Ubelgiji yaipatia Sh11.3 bilioni Serikali ya Tanzania
- Ni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji mkoani Kigoma.
- Mradi huo utasaidia wakazi wa Kigoma kuondolana na tatizo la maji.
Dar es Salaam. Huenda maisha ya wakazi wa Mkoa wa Kigoma yakaboreshwa zaidi siku za usoni baada ya Serikali kupata fedha zitakazosaidia katika utekelezaji wa miradi ya maji katika mkoa huo.
Serikali ya Tanzania imepokea nyongeza ya kiasi cha Euro milioni nne (Sh11.3 bilioni) kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji mkoani Kigoma kutoka Serikali ya Ubelgiji.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba amesema mradi huo ambao ulianzishwa kwa ajili ya wilaya zote sita za Mkoa wa Kigoma, mwanzoni ulitarajiwa kugharimu Euro milioni nane (Sh22.5 bilioni).
“Sasa hizi Euro milioni nne zitakwenda kuongezea na kufanya jumla ya Euro milioni 12 sawa na takribani Sh33 bilioni za kitanzania ambazo zitatumika kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa maji maeneo ya vijijini na mijini mkoani humo”, amesema Tutuba.
Tutuba aliyekuwa akizungumza katika hafla fupi ya utiaji saini wa mkataba wa marekebisho ya nyongeza ya mradi huo iliyofanyika jana Aprili 23 jijini Dodoma ameihakikishia Serikali ya Ubelgiji kuwa fedha hizo zitatumika kikamilifu na utekelezaji wa miradi hiyo utakamilika kwa wakati.
Zinazohusiana
- Unayoweza kufanya kudhibiti matumizi makubwa ya umeme nyumbani
- Mazoezi yanayoweza kuongezea ufanisi kazini
- Namna umeme vijijini unavyoweza kutumika kuchochea maendeleo
Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania, Peter Van Acker amesema Serikali ya nchi yake itaendeleza ushirikiano na Tanzania kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema anaamini mradi wa maji mkoani Kigoma utatatua changamoto ya maji mkoani humo na ameahidi kuwajibika katika masuala ya maji kama hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan ilivyosisitiza.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesema utekelezaji wa mradi wa maji mkoani Kigoma utanufaisha watu takribani 150,000.
Ameahidi kusimamia matumizi ya fedha hizo kikamilifu ili kuhakikisha malengo ya utekelezaji wa mradi huo yanatimia kwa wakati.
Latest