Sh44.1 bilioni za Uswiss zitakavyonufaisha kaya masikini Tanzania
- Zitasaidia kuboresha huduma za afya na elimu.
- Pia zitakuwa chachu ya kuimarisha nguvukazi ya watu kwenye kaya masikini.
- Serikali yasema itahakikisha fedha hizo zinatumika kama zilivyokusudiwa.
Dar es Salaam. Watanzania hasa wale wanaoishi katika kaya masikini wana kila sababu ya kutabasamu kutokana na msaada wa Sh44.1 bilioni uliotolewa na nchi ya Uswiss ili kuboresha nguvukazi na huduma za jamii ikiwemo afya na elimu Tanzania.
Msaada huo ni kwa ajili ya awamu ya pili ya mpango wa kunusuru kaya masikini chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2020 hadi 2023 na kuchangia Mfuko wa Pamoja wa Afya kwa mwaka wa fedha 2020/21.
Mikataba wa misaada hiyo imesainiwa jijini Dodoma Oktoba 6, 2020 na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa Uswiss nchini Tanzania, Didier Chassot kwa niaba ya Serikali ya Uswiss.
James, amesema kati ya fedha zilizotolewa, Sh39.15 bilioni ni kwa ajili ya Tasaf ambapo zitasaidia kuboresha maisha ya kaya masikini Tanzania.
“Msaada kwa ajili ya Tasaf utasaidia kupunguza umasikini na kuboresha nguvukazi, kuboresha uwezo wa kununua mahitaji ya kaya masikini, kuongeza uandikishwaji wa watoto shuleni na kuimarisha huduma za jamii,” amesema James.
Fedha zilizobaki ambazo zitaenda katika Mfuko wa Pamoja wa Afya zitasaidia kuboresha utendaji wa watoa huduma ya afya ya msingi, kuhakikisha huduma bora za afya zinatolewa na kuwezesha utekelezaji wa mpango mkakati wa sekta ya afya pamoja na malengo yake.
Mfuko wa Afya wa Pamoja ulioanzishwa mwaka 1999 na umefanikiwa kuboresha huduma za afya katika zaidi ya kaya 184 Tanzania.
Soma zaidi:
- Tanzania yapokea msaada wa vifaa tiba kupambana na Corona
- Benki ya Dunia yaeleza sababu za kuipatia Tanzania mkopo wa Sh1 trilioni
Balozi wa Uswiss nchini Tanzania, Didier Chassot amesema fedha hizo zilizotolewa zitasaidia kutunisha mfuko huo ili kuongeza wigo wa utoaji wa huduma za afya nchini.
“Kusainiwa kwa makubaliano ya msaada wa leo kutaruhusu kuendelea kuchangia mpango wa afya kwa wote nchini na tutaendelea kuwekeza katika mfuko huu”, amesema Balozi Chassot.
Amesema wakati Tanzania inapiga hatua kiuchumi ni lazima pia kulinda maisha ya watu ambao hawajanufaika kikamilifu na ukuaji huo wa uchumi.
Mpango wa pili wa Tasaf ulioanza mwaka 2020/2021 umepanga kutumia Sh2.02 trilioni kuzifikia kaya masikini katika vijiji na mitaa ambayo haikufikiwa wakati wa kutekeleza mpango wa Tasaf awamu ya kwanza.
Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha na Mipango, mpango wa Tasaf awamu ya kwanza ulitekelezwa mwaka 2013 hadi mwaka 2019 ambapo kaya milioni 1.1 zenye watu milioni 5.3 katika Serikali za Mitaa 159 Tanzania Bara na Zanzibar, zilinufaika na ufadhili huo.
Pia hatua hiyo imewezesha watoto milioni 1.8 kuandikishwa elimu ya msingi na wanafunzi 448,409 wamesomeshwa elimu ya sekondari katika kaya 1.1 zilizonufaika.
Latest