Hii ndiyo tofauti ya kompyuta za Mac, Windows

March 13, 2021 9:37 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Kompyuta hizo, hutofautiana kuanzia mifumo endeshi, utendaji kazi na hata miundo yake.
  • Pia, uwezo wa ulinzi pindi kompyuta inapovamiwa na virusi.

Dar es Salaam. Kufahamu kuwa unahitaji kununua kompyuta siyo kazi ngumu. Kazi huanza pale unapoingia katika duka linalouza bidhaa hiyo na kukutana na mamia ya kompyuta kiasi cha kushindwa kung’amua ni ipi itakufaa.

Mbali na utofauti wa bei, majina, uwezo wa uhifadhi kumbukumbu, mfumo endeshi na mengineyo mengi, kompyuta hutofautiana utendaji kazi na mara nyingi hiyo huchochewa na baadhi ya sifa zinazopatikana kwenye kompyuta husika. 

Kama ilivyo kwa simu janja, kuna simu zinazotumia mfumo endeshi wa Android (Samsung, HTC, Techno na kadhalika) na iPhone ambazo zinatumia mfumo endeshi wa IOS, pia kompyuta ziko katika makundi mawili yanayofahamika zaidi.

Makundi hayo ni kompyuta zinazotumia mfumo endeshi wa “Windows” na mfumo endeshi wa “macOS”.

Mtaalamu wa masuala ya teknolojia kutoka Media Crafters, Elias Maeda amesema, kompyuta zinazotumia mfumo endeshi wa Windows ni pamoja na Dell, Hp, Lenovo huku kompyuta za Apple Mac zikitumia mfumo endeshi wa macOS.

Nini kinatofautisha kompyuta hizi?

Njia za kuilinda kompyuta yako

Kwa kawaida, kompyuta nyingi huwa na njia mbili za ulinzi ikiwemo alama za vidole na msimbo almaarufu kama neno siri. Kwa kompyuta za daraja la juu zaidi za Windows ikiwemo HP Spectre 13, zinampatia mtumiaji uwezo wa kutumia alama za vidole, sura, neno siri la maneno na neno siri la namba kitu ambacho ni tofauti na kompyuta za Mac.

Kwa Mac, mtumiaji anaweza kuweka neno siri au kutumia saa ya Apple Watch au simu kuingia kwenye komyuta kama simu au saa zipo karibu na kompyuta.

Kwa mdau ambaye anahitaji kuwa na machaguo zaidi ya kuilinda kompyuta yake, huenda akafurahia kufungua kompyuta kwa sura, alama za vidole na kadhalika kama inavyotolewa na baadhi ya komyuta za Windows.

Hakuna kompyuta ya Mac ambayo inaweza kutumika kwa kushika skrini (touch screen). Picha| Notebookcheck.

Programu tumishi zinazokuja na kompyuta yako

Mara nyingi unaponunua kompyuta, utakuta ina programu tumishi zilizopakiwa tangu utengenezwaji wake. Programu hizo ni pamoja na sehemu ya picha (gallery) programu za kuhariri picha, kamera na kadhalika.

Kwa kompyuta za Windows, nyingi huongeza programu zikiwemo Skype na zingine ambazo huenda watu hulazimika kupakia programu ambazo ni bora zaidi.

Tovuti ya pcmag imeandika kuwa kompyuta za Mac huambatana na programu nzuri zaidi zikiwemo programu za kuhariri video, programu za kusikiliza muziki kwa njia ya mtandao (streaming), na programu za kutengenezea muziki kitu ambacho ni tofauti kidogo na kompyuta za Windows.

Uwezo wa kutumika kwa namna tofauti 

Hakuna asiyependa kuwa na njia mbadala za kutumia kitu chake. Mfano, kuwa na kompyuta inayojikunja tofauti, kompyuta inayoweza kuondolewa kichapio (keyboard) na kadhalika. 

Kwa kompyuta za Windows, huenda zikawa zimeshinda katika hili kwani zipo ambazo unaweza kuzitumia kwa kubonyeza skrini yake (touch screen) huku zingine zikiwa na uwezo wa kukunjika kitofauti.

Jambo hilo ni gumu kwa kompyuta za Mac ambazo haziwezi kutumika kwa kubonyeza skrini.

Ni matoleo machache ya Mac ambayo huweza kuwekwa katika mkao wa nyuzi 180 huku kompyuta za Windows ikiwemo ya Lenovo Yoga, zinaweza kukunjika kwa namna tofauti tofauti huku HP Spactre ikimwezesha mtu kuitimia kwa kushika skrini (touch screen).


Soma zaidi:


Utofauti mwingine huu hapa

Maeda amesema zipo tofauti nyingine ambazo huenda kabla ya kununua inabidi mtu azingatie ikiwemo kichapio ambacho hutofautiana utendaji kazi.

Kichapio cha kompyuta za Mac kimetofautiana batani na hata mifumo ya mikato (shortcut) kama kunakiri (copy), kuweka (paste) na hata kunakili kwa kufuta (cut). 

Muundo huo wa kichapio unaweza kumpa changamoto mtumiaji katika siku za awali za matumizi yake hasa yule aliyezoea kutumia kompyuta za Windows.

“Hata jinsi ya kupakia na kufuta mifumo endeshi pia inatofautiana,” amesema Maeda.

Mbali  na hayo yote, Maenda amesema kompyuta za Windows huwa na changamoto kadha wa kadha ikiwemo usalama wa kumbukumbu za mtumiaji kwani ikilinganishwa na kompyuta za Mac, zina uwezo mkubwa wa kupata virusi vya kitehama (virus).

Pia, kompyuta za Mac ni za bei ghali ikilinganishwa na kompyuta zinazotumia mfumo endeshi wa “Windows”. Tofauti hiyo ya bei ni kwa sababu kompyuta za Windows zinazalishwa na makampuni mengi huku kompyuta za Mac zikizalishwa na kampuni moja ya Apple ya nchini Marekani. 

Unatumia kompyuta ya aina gani? 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW