Magufuli aeleza sababu za kuwafuta kazi RC, DC Arusha

June 22, 2020 12:20 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Sababu kuu ni kutokuwepo kwa maelewano baina ya viongozi waliotenguliwa.
  • Ameagiza viongozi wapya kuwajibika na kutokufanya makosa kama yaliyofanywa na viongozi walioondolewa.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameeleza sababu mbalimbali za kutengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo na viongozi wengine wawili wa mkoa huo ikiwemo kushindwa kuelewana na kutimiza majukumu yao. 

Juni 19 Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na alimteua Idd Kimanta kushika nafasi hiyo. 

Kabla ya uteuzi huo Kimanta alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli mkoani humo.

Pia Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqarro na alimteua Kenan Kihongosi kuwa kushika nafasi hiyo.

Kabla ya uteuzi huo, Kihongosi alikuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Iringa.

Mwingine ambaye uteuzi wake ulitenguliwa ni Mkurugenzi Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dk Maulid Madeni na nafasi yake imechukuliwa na Dk John Pima. 

Kabla ya uteuzi huo, Dk Pima alikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora.

Dk Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Juni 22, 2020) wakati akiwaapisha wateuliwa wapya, amesema viongozi waliotenguliwa nyadhifa zao walishindwa kuwajibika kwa viapo vyao vya kazi kwa sababu kila mtu alijiona ni bosi kwa mwenzake.

“Utakumbuka hivi karibuni Arusha ilibidi nitengue uteuzi wa wote niliokuwa nimewateua kuanzia RC, Mkurugenzi wa mji pamoja na DC ni kwa sababu katika kipindi cha karibu miaka miwili walikuwa wanagombana tu, kila mmoja ni bosi, kila mmoja anatengeneza mizengwe ya mwenzake. Sikufurahishwa” amesema Dk Magufuli.

Rais Magufuli Amewataka wawe na ushirikiano mzuri na viongozi wenzao watakaowakuta katika nafasi zao mpya na kuwasihi waepukane na mabishano pamoja na kugombana. Picha| EAtv

Aidha, Rais amewaagiza viongozi waliopishwa leo kuchapa kazi na kuridhika na nafasi walizopewa.

“Ninachowaomba mkafanye kazi, na ikiwezekana mkaridhike na mlichonacho. Kwa sababu tatizo lingine la vijana unapompa nafasi wana tendency ya kutoridhika na hizo nafasi wanashindwa kuelewa miaka bado ipo mingi sana. Sasa mkaridhike na kazi mliyonayo mkawatumie Watanzania” Amesema Magufuli.

Amewataka wawe na ushirikiano mzuri na viongozi wenzao watakaowakuta katika nafasi zao mpya na kuwasihi waepukane na mabishano pamoja na kugombana.

Kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Idd Kimanta, Dk Magufuli amemsisitiza kusimamia migogoro ya mkoa huo huku akisema migogoro mingine imekuwa ikitengenezwa kwa makusudi.

Mkurugenzi mpya naye ameagizwa kukamilisha ujenzi wa stendi katika Halmashauri hiyo.

“Ile stendi iliyopangwa kujengwa, sasa hiyo issue (suala) ya stendi ikaishe. Ile stendi ni ya watanzania wote. Kama ni kubishana na kugombana, kagombane na mke wako na watoto wako lakini ndani ya Serikali hapana,” amesisitiza Magufuli.


Zinazohusiana


Vyombo vya dola navyo vyapewa maagizo

Magufuli ametoa onyo kwa Kamanda waPolisi wa Mkoa wa Arusha (RPC) pamoja na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wa Mkoa wa Arusha akiwasisitiza kufanya kazi alizowaagiza na siyo kazi wanazojipangia.

“Nao leo ilikuwa niwatoe. RPC pamoja na Mkuu wa Takukuru wa Arusha. Nimeamua kuwasamehe lakini sijawasamehe moja kwa moja wakifanya kosa lolote wataondoka. Nataka wakafanye kazi nilizowatuma, siyo kazi wanazojituma wao,” amesema Rais Magufuli.

Enable Notifications OK No thanks