Maelfu wajitokeza kumuaga Maalim Seif Unguja

February 18, 2021 2:30 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link

Maelfu ya wananchi wamejitokeza Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad katika viwanja vya mnazi mmoja. Picha|Mtandao.


  • Ni katika safari ya kuusindikiza mwili wake katika kijiji cha Matembwe kisiwani Pemba ambako utapumzishwa.
  • Viongozi na wananchi wamejitokeza kwa wingi katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Unguja kumuaga.

Dar es Salaam. Mwili wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad umeagwa na maelfu ya Watanzania kisiwani Unguja, Zanzibar kabla ya kupumzishwa katika nyumba yake ya milele katika kijiji cha Mtambwe visiwani humo.

Ibada ya sala ya kumuombea marehemu iliyofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja, Unguja mchana wa leo Februari 18, 2020 imehudhuriwa na maelfu ya wakazi wa Zanzibar wa rika zote wakiongozwa na Rais Hussein Mwinyi.

Viongozi wengine ni pamoja na Makamu wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu wa CCM Taifa Dk Bashiru Ali, Rais Mstaafu wa Zanzibar Dk Aman Abed Karume, Makamu wa Rais mstaafu Dk Mohamed Gharib Bilal na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Mwili wa Maalim Seif uliwasili katika viwanja vya Mnazi mmoja ukitokea uwanja wa ndege wa Abeid Aman Karume ukisindikizwa na wanajeshi wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) ambapo  ulipokelewa na maelfu ya wananchi waliojipanga barabarani ikiwa ni ishara ya kuguswa na kifo hicho.

Katika viwanja hivyo wananchi wengi wamejitokeza kumsindikiza kiongozi wao ambapo alifanyiwa sala fupi na taratibu za kumsafirisha kuelekea Pemba zikafanyika ambako huko nako atafanyiwa sala kabla ya kupumzishwa katika nyumba yake ya milele katika kijiji cha Mtambwe.


Soma zaidi:


Enzi za uhai wake, Maalim Seif  aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za kiuongozi ikiwemo Waziri Kiongozi wa Zanzibar mwaka 1984 hadi 1988.

Mwaka 2010 hadi 2015, Maalim Seif ilitumika kama Makamu wa kwanza wa Rais Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK).

Pia aliwahi kuwa mwalimu wa kujitolea, huku akitumikia taifa kama Mwenyekiti wa Chama Cha ACT-Wazalendo, mwanachama wa Chama Cha Wananchi (CUF) na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Endelea kufuatilia Nukta Habari kwa ukaribu kupata taarifa zaidi kuhusu msiba huo wa kitaifa.

Enable Notifications OK No thanks