Dar es Salaam kinara matokeo darasa la saba mwaka 2020

November 21, 2020 11:39 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Baada ya kuongoza kitaifa katika mitihani hiyo iliyofanyika Oktoba mwaka huu.
  • Ufaulu wa Dar ni juu ya wastani wa kitaifa kwa zaidi ya asilimia 10.
  • Simiyu yaongeza ufaulu kwa mwaka wa tatu mfululizo.

Dar es Salaam. Mkoa wa Dar es Salaam umeibuka kinara katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka 2020 baada ya kufanikiwa kupata ufaulu wa asilimia 93.5, ikiwa ni juu ya wastani wa ufaulu wa kitaifa wa asilimia 82.68.

Dar es Salaam ambalo ni jiji la kibiashara, kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa leo (Novemba 21, 2020) na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) Dk Charles Msonde umefaulisha watahiniwa 76,372 kati ya wanafunzi 81,677 waliofanya mitihani hiyo kutoka katika shule 671.

Arusha imeshika nafasi ya pili katika orodha ya mikoa 10 bora kitaifa baada ya kupata wastani wa ufaulu wa asilimia 92.42 ukifuatiwa na Simiyu wenye takriban asilimia 92.

Simiyu ni moja ya mikoa mashuhuri katika kuwafundisha wanafunzi wake kupitia mpango wa kuweka kambi za masomo ambao umekuwa ukipewa msukumo mkubwa na mkuu wa mkoa huo Antony Mtaka.

Simiyu ni miongoni mwa mikoa mitatu nchini iliyoongeza ufaulu wake kwa miaka mitatu mfululizo wakiwa sambamba na Mara na Lindi uliopo kusini mwa Tanzania.

Mkoa huo wa Simiyu umefuatiwa na Katavi uliopo Magharibi mwa Tanzania ambao umepata ufaulu wa takriban asilimia 91.1.


Soma zaidi: 


Mikoa mingine katika orodha 10 bora mwaka huu ni Kilimanjaro wenye ufaulu wa asilimia 88.84, Iringa (asilimia 88.59) na Kagera wenye asilimia 88.28.

Morogoro wenye shule 883 wenyewe kwa mujibu wa Dk Msonde umefaulisha watoto 45,457 kati ya 52,121 waliofanya mitihani hiyo mapema Oktoba mwaka huu na kuifanya kuwa na ufaulu wa asilimia 87.21 katika nafasi ya nane.

Majirani zao Pwani wao wameshika nafasi ya tisa baada ya kupata ufaulu wa asilimia takriban 87 baada ya kufaulisha wanafunzi 30, 212 kati ya 34,732 waliofanya mitihani hiyo ya kuhitimu elimu ya msingi.

Dk Msonde ameutaja Mwanza kuwa ndiyo mkoa wa 10 kitaifa katika matokeo ya mwaka huu baada ya kupata ufaulu wa asilimia 86.71 ukiwa bado juu ya wastani wa ufaulu wa kitaifa.

Enable Notifications OK No thanks