Unyanyasaji kingono: Jinamizi la afya ya akili

June 20, 2020 6:54 am · Joshua
Share
Tweet
Copy Link
  • Kumbukumbu za matukio hayo hukaa kwa muda mrefu katika ubongo wa mwanadamu.
  • Humfanya mtu kujiona hana thamani, mpweke na asiyestahili kuchangamana na watu wengine. 
  • Unachohitaji ni msaada wa kisaikolojia na utakuwa sawa. 

Asaalam wa-aleykum! 

Huenda ninapoandika makala hii moyo wangu ndiyo kidogo unapata japo ahueni ya maumivu na masikitiko yatokanayo na tafakuri nzito na kuguswa zaidi na matukio ya siku za hivi karibuni yanayohusisha ukatili na unyanyasaji wa kingono kwa vijana wa kike na kiume. 

Masikitiko yangu yanachochewa zaidi na namna ambavyo vitendo hivi huacha makovu katika afya za wahanga hawa hususani afya ya akili. 

Wengi huwalazimu kuishi na maumivu na majuto na masikitiko ambayo husababisha athari katika mjumuiko wao kijamii, kielemu nk.

Siyo utamaduni hasa kwa Afrika kutilia maanani suala la afya ya akili. Mara nyingi matatizo kama mkazo, sonona na msongo huonekana kama yasio na ulazima wa kupatiwa ufumbuzi. 

Hali hii inasababisha wahanga na wenye changamoto hizi kujificha na kushindwa kujitokeza wapate msaada na matatizo haya yamekua yakiwaandama na kuathiri utendaji wao na namna wanavohusiana na watu wao wa karibu na jamii kwa ujumla. 

Sio lengo langu kuongelea hili kwa sasa, turudi kwenye msingi wa Makala hii.

Sitaki kugusa wala kuingilia wigo wa kisheria au kiusalama wa namna wanavopaswa kufanya kazi bali nataka kugusia upande wa afya ambao ndio taaluma yangu. Upande huu unawagusa wahanga wa unyanyasaji wa kingono. 

Unyanyasaji hujenga kumbukumbu isiyofutika katika akili ya mtu na kumjeruhi kisaikolojia. Picha|DW

Akili inavyoumizwa na unyanyasaji wa kingono

Akili ya mwanadamu imeumbwa kutunza kumbukumbu ambazo hutusaidia kufanya kazi na kuishi kila siku maana bila kumbukumbu ni dhahiri hata nyumbani tungesahau. Vivyo hivyo mtiririko wa matukio hutunzwa ndani ya seli za ubongo katika mfumo wa kumbukumbu. 

Matukio ya unyanyasaji wa kingono huingia katika mfumo wa utunzwaji wa kumbukumbu. Lakini hizi siyo kumbukumbu nzuri, ni sawa na zile za kupoteza mpendwa, kushindwa katika jambo ambazo mara nyingi tunapozikumbuka hutukosesha amani. 

Lakini hii ina utofauti zaidi  kidogo maana huingia katika kumbukumbu za matukio hasi ya kuumizwa (traumatic memories) ambazo huathiri mfumo mzima wa namna ambavyo muhusika atakavyoishi na watu kwenye jamii. 

Mara nyingi kumbukumbu hizi humjengea mtazamo hasi kwenye jamii au kwa watu fulani.

Mhusika huwa na hali ya kujihisi hafai, kana kwamba ni wa ajabu au yuko uchi kisaikolojia. Akili yake hulifanya tukio hili kama nguzo ya utendaji wake. 

Ni ngumu kuwa na uwezo wa kawaida wa kuishi na watu na mara nyingi hulazimika kuweka maigizo ilimradi asionekane wa tofauti. Lakini kiuhalisia ndani ya mioyo yao huwa wanatafunwa taratibu.

Changamoto nyingine ni uoga. Mara nyingi matukio haya yanapotokea hufunikwa na kiremba kwa sababu zisizo za mashiko ama kuficha aibu au muhusika kutishiwa na mtendaji kutosema. 

Hivyo maisha yake yote huibeba siri hii ndani ya akili yake na kusumbuliwa maradufu na mzigo mzito. Hii huwajengea uoga wa kutafuta msaada na ujasiri wa kusema jambo hilo. 

Kihoro kisichoisha na hofu hutanda ndani ya mioyo yao kila wanapopata kumbukumbu hizi mbaya.


Soma zaidi: 


Mahusiano ya kimapenzi huingia doa

Adha kubwa nyingine ni mahusiano yao. Kumbukumbu hizi huathiri sana namna wanavyohusiana na watu hasa wa jinsia tofauti hususani ile inayoendana na mtenda wa lile tukio. 

Ikiwa ni mahusiano ya kimapenzi, wahanga hawa hupatwa na woga, kukosa uhuru maana ni kama wanatonesha kidonda cha zamani hali ambayo husababisha kuzorota kwa mahusiano yao au kuharibika zaidi. 

Kupendelea upweke, kushindwa kujumuika, kupiga hatua na kupata mawazo mabaya ikiwemo ya maamuzi magumu ya kujiumiza ama kuondoa uhai ni changamoto wanazokutana nazo. Hujiona wameshuka thamani na kwamba hawastahili tena, yote haya ni madhila ya kuzorota kwa afya ya akili itokanayo na msongo.

Ubongo wa mwanadamu ni kiungo chenye nguvu sana. Akili ina uwezo wa kubeba matukio mengi lakini yale yanayousumbua ufahamu kama haya huathiri utendaji kazi na ufanisi wa ubongo katika kazi zingine muhimu. Na hii ni hatari kwa uzalishaji mali, elimu, mahusiano ya kijamii nk.

Iwapo unatambua unapitia wakati mgumu kama huo, tambua ya kwamba wewe ni shujaa na ni mshindi. Picha| Pychology Today.

Tiba ya afya ya akili

Habari njema ni kwamba, matatizo kama haya hutibika kwa msaada wa kitabibu na ule wa kisaikolojia. Wazazi na jamii itambue ya kuwa watu waliopatwa na changamoto kama hizi wanahitaji msaada wa kiafya kama ilivyo kuumwa malaria ama kikohozi. 

Huduma zipo na ni rafiki sana. Zitawawezesha kuendana na hali waliyopata na kuweza kurejea ufanisi wao wa awali.

Iwapo unatambua unapitia wakati mgumu kama huo, tambua ya kwamba wewe ni shujaa na ni mshindi. 

Zaidi tambua ya kwamba hauko peke yako kokote ulipo. Fahamu ya kwamba wahudumu wa afya tupo kwa ajili yako kukusaidia na kukuvusha kwa pamoja katika changamoto hiyo unayopitia.  

Usiogope na wala usijifiche, wewe ni wa thamani sana na thamani yako haijawahi kushuka. Unachohitaji ni msaada wa kisaikolojia na utakua sawa. Chukua maamuzi sasa ya kuutafuta msaada huo. Wewe ni shujaa.

Nipo !!!!

Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) na Mkurugenzi wa Indigo Afya. Hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, baruapepe: joshualameck9@gmail.com.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV