Mfumuko wa bei washuka baada ya ‘kuganda’ kwa miezi miwili Tanzania
- Washuka baada ya kung’ang’ania katika kiwango cha asilimia 3.1 kwa miezi miwili mfululizo.
- Umeshuka hadi asilimia 3 kwa mwaka ulioishia Novemba 2020 kutoka asilimia 3.1 iliyorekodiwa Oktoba mwaka huu.
- Umechagizwa na kupungua kwa gharama za bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.
Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Novemba 2020 imeshuka baada ya kung’ang’ania katika kiwango kimoja kwa miezi miwili mfululizo, ikichagizwa na kupungua kwa gharama za bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.
Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini Tanzania imeshuka hadi kufikia asilimia 3 kwa mwaka ulioishia Novemba 2020 kutoka asilimia 3.1 iliyorekodiwa Oktoba mwaka huu.
Kushuka kwa mfumuko wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Novemba 2020 kumekuja baada ya kasi yake kung’ang’ania katika kiwango kimoja kwa miezi miwili mfululizo.
Mwezi uliopita NBS ilieleza kuwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Oktoba 2020 ulikuwa asilimia 3.1 ikiwa ni sawa kabisa na kiwango kilichorekodiwa katika mwaka ulioishia Septemba 2020.
Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
Zinazohusiana:
Ripoti ya mfumuko wa bei ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) iliyotolewa leo Desemba 8, 2020, imeeleza kuwa kushuka kwa mfumuko wa bei kumechangiwa na kupungua kwa mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula ikilinganishwa na Oktoba mwaka huu.
Kwa bidhaa za vyakula na vinywaji, mfumuko wa bei umeshuka hadi asilimia 3.7 kutoka asilimia 4.4 kama ilivyorekodiwa Oktoba 2020.
