Mambo bado: Serikali yasema agizo la Rais Samia halihusu kufungulia magazeti
- Ufafanuzi huo unawaweka njiapanda wadau wa habari ambao wamekuwa wakimpongeza Rais Samia kwa kuongeza uhuru wa habari.
Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuagiza mamlaka zinazosimamia tasnia ya habari kuvifungulia vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa, Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema agizo la kiongozi huyo wa juu lilihusu kufunguliwa kwa televisheni za mtandaoni pekee na si vyombo vingine vilivyofungiwa kisheria.
Kauli hiyo ya Msigwa inakuja baada ya kuwepo maswali lukuki yaliyoibuka tangu jana baada ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Hassan Abbasi kukieleza kituo cha televisheni cha Wasafi TV kuwa agizo hilo la Rais Samia lilihusu televisheni za mtandaoni pekee na kwamba wakipata maelekezo kuhusu magazeti watatekeleza.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameelekeza Televisheni za Mtandaoni (Online TV) tu ndio zifunguliwe na SIO vyombo vya habari vingine yakiwemo magazeti vilivyofungiwa kwa mujibu wa Sheria. Gerson Msigwa Msemaji Mkuu wa Serikali,” amesema Msigwa kwenye ukurasa wa Twitter wa ofisi yake.
Ufafanuzi huo wa Msigwa unazidi kuiweka njiapanda tasnia ya habari hasa baada ya wanahabari na taasisi nyingi jana kumpongeza Rais Samia kwa uamuzi huo wakieleza kuwa ulikuwa unaenda kuongeza uhuru wa habari nchini Tanzania.
Zinazohusiana:
Katika hotuba yake Jumanne hii, Rais Samia alisema “…nasikia kuna vyombo milivyofungia. Sijui ViTv vya mikononi vile, vifungulieni lakini wafuate sheria na miongozo ya Serikali.”
“Lakini vifungulieni tusiwape mdomo wa kusema tunabinya uhuru wa vyombo vya habari. Lakini mhakikishe kila mliyempa ruhusa ya kuendesha chombo cha habari anafuata sheria za Serikali na kanuni ziwe wazi,” alisema Rais Samia.
Wadau wengi wa habari walisema huo ni mwelekeo mzuri huku Jukwaa la Wahariri (TEF) likieleza kuwa maelekezo ya Rais Samia “yataleta ahueni kubwa katika uhuru wa wa vyombo vya habari na ule wa kihabari kwa ujumla.”
Hata hivyo, baadhi akiwepo mwanaharakati wa haki za binadamu na Mkurugenzi wa kituo cha televisheni ya mtandaoni Kwanza TV, Maria Sarungi pamoja na kupongeza walishauri mabadiliko ya sheria yangeyapa nguvu zaidi maelekezo hayo.
Kituo cha Kwanza TV ni miongoni mwa vyombo vya habari vilivyofungiwa ndani ya mwaka mmoja uliopita likiwemo gazeti mashuhuri la Tanzania Daima ambalo mamlaka zililifutia leseni kutokana na madai ya kuvunja sheria kwa kuandika habari za uongo na za kichochezi.
Latest