti: Tanzania yaongeza watumiaji wa intaneti zaidi ya milioni moja ndani ya miezi mitatu
- Watumiaji wa huduma hizo wamefikia milioni 26.8 Machi 2020 kutoka milioni 25.7 waliorekodiwa Desemba 2019.
- Wachambuzi wasema hiyo ni ishara kuwa Watanzania wanachangamkia fursa za mtandaoni.
Dar es Salaam. Watumiaji wa intaneti Tanzania wameongezeka kwa asilimia 4.1 katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, jambo linalofungua milango kwa Watanzania kufaidika na fursa za mtandaoni ikiwemo kufanya biashara na kupata ujuzi.
Takwimu mpya za robo ya kwanza ya mwaka 2020 za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa watumiaji wa huduma hizo walifikia milioni 26.8 Machi 2020 kutoka milioni 25.7 waliorekodiwa Desemba 2019.
Hilo ni sawa na ongezeko la watumiaji zaidi ya milioni moja ndani ya kipindi cha miezi mitatu.
Hata hivyo, ripoti hiyo haijaweka wazi ni aina gani ya intaneti inayotumiwa zaidi na Watanzania kama ambavyo imekuwa ikifanyika miaka iliyopita, ambapo intaneti inayohamishika isiyo ya waya (mobile wireless) ilikuwa ikitumiwa na watu wengi zaidi. Intaneti inayohamishika hutumika zaidi na simu za mkononi, tableti na kompyuta mpakato.
Kwa takwimu za mwaka 2018, watumiaji intaneti inayohamishika walikuwa asilimia 96.2 wakifuatiwa na intaneti isiyo ya waya na isiyohamishika kwa asilimia tatu.
Hiyo ina maana kuwa kila watumiaji 10 wa intaneti basi tisa walikuwa wanatumia intaneti inayohamishika.
Ongezeko la watumiaji wa intaneti limekuwa likishudiwa kila mwaka jambo linaloashiria kuwa Watanzania wanavutia na huduma hiyo ambayo imekuwa ikisaidia kutafuta vitu mbalimbali mtandaoni.
Mathalan, hadi mwaka 2019 Tanzania ilikuwa na watumiaji milioni 25.8 ambapo waliongezeka kutoka milioni 23.1 waliorekodiwa mwaka 2018,
Zinazohusiana:
- Ni historia: Watumiaji wa intaneti Tanzania sasa wafikia milioni 23
- Mbinu tano za kudhibiti matumizi makubwa ya intaneti kwenye ‘smartphones’
Mtaalam wa programu za kompyuta kutoka kampuni ya Code forAfrica Clemence Kyara ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa kuongezeka kwa watumiaji wa intaneti kunamaanisha shughuli za watu mtandaoni zimeongezeka.
Amesema kwa sasa watu wanapendelea kufanya malipo, manunuzi wakiwa mtandaoni hivyo ni lazima matumizi ya huduma hiyo yaongezeke.
“Huenda kuna vitu vinawavutia mtandaoni, ni lazima watumie intaneti ili kukidhi matakwa yao,” amesema Kyara na kuongeza kuwa ujio wa intaneti zenye kasi ikiwemo 4G na 5G nacho ni kivutio kwa watu kutumia huduma hizo kwa shughuli mbalimbali.
