Majaliwa awataka mabosi Afrika kushughulikia afya ya akili

November 4, 2024 6:48 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema afya ya akili ni miongoni mwa changamoto inayozungumziwa sana kwa sasa.
  • Awasisitiza kusimamia rasilimali watu ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Arusha. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka mameneja rasilimali watu katika utumishi wa umma barani Afrika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazolikumba makundi wanayoyaongoza katika nchi zao ikiwemo afya ya akili.

Majaliwa anatoa kauli hiyo ikiwa ni wiki chache tangu kufanyika kwa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya afya ya akili duniani yaliyokuwa na kauli mbiu inayotoa kipaumbele afya ya akili mahali pa kazi.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Mwaka 2019, takribani watu bilioni 1 wakiwemo asilimia 14 ya vijana wote duniani walikuwa wanaishi na tatizo la afya ya akili ambapo mtu mmoja  kati ya 100 hujiua na asilimia 58 ya wanaojiua ni watu wenye umri wa chini ya miaka 50. 

Barani Afrika, WHO inabainisha kuwa takriban watu milioni 116 walikadiriwa kuwa na matatizo ya afya ya akili mwaka 2022.

Kwa kutambua changamoto hiyo, Majaliwa aliyekuwa akizungumza katika mkutano wa mameneja wa rasilimali watu katika utumishi wa umma barani Afrika uliofanyika jijini Arusha leo Novemba 4, 2024 amesema suala la afya ya akili kwa watumishi wa umma Afrika linapaswa kuzingatiwa.

“Mzingatie lile ambalo sasa linazungumzwa, suala la afya ya akili kwa rasilimali watu…tuhakikishe kwamba watumishi wetu wanakuwa tayari kukabiliana na msongo wa majukumu kwa kukaa nao kuwasikiliza na kupanga mpango mzuri utakaowawezesha kutekeleza majukumu yao,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa akizungumza na wahudhuriaji wa mkutano wa tisa wa mameneja wa rasilimali watu Afrika katika ukumbi wa kimataifa AICC, Arusha. Picha|OWM.

Majaliwa amewasisitiza viongozi hao kusimamia vyema kundi la rasilimali watu katika nchi zao ili kuhakikisha utolewaji wa huduma bora kwa wananchi.

“Mustakabali wa huduma za umma wa Afrika unategemea uwezo wa usimamizi wa rasilimali watu katika kubuni, kuongoza na uadilifu…kusimamia rasilimali watu kunatoa huduma za hali ya juu zinazozingatia mahitaji ya wananchi katika maeneo yetu,” ameongeza Majaliwa.

Awali Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema mkutano huo unatoa fursa kupata majibu ya changamoto zinazoikabili sekta ya rasilimali watu Afrika.

“Tunaamini kwa siku hizi tatu ambao watumishi hawa wako hapa watapata fursa ya ‘kuinteract’ (kuingiliana) lakini pia watapata fursa ya kuwa na bunifu katika kila aspect (nyanja) ya maendeleo ya kiuchumi ya kijamii na kisiasa…

…Rasilimali watu ndiyo rasilimali muhimu namba moja katika nchi yoyote na katika bara lolote zaidi katika maendeleo ya nchi,” amesema Simbachawene.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks