Filamu ya Greenland: Baba alivyobebeshwa mzigo mzito wa kuiokoa familia

October 30, 2020 7:03 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Inamhusu baba ambaye ana dhamira ya kuiokoa familia yake dhidi ya mvua ya vimondo inayoinyeshea dunia.
  • Ni nyota wa filamu Gerard Butler atakayekufundisha jukumu la baba katika familia.

Dar es Salaam. Unaweza kuiita siku hii jinsi upendavyo. Kiama, mwisho wa dunia au neno lolote lnalokuja kichwani mwako baada ya kufika siku ambayo hauna tumaini la kuiona kesho kwani hauna uhakika wa usalama wako hata kwa sekunde mbili zijazo.

Siku hiyo inaanza na wanafamilia wakiendelea na majukumu yao ya kila siku. Taarifa ya habari ikisema kuwa kimondo kipo njiani kudondokea sehemu ya dunia lakini kwa kuwa binadamu wameumbwa kuheshimu matukio na siyo habari, hata televisheni inazimwa.

“Wanasemaje huko?” John Garrity (Gerard Butler) anamuuliza mke wake juu ya kinachojiri kwenye taarifa ya habari.

“Yale yale,” Allison Garrity (Morena Baccarin) anamjibu mume wake.

Garrity na familia yake, wanajumuika na marafiki na majirani kutazama taarifa ya habari kuhusu kimondo ambacho kinatarajiwa kuangukia baharini.

Loh! yanayotarajiwa hayatokei. 

Kimondo kinaangukia kati kati mwa jiji la Florida nchini Marekani na hilo ni trela tu. Picha kamili, inakuja.

Safari ya Garrity kuhamisha familia yake na kuipeleka kwenye moja ya mahandaki pekee yaliyobaki kama tumaini la wengi inaanza. Hata hivyo, safari haiwi nyepesi kama inavyosimuliwa.

Kupotezana na familia yake, kulipuliwa kwa ndege wanazotarajia kuzipanda na kukoswa koswa na kimondo ni sehemu ya mapito anayokutana nayo akiwa kwenye zoezi la kuokoa mke na mtoto wake.

Taarifa ya habari nayo, haipo nyuma. Inatangazwa kuwa, kimondo kingine kikubwa kinatarajia kuanguka kwenye uso wa dunia ndani ya saa 24, haijulikani ni nini kitabaki kwenye uso wa dunia. 

“Ninaapa! Ninaweza kuifikisha familia yangu kwenye hilo handaki,” anasema Garrity.

Komando huyo maarufu kwa filamu zaidi ya 45 ikiwemo ya “London Has Fallen”, “Geostorm”, na “Den of Thieves” atafanikisha safari yake?


Soma zaidi:


Usikose filamu hii inayotamba kwenye kumbi za sinema za Century Cinemax zilizopo kwenye maduka makubwa jijini Dar es Salaam ikiwemo Mlimani City na Dar Free Market (DFM) kwa gharama ya Sh10,000.

Pia, unaweza kuitumia wikiendi yako kwa kupata mapumziko ya kutosha na kutumia muda vizuri na familia yako.  

Enable Notifications OK No thanks