Sanamu zinazohusishwa na ubaguzi wa rangi zaendelea kung’olewa duniani

June 13, 2020 8:10 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kuhusishwa na ubaguzi wa rangi pamoja na biashara ya utumwa.
  • Kati ya sanamu hiyo ni ya Mfalme Leopold aliyesababisha maumivu kwa mamilioni ya watu wa Congo DRC.
  • Baadhi ya sanamu hizo zitahifadhiwa katika makumbusho ya nchi husika baada ya kuchafuliwa na waandamanaji wanaopinga ubaguzi wa rangi.

Dar es Salaam. Sanamu ni kati ya vitu ambavyo vinatengenezwa kwa ajili ya kumbukumbu ya matukio na watu maarufu kwenye jamii ili kuwawezesha kujua historia ya mambo yaliyopita.

Sanamu zingine zimetengenezwa kuwakilisha vitu muhimu kama uhuru wa nchi fulani na huwa ni kivutio kikubwa cha shughuli za utalii. 

Kati ya sanamu maarufu ni ile ya “Statue of Liberty” ya Marekani inayoashiria uhuru wa Taifa hilo  na ile ya “Cristo Redentor” iliyopo Brazil inayowakilisha msalaba kwa waumini wa dini ya Kikristo.

Hata hivyo, hivi karibuni kumeibuka mivutano baina ya waandamanaji wanaopinga ubaguzi wa rangi (#BlackLivesMatter) duniani ambao wamefikia hatua ya kutaka baadhi ya sanamu ziondolewe hasa zinazowakilisha ubaguzi wa rangi.

Mpaka sasa, sanamu zaidi ya tano zimeondolewa nchini Marekani ambazo kwa mujibu wa wadau wa historia nchini humo, zilisimikwa mwishoni mwa karne ya 19 zikiwa zina nia ya kuwakumbusha Wamarekani weusi (wenye asili ya Kiafrika) kuwa Wamarekani weupe ndiyo watawala wa nchi hiyo.

Waandamanaji hao ambao wanapinga ubaguzi dhidi ya watu weusi na kung’oa sanamu hizo baada ya Mmarekani mweusi George Floyd kufariki dunia wakati akidhibitiwa na polisi nchini humo. 

Kifo cha Floyd kimeibua mijadala na maandamano katika maeneo mbalimbali duniani. 


Soma zaidi: 


Sanamu zingine zilizong’olewa

Sanamu ya Edward Colston ambayo ilikuwepo katika Jiji la Bristol nchini Uingereza ni ukumbusho wa mfanya biashara ya utumwa enzi za biashara hiyo. 

Sanamu hiyo iling’olewa Juni 7, 2020 na kutupwa kwenye mto na waandamanaji.

Sanamu nyingine ni ile ya Mfalme wa zamani wa Ubelgiji, Leopold II aliyetawala nchi ya Ubelgiji kuanzia mwaka 1865 hadi 1909 ambayo iliangushwa baada ya waandamanaji kurejea historia ya mfalme huyo aliyedaiwa kuwatesa Waafrika katika nchi ya Congo DRC.

Sanamu hiyo ambayo iliwekwa miaka 150 iliyopita imeondolewa  Juni 9, 2020 baada ya waandamanaji kuhusisha historia yake na ubaguzi wa rangi na Serikali ya Ubelgiji imesema itahifadhiwa katika makumbusho.

Mfalme wa zamani wa Ubelgiji, Leopold II iliyoangushwa chini na waandamanaji nchini Ubelgiji. Picha| Designboom. 

Waandamanaji waliimwagia rangi nyekundu sanamu ya mtawala huyo iliyopo katika jiji la Antwerp ikiashiria ubaguzi wa rangi na kumwaga damu ya watu wasio na hatia.

Mfalme Leopold II pamoja na majeshi yake alivamia Congo DRC na kusababisha vifo vya mamilioni ya raia wa nchi hiyo. Na kwa miaka mingi, wananchi wa Ubelgiji wamefundishwa kuwa nchi hiyo imechangia kwenye kustaarabisha bara la Afrika.

Sanamu zingine zilizotolewa ni ya Kamanda wa Jeshi la Confederate nchini Marekani Robert  Lee ambaye aliongoza mapigano yaliyochochewa na biashara ya utumwa, 

Sanamu ya kiongozi Williams Wickham katika mji mkuu wa Virginia, Marekani pamoja na sanamu ya Mfanyabiashara ya utumwa Robert Milligan huko West India Quay, Uingereza nazo zimeangushwa. 

Aidha, waandamanaji wametoa orodha ya sanamu 60 nchini Uingereza ambazo zinapaswa kuondolewa.

Orodha hiyo imewasilishwa baada ya Meya wa Jiji la London kuagiza kufanyika kwa mapitio ya sanamu zote jijini humo.

Sanamu ziilizopendekezwa ni pamoja na sanamu za Francis Drake, Nancy Astor, Christopher Columbus na William Gladstone.

Enable Notifications OK No thanks