SI KWELI: Rais Samia atuma ujumbe wa kutatanisha kupitia ukurasa wake wa X

July 14, 2025 4:30 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link

Dar es Salaam. Katika siku za hivi karibuni, kumesambaa chapisho kwenye mitandao ya kijamii likiwa katika mfumo wa picha ya skrini (screenshot) inayodai kuonesha ujumbe uliotumwa kupitia akaunti rasmi ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwenye mtandao wa X (zamani Twitter).

Chapisho hilo lina maneno ya kutatanisha yanayomhusisha moja kwa moja Rais, likieleza: “Hata ukipiga kelele vip Lissu hawezi kutoka jela na simwachii ng’oo mpaka uchaguzi upite na hakuna kenge yoyote wala hata Mahakama haina uwezo wa kumuachia mpaka mimi Amiri Jeshi Mkuu niamue.”

Mbali na kusambazwa kwenye X, ujumbe huo pia umeonekana kwenye ukurasa wa Facebook unaojiita “ITV Tanzania Breaking News”, ambao si ukurasa rasmi wa kituo cha habari cha ITV.

Taarifa hiyo imezua mijadala mikubwa na taharuki miongoni mwa wananchi, huku wengi wakibaki na sintofahamu kuhusu ukweli na uhalali wa chapisho hilo.

UKWELI: Chapisho hilo ni feki – Halijatolewa na Rais Samia

Uchunguzi uliofanywa na Nukta Fakti umebaini kwamba chapisho hilo ni la kughushi. Hakuna ushahidi kuwa limetumwa na Rais Samia, na halipo kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa X.

Aidha, aina ya mwandiko (font) uliotumika kwenye chapisho hilo haulingani na ule unaotumika katika machapisho rasmi ya Rais au ya taasisi za Serikali. Hii ni dalili ya wazi kuwa ujumbe huo umetengenezwa kwa nia ya kupotosha umma au kueneza propaganda zenye lengo la kuchafua jina la uongozi.

Zaidi ya hapo, ITV haina ukurasa wa Facebook unaoitwa “ITV Tanzania Breaking News”. Ukurasa rasmi wa kituo hicho unajulikana kama “ITV Tanzania”. Kutumia jina linalofanana ni njia nyingine ya kupotosha wananchi kwa makusudi.

Katika vipindi vya siasa na kuelekea uchaguzi mkuu, taarifa za kughushi zinazotumia majina ya viongozi wakuu huwa nyingi na huenea kwa kasi. Taarifa hizi zinalenga kupotosha umma, kuchochea hisia, au kuvuruga amani ya nchi.

Tunatoa wito kwa wananchi wote watumie vyanzo rasmi kama ukurasa wa X wa Rais Samia, tovuti ya Ikulu, na vyombo vya habari vilivyosajiliwa. Wafanye uhakiki wa taarifa kwa kutumia majukwaa ya uhakiki kama Nukta Fakti. Tuwe makini na tuwe walinzi wa amani kwa kuchuja taarifa kabla ya kuzisambaza.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks