Alichokisema Dk Bashiru baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi
- Amesema amepokea uteuzi huo kwenye mitandao wakati akijiandaa kutekeleza majukumu ya chama.
- Awaomba Watanzania wamuombee akidhi matarajio ya imani aliyopewa na Rais Magufuli.
- Pia awaomba viongozi wa Serikali kushirikiana naye na kuwa waalimu wake.
Dar es Salaam. Katibu Mkuu Kiongozi mpya Dk Bashiru Ally amesema amepokea taarifa za kuteuliwa katika nafasi hiyo kwenye mitandao ya kijamii huku akiomba Watanzani wamwombee atimize matakwa ya kazi mpya na kuwa mwepesi wa kujifunza katika utumishi wake.
Rais John Magufuli alimteua Dk Bashiru Ally kuwa Katibu Mkuu Kiongozi na Balozi jana Februari 26, 2021 akichukua nafasi iliyoachwa na Balozi John Kijazi aliyefariki mwezi huu wa Februari 17 wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.
Dk Bashiru ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) akizungumza baada ya kuapishwa leo Ikulu jijini Dar es Salaam amesema taarifa za uteuzi huo zimemshtua kwa sababu amezipata kwenye mitandao ya kijamii wakati akijianda kwenda kutekeleza majukumu ya chama kwa mwezi mzima wa tatu.
“Jana jioni nilikuwa nasoma mafaili yangu, nikapata taarifa kwenye mitandao kwamba umeniteua. Mshtuko huo hauniwezeshi kusema mengi,” amesema Dk Bashiru ambaye aliwahi kuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Kutokana na nafasi aliyokabidhiwa, amemwahidi Rais Magufuli na Watanzania kuwa hatawaangusha katika kutimiza wajibu wake wa utumishi wa umma.
Amesema bado anatafakari ni jinsi gani atakadhi matarajio ya Rais na anamuomba Mungu amsaidie kama kiapo cha kazi yake kinavyotaka.
“Niwaombe Watanzania wote mniombee niweze kukidhi matarajio ya Mheshimiwa Rais, siwezi kusema mengi namshukuru Mungu anisaidie kama kiapo kinavyotaka,” amesema Dk Bashiru.
Kulingana na majukumu ya kazi yake hiyo mpya, hatakuwa mtu wa kuzungumza sana lakini atatumia muda mwingi kujifunza, kutenda kwa vitendo ili kutimiza majukumu yake kwa weledi na ufanisi.
“Sababu ya pili ni mila, maadili, miko ya kazi hii mpya, upande mmoja Balozi, upande mwingine Katibu Mkuu Kiongozi. Kwa mila, desturi, miiko na utamaduni wa kazi hizi si kazi za maneno, ni kazi za kusikiliza, kujifunza, kuchambua, kuamua na kutenda.
“Wale waliotegemea nitazungumza tena, nitazungumza kwa hadhari na umakini kwa sababu kiapo mmekisikia ni katiba, ni sheria, ni taratibu, ni mila, ni desturi, nakuahidi Mheshimiwa Rais sitakuangusha,” amesisitiza kiongozi huyo.
Soma zaidi:
- Safari ya mwisho ya Maalim Seif kuhitimishwa leo Zanzibar
- Magufuli, Watanzania wamlilia Maalim Seif
- Balozi Kijazi kuzikwa Tanga, wengi wakimlilia
Amewaomba viongozi wa Serikali hasa Makatibu Wakuu na Mawaziri kuwa walimu wake na kumpa ushirikiano na yeye atakuwa mwanafunzi mwepesi wa kujifunza.
Kwa utaratibu wa Tanzania, Katibu Mkuu Kiongozi ndiye Katibu Mkuu wa Rais ambapo anayeshika cheo hicho anakuwa Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Rais, Mkuu wa Utumishi wa Umma na Katibu wa Baraza la Mawaziri.
Pia miongoni mwa majukumu yake ni pamoja na kumshauri Rais kuhusu masuala yahusuyo utumishi wa umma, kuandaa vikao vya Baraza la Mawaziri na kutunza rekodi za vikao hivyo.
Dk Bashiru anakuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa tisa tangu nchi ipate uhuru ambapo mtu wa kwanza kupata nafasi hiyo alikuwa Dunstan Omar ambaye aliishikiria kati ya mwaka 1962 hadi 1964.