Wizara ya afya: Mambo ya kuzingatia kabla ya shule, vyuo kufunguliwa Juni mosi

May 28, 2020 11:09 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wizara ya afya imetoa mwongozo utakaosaidia shule na vyuo kuchukua tahadhari dhidi ya Corona.
  • Wanafunzi wasisitizwa kuvaa barakoa, kunawa mikono, kukaa umbali wa mita moja wawapo shuleni.
  • Vyuo, shule zatakiwa kutumia mifumo ya kidijitali kufundisha wanafunzi. 

Dar es Salaam. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa mwongozo wenye maeneo manne ambayo yanapaswa kuzingatiwa na shule na vyuo vitakapofunguliwa Juni mosi ili kuwawezesha kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya Corona. 

Waziri wa wizara hiyo Ummy Mwalimu katika mwongozo huo amesema maeneo hayo ni maandalizi ya mazingira ya taasisi za elimu kabla ya kufunguliwa, uchunguzi wa afya, usafiri wa kwenda na kurudi shuleni/chuoni na mazingira ya kujifunzia. 

Katika mazingira ya shule au vyuo, Ummy amesema yanatakiwa kutakaswa kwa kuzingatia miongozo ya utakasaji iliyotolewa na wizara na ufanyike angalau masaa 72 kabla ya wanafunzi kuingia. 

“Siku ya kwanza ya kufunguliwa shule, chuo au taasisi ya elimu ni muhimu itumike kutoa elimu kwa wanafunzi/wanachuo na wafanyakazi wote kuhusu ugonjwa wa COVID-19 pamoja na dalili zake na hatua za kuchukua ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu,” inasomeka sehemu ya mwongozo huo.

Pia kuhakikisha uwepo wa vitakasa mikono na  vifaa vya kunawia mikono (sabuni na maji tiririka) kwa ajili ya usafi wa mikono katika maeneo ya madarasa, ofisi, mabweni, maktaba, bwalo la chakula, vyoo na maeneo mengine muhimu. 


Soma zaidi:


Waziri huyo ameagiza shule na vyuo vinavyotoa huduma za kulaza wanafunzi (bweni) zihakikishe kuna nafasi ya kutosha kati ya kitanda kimoja hadi kingine na kudhibiti uchangiaji vifaa kwa wanafunzi kama vile taulo, mashuka, vyombo vya kuogea na vifaa vya usafi wa mwili.

“Uongozi wa shule, chuo na taasisi za elimu zihamasishe wanafunzi, walimu na wafanyakazi wao kuvaa barakoa za vitambaa (Cloth masks) wakati wanaporudi shuleni au vyuoni. Aidha, wazazi/walezi wahimizwe kuwapatia watoto wao barakoa za vitambaa kabla ya kwenda shuleni/vyuoni,” amesema Ummy. 

Kwa shule na vyuo vyenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu, walimu wanapaswa kuvaa barakoa maalum zitakazoruhusu mwanafunzi mwenye matatizo ya usikivu kuwasiliana na mwalimu kwa ufasaha. 

Uchunguzi wa na usafiri

Ameagiza kuwa wanafunzi watakaohisiwa kuwa na dalili za COVID-19 wafanyiwe vipimo kabla ya kurudi shuleni au chuoni na watakaobainika kuwa na maambukizi wabaki nyumbani hadi hapo hali zao za afya zitakapoimarika. 

Zoezi hilo litaendelea hata baada ya kwenda shuleni au chuoni ambapo watakaobainika kuwa dalili za ugonjwa huo watatakiwa kufanyiwa uchunguzi na matibabu katika vituo vya afya vya karibu. 

Nao wamiliki wa magari ya Shule (School bus) waweke vitakasa mikono kwenye magari yao kwa ajili ya wanafunzi wakati wa kupanda kuelekea shuleni au Chuoni. 

Magari yanayobeba wanafunzi ni lazima yasafishwe na kuwa vitakasa mikono kwa ajili ya wanafunzi kutakasa mikono yao. Picha|Mtandao.

Ukaguzi na matumizi ya teknolojia 

Waziri Ummy amesema ziara za mafunzo nje ya shule zifanyike kwa kuzingatia tahadhari zote za kujikinga na maambukizi ya COVID-19 huku taasisi za elimu zikihimizwa kutumia Tehama katika kufundisha na kujifunzia ili kupunguza uwezekano wa maambukizi ya COVID-19.

“Wataalamu wa afya wa mikoa na halmashauri zote nchini wafanye ukaguzi wa mara kwa mara katika shule, vyuo na taasisi za elimu zilizoko katika maeneo yao ili kuhakikisha tahadhari zote za kujikinga na maambukizi ya COVID-19 zinazingatiwa kabla ya kufunguliwa shule/chuo na wakati wa masomo ikiwemo kutoa taarifa kwenye mamlaka husika,” amesisitiza Ummy.

Hata hivyo, mwongozo huu utaboreshwa mara kwa mara ili kukidhi mahitaji ya wakati husika.

Enable Notifications OK No thanks