Airtel, DSE wazindua programu mpya ya kuuza, kununua hisa Tanzania

February 16, 2021 1:40 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • App hiyo inayojulikana kwa jina la ‘Hisa Kiganjani’ imeanzishwa kwa lengo la kurahisisha shughuli za uwekezaji zinazochangamana na soko la hisa.
  • Inawapa nafasi wateja wa Airtel Money uwezo wa kufungua akaunti zao za biashara, kununua na kuuza hisa, na kupokea malipo kupitia akaunti zao.

Dar es Salaam. Kampuni ya simu ya Airtel Tanzania kwa kushirikiana na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) wamezindua programu maalum ya simu inayowapa nafasi wateja wa Airtel Money uwezo wa kufungua akaunti zao za biashara, kununua na kuuza hisa na kupokea malipo kupitia akaunti zao.

App hiyo inayojulikana kwa jina la ‘Hisa Kiganjani’ imeanzishwa kwa lengo la kurahisisha shughuli za uwekezaji za soko la hisa huku ubunifu huo ukilenga kuongeza ufanisi wa kibiashara kwa wawekezaji wa soko hilo.

Aidha, app hiyo inatarajiwa kuongeza wawekezaji wapya ambao kwa sasa hawapati huduma kwa sababu ya kutopatikana kwa jukwaa la biashara la dhamana ya DSE.

“Jukwaa la ‘DSE Mobile Trading’ ni alama mpya ya kuboresha uzoefu kwa wawekezaji. Mteja anaweza akafungua akaunti ya biashara ya Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), akanunua au kuuza hisa pamoja na kupokea malipo,” amesema Mkurugenzi wa Airtel Money Isack Nchunda katika uzinduzi wa app hiyo jijini Dar es Salaam Februari 16

Wateja wa Airtel Money wanaweza kupata huduma hizo kwa kupiga *152*00# na kisha kuchagua “malipo ya serikali” na kisha DSE.


Zinazohusiana: 


Mkurugenzi wa Biashara  wa DSE Ibrahim Mshindo amesema Hisa Kiganjani inalenga kurahishisha kazi ya uwekezaji na wawekezaji kupitia upatikanaji wa moja kwa moja wa jukwaa la soko la hisa la DSE. 

“Ubunifu huu wa Hisa Kiganjani ni imani yetu kuwa utaongeza ufanisi zaidi kwenye biashara kwa wawekezaji waliopo na kuleta wawekezaji wapya, ambao kwa sasa hawakupata nafasi ya kununua hisa zaidi au kuhudumiwa kwa sababu ya kutopatikana kwa jukwaa kama hili la DSE,” amesema Mshindo. 

Jukwaa hilo linarahisisha upatikanaji wa bidhaa na huduma, kupunguza gharama za usafiri na upatikanaji wake kwa urahisi,  na kuongeza uwazi na usalama wa wawekezaji.

Kwa sasa, app hiyo inapatikana katika simu zinazotumia mfumo endeshi wa Android pekee ikiwa imepakuliwa na watu zaidi ya 5,000.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW