Majaliwa: Rais wenu yuko imara, anafanya kazi zake kama kawaida ofisini
- Amewataka Watanzania kuwapuuza watu wanaosambaza taarifa za chuki na uongo kuhusu afya ya Rais John Magufuli.
- Mtendaji huyo mkuu wa Serikali amesema Rais yuko imara na anaendelea majukumu yake ofisini.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Rais John Magufuli Rais yuko imara na anaendelea na majukumu yake ofisini huku akiwata Watanzania kuondoa hofu juu ya taarifa zinazosambawa mitandaoni zikidai kuwa kiongozi huyo wa juu wa nchi anaumwa.
Kauli hiyo ya Majaliwa imekuja wakati kukiwa na tetesi kwenye mitandao ya kijamii baada ya baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa na vyombo vya habari vya kimataifa kuhoji alipo Rais Magufuli kutokana na kutoonekana hadharani tangu Februari 27 mwaka huu alipomuapisha Katibu Mkuu Kiongozi mpya Dk Bashiru Ally, Ikulu jijini Des Salaam.
Majaliwa amesema kuwa kuanzia juzi hata leo asubuhi ameona “Watanzania wenye husda tena hawako ndani wako huko wanashawishi vyombo vya habari vya kimataifa viseme Rais wa Tanzania anaumwa, kajifungia.”
“Hizo ni chuki tu, husda tu,” Majaliwa amesema leo Machi 12, 2021 mkoani Njombe baada ya kushiriki swala ya Ijumaa katika msikiti mkuu wa mkoa.
Amewataka Watanzania kuwa watulivu kwa sababu Serikali inafanya kazi na wapuuze taarifa za uzushi kuhusu afya ya Rais Magufuli.
“Kumzushia ugonjwa ni chuki. Niseme wewe unaumwa! Inasaidia nini? Atoke! Aende wapi? Aende nje! Afanye nini? Uliwahi kumkuta Rais anadhurura Kariakoo, uliwahi mkuta Magomeni anazunguka?,” amesema Majaliwa huku akibainisha kuwa rais ana ratiba nyingi na hatoki hadharani kila mara.
Amesema Rais hawezi kuzunguka nchi nzima na ndiyo maana ana wasaidizi ambao wanamsaidia kutekeleza majukumu mbalimbali wakati yeye akiendelea na shughuli nyingine za ofisini.
Soma zaidi:
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka Watanzania kuwaombea viongozi wakuu wa nchi kwani wana dhamana kubwa ambayo wamepewa ya kuwatumikia.
”Tuendelee kufanya ibada na kupata mawaidha yanayohamasisha amani na utulivu. Rais Dk Magufuli ni mzima wa afya anaendelea na majukumu yake wakati sisi wasaidizi wake tukizunguka kuwahudumia wananchi. Leo nimezungumza naye na anawasalimia,” amesisitiza Majaliwa.