Magufuli avinyooshea vidole vyombo vya habari Tanzania
- Amesema vinatakiwa kutanguliza mbele uzalendo kwa Taifa.
- Awataka wanaotoa taarifa za uzushi mtandaoni kuacha.
- Watendaji Serikalini nao watakiwa kushirikiana na vyombo vya habari.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema Serikali inavihitaji sana vyombo vya habari vya Tanzania katika shughuli zake, lakini vinapaswa kujiepusha na habari za uzushi na kutanguliza mbele uzalendo kwa Taifa.
Dk Magufuli amesema wapo waandishi wa habari ambao hawatendi haki kwa habari wanazoripoti kwa sababu nyingine zinapotosha wananchi, huku baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wakiingia katika mtego huo.
“Pamekuwa na habari nyingi za uzushi zinatolewa. Siyo kwa waandishi wa habari tu kwa sababu wanaopost kwenye mitandao wengine wala sio waandishi wa habari. Tutangulize uzalendo wa taifa hili. Wajenga nchi ni sisi wenyewe na wabomoa nchi ni sisi wenyewe,” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli ametoa tahadhari hiyo wakati akizindua soko la Kisutu lenye ukubwa wa mita za mraba 11,938 lililopo Jiji la Dar es Salaam leo (Februrari 25, 2021) ambalo linatazamiwa kutoa ajira kwa vijana zaidi ya 2,000, nafasi za watu kuuzia bidhaa, migahawa na maegesho ya magari 40 kwa wakati mmoja.
Soma zaidi:
- Serikali yaahidi mazingira rafiki kuongeza idadi ya redio Tanzania
- Wanaomiliki redio Tanzania wapungua, televisheni wapaa
- Simu zachangia kushuka kwa redio majumbani Tanzania
Wakati akihutubia Watanzania, kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema “vyombo vya habari tunavihitaji sana lakini tutangulize uzalendo.”
Vyombo vya habari vimekuwa kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi kwa sababu vinatumika kutoa taarifa, kuelimisha, kuburudisha na kuendeleza uwajibikaji na uwazi katika matumizi ya rasimali za Taifa.
Aidha, Dk Magufuli katika hotuba yake amewaagiza watendaji wa Serikali kutoa ushirikiano pale wanahabari wanapokuwa wanahitaji taarifa kutoka kwao ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi kutoka serikalini.
“Upande wa serikali tuwe wepesi katika kutoa taarifa zilizo sahihi na upande wa vyombo vya habari navyo viwe vyepesi kutoa taarifa za ukweli bila kuweka chumvi lakini wakizingatia masilahi ya Taifa na uzalendo kwa taifa hili,” amesema Magufuli.

Latest