Serikali kuitua mzigo wa madeni, tozo ATCL Tanzania
- Litaendeshwa kimkakati ii liweze kujiendesha kwa ufanisi na kulipunguzia hasara.
- Serikali italitua mzigo wa madeni makubwa na kulipa ahueni ya baadhi ya tozo na kodi.
- Rais Samia amesema ATCL itafanyiwa marekebisho makubwa ili ijiendeshe kibiashara.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali yake itaendelea kulilea Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kimkakati ii liweze kujiendesha kwa ufanisi ikiwemo kulitua mzigo wa madeni makubwa na kulipa ahueni ya baadhi ya tozo na kodi.
Rais Samia ameliambia Bunge leo Aprili 22, 2021 jijini Dodoma kuwa hatakubali kuona ATCL inapata hasara licha ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali.
“Naposema kimkakati ni pamoja na kuangalia kutoa unafuu wa madeni na baadhi ya kodi na tozo kama inavyofanyika kwenye nchi nyingine ili liweze kukua na liweze kuweka mahesabu sawa,” amesema kiongozi huyo.
Hatua hiyo itaisadia ATCL kuweza kupunguza gharama ya matumizi na sahara inayoikabili.
Soma zaidi:
- Ripoti ya CAG: ATCL ilipata hasara ya Sh60 bilioni 2019-20
- Airbus yatundika daruga kutengeneza ndege za kifahari za Airbus A380 Superjumbo
- Mambo unayotakiwa kufanya ukifika mapema ‘Airport’
Hivi karibuni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere alisema ATCL ilipata hasara ya Sh60 bilioni katika mwaka wa fedha 2019/20 na kwamba miaka yote mitano pia ilipata hasara.
Rais amesema kwa sasa shirika linasomeka kuwa na hasara kwa sababu ya kurithi madeni ya nyuma.
“Tutajitahidi kusoma mwenendo wa biashara ya ndege ulimwenguni…hatutakubali kuona Shirika linaendelea kupata hasara baada ya uwekezaji mkubwa tuliofanya,” amesema na kuongeza kuwa wataenda kulifanyia uchambuzi wa kina na kuhakikisha kuwa watakaoachiwa kuliendesha ni wale wenye weledi na uwezo wa kuliendeleza.
Hata hivyo, Rais Samia hakuweka bayana kiwango cha madeni ambacho Serikali watayapunguza na aina za tozo ambazo ATCL inadaiwa.