Sony Xperia 1ii: Simu inayokuhakikishia kumbukumbu za kudumu za maisha
- Ni simu yenye kamera tatu kukupatia picha zenye ubora wa hali ya juu kwa ajili ya kumbukumbu za kudumu.
- Betri lake lina uwezo wa kukaa hadi siku mbili japo inategemeana na matumizi yako.
- Pochi yako inatakiwa iwe sawa kumiliki simu hii inayouzwa zaidi ya Sh2 milioni.
Dar es Salaam. Huenda baada ya kuona kichwa cha habari hii ulibaki na mshangao na kujiuliza kama kampuni ya Sony bado inatengeneza simu. Ndiyo, bado inatengeneza!
Mbali na kampuni zingine zilizopo ambazo zinazotoa simu kwa ajili ya matumizi mbalimbali, Sony imejikita kutoa simu ambazo zinawafaa watengeza maudhui hasa ya mtandaoni (Video na picha)
Na hii ndiyo sababu inayotuvuta kuchambua simu ya Sony Xperia 1ii iliyotolewa Februari, 2020 na kampuni ya kutengeneza vifaa vya kielektroniki ya Sony.
Je, Ni kipi kimezingatiwa na Sony katika kutengeneza simu hii?
Kasi ya kamera kufokasi kitu na mtu (Auto focus)
Hakuna kitu muhimu kwa mtengeneza maudhui ya picha na video kama kuwa na kamera ambayo inaweza kung’amua picha kwa haraka hata wakati anapiga picha ya kitu ambacho kinatembea.
Xperia 1ii inakuja na kamera tatu zenye ukubwa wa Megapikseli 12 (MP12) ambapo moja ni kwa ajili ya kupiga picha kwa mapana (wide angle), kamera ya pili ni kwa ajili ya picha za mbali na ya tatu ni kwa ajili ya picha za mapana zaidi.
Kamera yake ya mbele ina ukubwa wa MP nane.
Xperia 1ii inakuja na kamera tatu zenye ukubwa wa Megapikseli 12 (MP12). Picha| YouTube.
Ina uhifadhi mkubwa
Kabla ya kufahamu ukubwa wa uwezo wa uhifadhi wa simu hii, Jiulize simu yako inahifadhi vitu kwa ukubwa gani.
Uhifadhi huo utamuwezesha mtumiaji kurekodi video na kupiga picha nyingi bila ulazima wa kuzifuta na kuzihamisha.
Baada ya hapo, fahamu kuwa Xperia 1ii ina uwezo wa kuhifadhi vitu vyenye ukubwa wa jigabaiti 256 (GB) kwa uhifadhi wa kawaida huku ikiambatana na sehemu ya kuweka kadi ya uhifadhi (memory card) na GB8 ya uhifadhi wa ndani (RAM).
Uhifadhi huo ni sawa na simu ya LG V60 ThinQ na OnePlus 8 Pro ambazo pia zinatamba kwa kuwa na sehemu kubwa ya kuhifadhi vitu.
Nguvu ya betri
Xperia 1ii ina betri lenye uwezo wa mAh 4000 ambalo linaweza kukaa hadi siku mbili kulingana na matumizi yako ambapo ni nzuri kwa mtengeneza maudhui ya video na picha.
Hata hivyo, kwa upande wa betri inaweza isiwe jambo geni kwani ikilinganishwa na LG V60 thin Q yenye betri lililo na uwezo wa mAh 5000 na Samsung Galaxy S20 iliyo na betri lenye uwezo wa mAh 4500.
Simu hiyo inayochajiwa na Chaja aina ya USBC, inaweza kuchaji bila kutumia mfumo wa waya.
Zinazohusiana
- Sifa za simu mpya za Samsung zilizoingia sokoni Agosti 7
- Upo tayari kununua simu ya mkononi ya zaidi ya Sh3 milioni?
- Samsung, Huawei zinavyochuana katika soko la simu duniani
Mbali na hivyo vyote, simu hii pia ina uwezo mzuri wa sauti kwani ina spika za “sterio” pamoja na sehemu kwa ajili ya kuwekea spika za masikioni (earphones).
Uzito wake ni gramu 181.4 huku ikiwa inaruhusu matumizi ya laini moja tu ya simu. Pia ina uwezo wa kuruhusu mtandao wa 5G huku ikitumia mfumo endeshi wa Android kizazi cha 10.
Xperia 1ii haina redio na inapatikana kwa rangi nyeusi na zambarau.
Kuimiliki, siyo haba kwani inabidi ujipange na uwe na mtonyo unaoeleweka. Xperia 1ii inauzwa Sh2.77 milioni.
Kama hutaki kupitwa na matoleo ya simy kutoka Sony, basi wakati huu ndio wakati mwafaka kuinyakua simu hii na kufurahia maisha kwa kumbukumbu nzuri za picha.