Jinsi wajawazito wanavyoweza kuepuka vitu visivyofaa mwilini

September 26, 2020 10:13 am · Joshua
Share
Tweet
Copy Link
  • Ulaji wa vitu kama udongo, chaki huathiri afya ya mama mjamzito.
  • Hiyo ni ishara kuwa, mama mjamzito umepungukiwa na madini ya chuma na vitamini.
  • Njia rahisi ya kuacha vitu hivyo kupata ushauri wa daktari na kula mlo kamili.

Ni Ijumaa katika moja ya kliniki zangu, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam, Wilaya ya Kigamboni, katika majadiliano na mmoja wa wagonjwa wangu ananieleza kuwa mkewe anapenda kula vitu ambavyo siyo vyakakula. 

Ananitajia vitu hivi: mchanga, udongo na wakati mwingine chaki. 

Mwanaume huyo anasema mke wake amepata ujauzito wa kwanza na kwa sasa una miezi mitatu ya mwanzo. Kitaalam, hali hiyo huitwa Pica.

Pica ni hali ya mtu kuwa na hamu ya kula vitu ambavyo kimsingi siyo vyakula na wala havina mchango wowote katika lishe. Pica ni neno la Kilatini ambalo humaanisha ndege aitwaye “Magpie” ambaye hula karibia kila kitu. 

Tabia zilizozoeleka za Pica ni pamoja na kutamani kula mchanga, barafu (Ice Cream), udongo, chaki na mkaa. 

Sababu ya kupatwa na hali hiyo kwa wanawake wajawazito haiko wazi wala haina mlengo mmoja wa kimantiki. 

Wakati mwingine mjamzito hujikuta akitamani kula vitu ambavyo siyo vya kawaida ikiwemo chaki, jambo linaloashiria upungufu wa madini ya chuma mwilini. Picha| Happy Family. 

Hata hivyo, Pica huhusishwa na upungufu wa madini ya chuma au vitamini ambayo mwili hauwezi kupata kwa njia ya chakula cha kawaida. 

Hali hii ni ya kawaida kutokea na haina haja ya kushtuka. Hata hivyo, ni muhimu kuzingatia aina ya vitu ambavyo mama mjamzito anatumia. 

Kuna uwezekano mkubwa matumizi ya vitu hivi vikaathiri afya ya mama na mtoto iwapo vikiwa vimeingiliana na bakteria au vitu vyenye madini yenye viambata sumu.


Soma zaidi: 


Ufanye nini unapopatwa na hali hii?

Kuna mambo muhimu ya kufanya unapopatwa na hali hii ili kujiweka salama wewe na mtoto wako aliyepo tumboni:

Mfahamishe mtoa huduma wa afya anayekuhudumia ili akupe elimu kuhusu aina ya vitu unavyotamani kula na hatari zinazoweza kuwepo kwako na kwa mtoto aliye tumboni mwako. 

Hiyo itamsaidia kupitia kwa undani rekodi za ujauzito wako hasa mwenendo wa ulaji wa chakula ikiwemo madini ya chuma, vitamini na madini mengineyo muhimu kwenye mwili wako. 

Unaweza kutafuta mbadala wa vitu vingine ambavyo unatamani kula ili kupunguza hamu ya ulaji wa vitu ambavyo siyo lishe na vinavyoweza kuwa hatarishi kwa afya yako. 

Tumia vitu vya kutafuna kama “Big G” na kulamba sukari ili kudhibiti arosto itokanayo na Pica. 

Mume na ndugu wanatakiwa kukaa karibu na mama mjazito ili kumsaidia kuacha kula vitu ambavyo ni hatari kwa afya yake na kuhakikisha anapata chakule bora ambacho kitamsaidia kukidhi mahitaji ya mwili wake. 

Kwa msingi huo, ni muhimu kwa wajawazito kuzingatia kanuni za afya na kumuona daktari kwa wakati ikiwemo kuhudhuria kliniki kila inapobidi.

Nipo!

Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) na Mkurugenzi wa Indigo Afya. Hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.

Enable Notifications OK No thanks