Buriani Mkapa: Mwamba uliofanya mageuzi makubwa ya kiuchumi Tanzania

July 28, 2020 11:06 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Atakumbukwa kwa kujenga misingi ya uchumi iliyosaidia kuboresha maisha ya Watanzania.
  • Alifuta kodi mbalimbali ikiwemo ya kichwa na baiskeli.
  • Aliimarisha diplomasia ya kimataifa, akiba ya fedha za kigeni na kupunguza deni la Serikali. 
  • Atazikwa kesho Julai 29 kijijini kwao Lupaso mkoani Mtwara. 

Dar es Salaam. Ilikuwa ni huzuni na simanzi katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam wakati Rais John Magufuli, viongozi kutoka nje ya nchi na Watanzania walipokuwa wakitoa heshima za mwisho kwa Rais mstaafu wa awamu ya tatu wa Tanzania, Hayati Benjamin Mkapa. 

Uwanja huo kwa sehemu kubwa ulitawaliwa na mavazi ya rangi nyeusi ikiwa ni ishara ya huzuni ya kuondokewa na mpendwa wao ambaye aligusa maisha ya watu wengi kwa namna tofauti.

Kiongozi huyo, aliyeiongozaTanzania kati ya mwaka 1995 na 2005, atakumbukwa kwa mengi ikiwemo kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi ambayo yamechangia kujenga msingi wa kuboresha maisha ya Watanzania katika nyanja mbalimbali. 

“Watanzania wengi wanamkumbuka Mzee Mkapa kwa mageuzi makubwa ya kiuchumi aliyoyafanya,” amesema Rais John Magufuli leo wakati akitoa hotuba mbele ya waombolezaji.

Wakati anaingia madarakani mwaka 1995, Tanzania ilikuwa kwenye matatizo ya kiuchumi kutokana na kuwepo kwa deni kubwa la Serikali, jambo  lililofanya taasisi nyingi za fedha za kimataifa na nchi nyingi wahisani kusitisha kutoa mikopo na misaada kwa Tanzania. 

Kutokana na uwezo wake wa uongozi na diplomasia, Mkapa alianza kulipa madeni na kuanza kuzishawishi taasisi za kimataifa kusamehe madeni yake kwa Tanzania ili kuiwezesha kujitegemea na kuwaletea wananchi maendeleo.

“Jitihada hizo zilizaa matunda ambapo nchi yetu iliweza kusamehewa madeni ya Dola za Marekani  3 bilioni (Sh1.3 trilioni) kati ya Dola za Marekani 7 bilioni (Sh3.1 trilioni) mpango uliosimamiwa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF),” amesema Rais Magufuli.

Sehemu ya uwanja wa huru ambako Watanzania walikusanyika kutoa heshima za mwisho kwa Hayati Benjamin Mkapa. Picha| Daniel Samson. 

Mzee Mkapa aliyefariki akiwa na miaka 81 alibuni na kutekeleza mipango na mikakati mbalimbali ya kuwakomboa wananchi kiuchumi ukiwemo wa Mkakati wa Kupunguza na Kuondoa Umaskini Tanzania (MKUKUTA), Mpango wa Kurasimisha Mali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) pamoja na Mpango wa Kusaidia Kaya Maskini Tanzania (TASAF).

Mathalan, utekelezaji wa mpango wa Tasaf uliofikia awamu ya tatu tangu uanze mwaka 2000 hadi utakapokamilia mwaka 2023, utakuwa umetumia Sh4.109  trilioni ili kuwawezesha wananchi wanyonge kuinikia kiuchumi.

“Ilikuwa wakati wa Mzee Mkapa ambapo kodi ya kichwa ama kodi ya kujitegemea ilifutwa. Kwa waliokuwepo watakumbuka kodi hii ilikuwa ikisibabisha mateso na usumbufu mkubwa kwa wananchi ambao baadhi ya watu walidiriki hata kukimbia nyumba au familia zao kwa sababu ya kodi hizo,” amesema Dk Magufuli wakati akielezea mchango wa Mkapa wakati wa uongozi wake.

Pia, Mkapa ambaye alifariki Julai 23, 2020 jijini Dar es Salaam alifuta kodi ya baiskeli pamoja na kodi za mifugo. 

Uendelezaji wa sekta binafsi

Kutokana na umuhimu wa sekta binafsi katika uchumi wa Tanzania, Rais Magufuli amesema katika kipindi cha uongozi wake ndipo Baraza la Taifa la Biashara Tanzania (TNBC) lilianzishwa ili litumike kama jukwaa la majadiliano kati ya Serikali na sekta binafsi. 

Moja ya kazi kubwa aliyofanya ni kuanzishwa kwa benki mbili za biashara za Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na NMB ambazo ni miongoni mwa benki kubwa nchini ambazo zinachangia kukuza sekta ya fedha na uwekezaji.


Zinazohusiana:


Alianzisha taasisi mbalimbali za kujitegemea

Baadhi ya taasisi za umma ambazo zilianzishwa wakati wa uongozi wa Mkapa ambazo ziliiwezesha nchi kujitegemea ni pamoja na Bodi ya Mfuko wa Barabara pamoja na Wakala wa Barabara (TANROADS) ambazo zilianzishwa mwaka 2000.

Taasisi hizo, kwa mujibu wa Rais zilikuwa chachu ya ujenzi wa barabara za lami na madaraja nchini ikiwemo barabara ya Dar es Salaam-Nangurukuru na ukarabati wa barabara ya Dar es Salaam-Morogoro. 

Dk Magufuli amesema mzee Mkapa pia ndiye aliyesimamia uanzishwaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kudhibiti mfuko wa bei kutoka silimia 27 mwaka 1995 hadi kufikia wastani wa asilimia 10 mwaka 2005.

“Aliongeza fedha za kigeni kutoka akiba yenye kutosheleza mahitaji ya mwezi mmoja mwaka 1995 hadi kufikia miezi 5.3 mwaka 2005 wakati anaondoka madarakani,” amesema Rais Magufuli huku waombolezaji wakiwa watulivu kuonyesha walivyoguswa na msiba huo wa Taifa.

Mzee Mkapa bado ana mengi ya kukumbukwa kwa sababu Dira ya Taifa ya Maendeleo iliyolenga kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati mwaka 2025 ilianzishwa wakati wa uongozi wake na ndoto hiyo imetimia kabla ya muda uliotarajiwa. 

Rais John Magufuli, viongozi kutoka nje ya nchi na Watanzania leo wametoa heshima za mwisho kwa Rais mstaafu wa awamu ya tatu wa Tanzania, Hayati Benjamin Mkapa. Picha| Daniel Samson. 

Alivyoimarisha huduma za jamii

Alianzisha Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Elimu ya Sekondari (MMES). Pia, alianzisha Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (MEMKWA), Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Baraza la Mitahani la Tanzania (NECTA), Kamisheni ya Vyuo Vikuu (TCU) na kuifanya Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi Tanzania (VETA) kuwa taasisi inayojitegemea. 

“Watanzania hawatamsahau Mzee Mkapa kwa kuwajengea uwanja mkubwa wa michezo tunaouona mbele yetu. Kwa sasa wengi wanataka uwanja ule uitwe uwanja wa Mkapa au Mkapa Stadium.

“Ninajua Mzee Mkapa hakupenda vitu vingi viitwe kwa jina lake lakini kwa sababu nimepokea meseji nyingi na kwa sababu sasa hawezi kuniadhibu chochote, yeye amelala hapo basi natamka uwanja huo utaitwa Mkapa Stadium,” amesema Rais Magufuli ikiwa ni shukrani za kutambua mchango wa Mkapa katika uboreshaji wa huduma za jamii nchini. 

Baada ya hotuba ya Rais Maguli uwanjani hapo familia, ndugu na viongozi mbalimbali walitoa heshima za mwisho na mwili wa marehemu umesafirishwa kuelekea mkoani Mtwara. 

Atapumzishwa katika nyumba yake ya milele kesho Julai 29, 2020 katika kijijini kwao Lupaso wilayani Masasi, Mtwara.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV