Vimbwenga vya babu na mjukuu havijawahi kumuacha mtu salama
- Ni katika filamu ya “War With Grandpa” inayohusu mahusiano yanavyotengenezwa kati ya babu na mjukuu wake.
- Kufikia hatua ya maelewano, wawili hao wanalazimika kuingia kwenye vita baridi ya kusumbuana nyumbani.
- Vimbwenga na sokombingo zilizopo kwenye filamu hii zitakufanya ufurahie wikiendi yako.
Dar es Salaam. Baada ya mtoto wake kumuona kuwa kwa umri wake, hawezi kuishi peke yake, anaamua kushauriana na mwenza wake kuanza kuishi na babu yake.
Babu huyo anayejulikana kwa jina la Ed (Robert De Niro) anaamua kuhamia nyumbani kwa mtoto wake Sally (Uma Thurman) ambaye ni mama wa watoto watatu na mke wa Arthur (Rob Riggle).
Mambo hayo yote yanafanyika kwa amani na upendo lakini linapofikia suala la Sally kumhamisha chumba mtoto wake wa kiume ili ampishe babu yake, hapo ndipo vita inapoanzia.
“Ntaka kurudi chumbani kwangu,” anapiga kelele kijana Peter Decker (Oakes Fegley) akimwambia mama yake ambaye alimhamishia kwenda kwenye chumba kilichotumika kama stoo zamani.
Akiwa amelala, gari roboti inaingia chumbani kwake kufikisha ujumbe unaosomeka “Tangazo la vita! Nipatie chumba changu au ukubiliane na maswaibu yajayo.”
Kwa kuwa mzee huyo hajachukua chumba hicho kwa lazima, analazimika kuingia kwenye vita na mjukuu wake ambao wanategeana mitego ya hapa na pale kuona nani atabaki ulingoni.
Soma zaidi:
- Filamu ya Greenland: Baba alivyobebeshwa mzigo mzito wa kuiokoa familia
- Sababu za miguu kutoa harufu mbaya
- Vunja mbavu zako na filamu ya “Hubie Halloween”
Kukuta nyoka akiwa amelala, kudondoka na mlango, kubadilishiwa zana za usafi ni maswaibu anayokutana nayo Ed huku naye akimtega mjukuu wake kwa kumfungulia nati za viti, vitanda na hata meza.
Je nini kitakuwa mwisho wa vimbwenga hivi?
Tazama filamu hiyo ya “War with Grandpa” kupitia kumbi za kuangalizia filamu zikiwemo ukumbi wa Century Cinemax wa Aura Mall, Mlimani City na Dar Free Market kwa Sh10,000.